Jumapili 20 Aprili 2025 - 20:13
Sifa za Imam; “Isma” (Kuhifadhiwa na kufanya makosa)

Hawza/ Kama Imam hato hifadhiwa kutokana na kukosea, basi itakuwa ni lazima kumtafuta Imam mwingine ili kukidhi mahitaji ya watu, na ikiwa naye pia hatakuwa salama kutokana na makosa, basi Imam mwingine tena atahitajika, na silsila hii itaendelea bila ya kikomo, jambo ambalo kwa mujibu wa akili, ni batili.

Shirika la Habari la Hawza - Mojawapo ya sifa muhimu za Imam na sharti la msingi la uimamu ni “Isma”, “Isma” ni sifa thabiti inayozaliwa kutokana na maarifa ya hakika na irada yenye nguvu, na Imam kwa sababu ya kuwa na viwili hivyo, hujiepusha kufanya dhambi au kosa lolote.

Imam, katika kutambua na kufafanua mafundisho ya dini, katika kuyatekeleza, na katika kutambua manufaa na madhara ya jamii ya Kiislamu, ni maasumu kutokana na kila aina ya kosa na upotofu.

Kwa ajili ya Isma ya Imam, kuna hoja za kiakili na za kinakili (kutoka Qur’ani na riwaya). Sababu kuu za kiakili ni kama zifuatazo:

1- Hifadha ya dini na njia ya uchamungu imo katika isma ya Imam; kwa kuwa Imam ana jukumu la kuhifadhi dini kutokana na upotoshaji na kuwaongoza watu kidini, si maneno yake tu, bali pia matendo yake na idhini au kutoidhinisha kwake matendo ya wengine, huathiri mwenendo wa jamii, kwa hivyo, lazima awe salama kutokana na makosa katika kuielewa dini na kuitekeleza ili awaongoze wafuasi wake kwa usahihi.

2- Moja ya sababu za haja katika jamii kwa Imam, ni kwamba watu hawako salama kutokana na makosa katika kuielewa dini na kuitekeleza. Sasa, ikiwa kiongozi wa watu naye pia si maasumu, atawezaje kuwa chimbuko la kuaminika kabisa kwao?! Kwa maelezo mengine, kama Imam hatakuwa maasumu, watu watakuwa na shaka katika kumfuata na kutekeleza maagizo yake yote.

Zaidi ya hayo, kama Imam hatakuwa salama kutokana na makosa, itabidi kumtafuta Imam mwingine ili ajibu mahitaji ya watu, na kama naye pia hatakuwa salama kutokana na makosa, Imam mwingine tena atahitajika, na mzunguko huu utaendelea bila ya kufika kikomo, jambo ambalo kwa akili, ni batili.

Aya za Qur’ani pia zinathibitisha ulazima wa isma ya Imam, na miongoni mwazo ni aya ya 124 ya Suratul Baqarah. Katika aya hii tukufu imesemwa kwamba baada ya daraja la unabii, Mwenyezi Mungu Mtukufu alimpa Nabii Ibrahim (as) daraja tukufu ya uimamu, kisha Nabii Ibrahim (as) alimwomba Mwenyezi Mungu aweke uimamu katika kizazi chake.

Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema:


«لَا يَنَالُ عَهْدِي الظَّالِمِينَ.»

Ahad yangu (Imamati) haipati madhalimu.

Yaani, nafasi ya uimamu ni maalumu kwa wale tu miongoni mwa kizazi cha Ibrahim (as) ambao si madhalimu.

Sasa, kwa kuzingatia kuwa Qur’ani Tukufu imehesabu kumshirikisha Mwenyezi Mungu kuwa ni dhulma kubwa, na vilevile aina yoyote ya kuvunja amri za Mwenyezi Mungu (= dhambi) kuwa ni dhulma kwa nafsi, basi yeyote ambaye katika kipindi cha maisha yake ametenda dhambi, ni miongoni mwa madhalimu na hastahili nafasi ya uimamu.

Kwa maneno mengine, bila shaka Nabii Ibrahim (as) hakuomba uimamu kwa ajili ya wale wa kizazi chake ambao katika maisha yao yote walikuwa watenda dhambi, au wale waliokuwa wema mwanzoni kisha wakawa waovu, Kwa hiyo, makundi mawili yanabaki:

1. Wale ambao mwanzoni walikuwa watenda dhambi kisha wakatubu na wakawa wema.
2. Wale ambao hawakuwahi kutenda dhambi yoyote kabisa.

Mwenyezi Mungu katika maneno yake, ameliondoa kundi la kwanza, matokeo yake ni kuwa daraja la Imamati ni maalumu kwa kundi la pili pekee.

Utafiti huu unaendelea…

Imenukuliwa kutoka katika kitabu “Negin ya Afarinsh”, huku ikifanyiwa mabadiliko kiasi.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha