Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, kazi hii ya kipekee na ya kushangaza inajumuisha vipande 302 vya maandishi (scrolls) vya pande mbili, ambapo kila kipande kina urefu wa mita 4 (futi 13) na upana wa mita 1.5. Karatasi zilizotumika, ambazo zinafanana kwa sifa na karatasi ya ngozi (parchment) yenye uzito mkubwa, zilitengenezwa kwa agizo la Ustadh Zaman kwa mchanganyiko wa vifaa vya jadi, vikiwemo mayai, wanga wa mahindi na shaba ya alum, uasili wa mchanganyiko huu na na ukweli kwamba karatasi hizi zimetengenezwa kwa mikono, umeifanya nakala hii ya Qur’ani Tukufu iliyoandikwa kwa mkono kuwa ya pekee sana.
Nakala hii ya Qur’ani Tukufu inahifadhiwa katika makumbusho ya msikiti mmoja katika mji wa Istanbul. Msanii huyu mwenye umri wa miaka 54, katika mahojiano yake na shirika la habari la Associated Press, alisema:
“Kila ninapoifikiria Qur’ani hii, hunijia hisia nzuri sana; kwamba Mwenyezi Mungu Muweza alinipa uhai, roho na kipaji cha kisanaa ili niweze kuanza kazi hii na kuikamilisha. Sasa ninajihisi mwenye fahari.”
Bw. Zaman aliongeza kuwa; akiwa na umri wa takribani miaka 12, alipofahamiana kwa mara ya kwanza na sanaa ya hati nchini Iraq, alianza kuipenda sanaa ya uandishi wa Kiislamu.
Alisema: “Sanaa ya khati ilinivutia sana; nilihisi kwamba ninaweza kuipata roho yangu ndani yake, na kazi hii ni kioo kinachoakisi uwepo wangu.”
Kila ukurasa wa nakala hii ya maandishi ni wa kuandikwa kwa mkono kikamilifu, na kwa mujibu wa maelezo ya Ustadh Zaman, kwa muda wa miaka sita alikuwa akijishughulisha na kuandika na kunakili Qur’ani Tukufu kuanzia machweo ya alfajiri hadi machweo ya jua, katika chumba kidogo alichotengewa ndani ya Msikiti wa Mehrmah Sultan mjini Istanbul.
Chanzo: ABC NEWS
Maoni yako