Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, matini kamili ya ujumbe wa Mtukufu Ayatullah Makarem Shirazi katika Mkutano wa 21 wa Kimataifa wa Mahdawiyya ni kama ifuatavyo:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
Mwanzoni, ni wajibu kutoa shukrani na pongezi kwa waandaaji wote na washiriki wa mkutano huu uliopambwa kwa jina la Mtukufu Walii wa Zama, Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake kutukufu. Natumaini programu hii itafikia malengo na makusudio yake, na iwe hatua yenye manufaa katika kuwafahamisha watu na kueneza utamaduni wa Mahdawiyya katika jamii ya Kiislamu.
Ingawa imani juu ya kudhihiri kwa Mwokozi haimhusu Waislamu pekee, bali pia wafuasi wa dini nyingine za mbinguni wanaamini jambo hili, hata hivyo fikra hii haijapewa uzito na kutiliwa mkazo katika madhehebu yoyote kama ilivyo katika madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s.), wala haijawasilishwa kama fikra ya msingi kama ilivyo hapo.
Fikra ya Mahdawiyya na umuhimu wa haja ya Mwokozi ni mwendelezo wa nafasi ya Uimamu na ulazima wa kuwepo kwake katika jamii ya wanadamu; kwa kuwa bila Imam, njia ya uongofu hupotea na wanadamu hupata madhara katika kufikia furaha na ufanisi wa kweli. Kwa sababu hiyo, imani juu ya nafasi ya Imam na itikadi ya Uimamu inaweza kuhesabiwa kuwa ndiyo sifa kuu kabisa ya Ushia.
Dhuluma, uonevu na machafuko tunayoyaona leo duniani huenda yakawa hayajawahi kushuhudiwa kwa kiwango kama hiki, na sababu kuu yake—hasa katika eneo hili—ni kuwepo kwa utawala haramu na dhalimu wa Kizayuni pamoja na wanaouunga mkono.
Maafa makubwa ya Ghaza na Lebanon, pamoja na mashambulizi dhidi ya nchi ya Iran, hayajifichi kwa yeyote. Bila shaka, kile kinachotufanya tusimame imara dhidi ya utawala huu unaomwaga damu ni imani na yakini juu ya kuwepo kwa nguvu iliyo juu na inayotawala nguvu zote za kibinadamu. Kukuza imani na matumaini haya huweka msingi wa kulea subira ya kweli.
Kumtambua adui na kufahamu mipango yake, hila zake na njia zake za kupenyeza, husababisha kushindwa kwao katika kuuzima mwanga wa imani juu ya kudhihiri kwa Mwokozi na kuangamiza utamaduni wa kusubiri.
Bila shaka, kushughulikia vipengele mbalimbali vya tukio la kudhihiri—kama vile ukweli wa kusubiri faraja, maandalizi kwa ajili ya kudhihiri, sifa za dola ya Mahdi, na kwa ujumla kila jambo linaloongeza uelewa na basira ya Mashia na kwa jumla Waislamu kuhusu suala hili—ni kazi yenye thamani kubwa na inayostahili pongezi.
Mwisho, kwa mara nyingine tena, sambamba na kuwashukuru waandaaji wote wa mkutano huu na washiriki wake waheshimiwa, namuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu ailinde Iran katika usalama na heshima, na awape wananchi wetu wapendwa afya na amani. Natumaini kuwa hadi wakati wa kudhihiri, ardhi hii itaendelea kuwa kituo cha wapenda, wanaosubiri na Mashia wa Mtukufu Walii wa Zama—roho zetu ziwe fidia kwake. Insha’Allah.
Amani iwe juu yenu na rehema za Mwenyezi Mungu.
Naser Makarem Shirazi
2026/02/13
Maoni yako