Jumatatu 1 Septemba 2025 - 14:23
Nafasi ya Intidhari (Kusubiria Faraja) katika Utamaduni wa Kishia (Sehemu ya Kwanza)

Hawza/ Kile kinachomfanya mwanadamu awe na matumaini ya kuishi na kinachorahisisha kwake hofu na huzuni, ni intidhari (kusubiri) na matumaini ya mustakabali wenye mwanga na wa kustawisha, ambapo mahitaji yake yote ya kiroho na kimwili yatapewa majibu kwa ukamilifu

Shirika la Habari la Hawza - Furaha na mwamko wa mwanadamu katika kipindi chote cha maisha yake binafsi na ya kijamii, inatokana na neema ya “matumaini” na “intidhari”, ikiwa mwanadamu hatakuwa na matumaini ya mustakabali, maisha hayatakuwa na maana kubwa kwake, kile kinachompa mwanadamu matumaini ya kuishi, kukifanya kivutie na kukirahisisha kwake hofu na huzuni, ni intidhari na matumaini ya mustakabali wenye mwanga na kustawisha, ambapo mahitaji yake yote ya kiroho na kimwili yatapewa majibu kwa ukamilifu, mwanadamu, kwa msaada wa intidhari na matumaini haya, huvumilia tabu na matatizo na kuendelea na safari yake ya maisha.

Shia, kutokana na kunufaika na mafundisho ya Ahlul-Bayt (a.s.), kumeyafanya matumaini haya na intidhari ya mustakabali kuwa taa ya mwongozo wake.

Maana ya Lugha na Istilahi ya “Intidhari al-Faraj”
“Intidhari” kwa lugha ina maana ya kutarajia na kusubiri(1). Lakini katika istilahi, maana yake ni kusubiri kudhihiri kwa akiba ya mwisho ya Mwenyezi Mungu na kujiandaa kwa ajili ya kumnusuru katika kuanzisha serikali yenye uadilifu ulimwenguni kote.

Kwa maneno mengine, “intidhari” ni hali ya kisaikolojia inayozalisha utayarifu kwa kile kinachosubiriwa, na kinyume chake ni kukata tamaa na kukosa matumaini, kadiri intidhari inavyoongezeka na moto wake ukiwa mkali na wenye mwangaza zaidi, ndivyo harakati na mwamko wa mwanadamu, na hatimaye utayarifu wake, unavyoongezeka.(2)

“Faraj” maana yake ni “ufunguzi” au “wepesi baada ya dhiki”. Intidhari ya faraj inatokana na fitra ya mwanadamu mwenye kutafuta ukamilifu, ingawa sababu nyingine pia zinaweza kuwa chimbuko la intidhari.

Kinyume na dhana ya baadhi kwamba fikra ya Mahdawiyya ni jambo lililobuniwa na Shia pekee, imani ya Mahdawiyya si mali ya wafuasi wa Ahlul-Bayt (a.s.) peke yao, bali ni sehemu muhimu ya itikadi za Kiislamu na moja ya masuala ya msingi katika kanuni za Kiislamu, ambayo imejengeka miongoni mwa makundi yote na madhehebu ya Kiislamu kwa mujibu wa bishara za Qur’ani Tukufu na mafundisho ya Mtume Mtukufu (s.a.w). Riwaya zinazomhusu Imam Mahdi (ajf) – kama zilivyopokewa katika vyanzo vya Kishia – pia zimepokewa katika vitabu vingi mashuhuri vya Ahlus-Sunna.

Kwa hivyo, imani ya ushindi wa mwisho wa nguvu ya haki na kusimikwa kwa thamani za kibinadamu kwa ukamilifu na kwa upeo mpana kupitia shakhsia tukufu ambayo katika riwaya za Kiislamu imetajwa kwa jina la “Mahdi”, inatokana na wahyi, hivyo, intidhari ya zama hizo, pamoja na kwamba ipo katika mkusanyiko wa imani za wafuasi wote wa dini za mbinguni, baina ya Waislamu pia ina umuhimu wa pekee.

Nafasi ya Intidhari katika Utamaduni wa Kishia
Katika uchambuzi mfupi, riwaya ambazo ndani yake pametajwa intidhari zinagawanyika katika makundi mawili:

1- Intidhari al-Faraj kwa maana ya jumla.

2- Intidhari al-Faraj kwa maana mahsusi.


Utafiti huu unaendelea....

Imenukuliwa kutoka kwenye kitabu kiitwacho: Darsname-yi Mahdawiyyat; kilichoandikwa na Khodamur'ad Salimiyan, huku ikifanyiwa mabadiliko kiasi.

1. Lughatnama-yi Dehkhoda, neno Intidhari.

2. Mikyalul-Makarim, juzuu ya 2, uk. 235.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha