Jumatano 15 Julai 2026 - 12:35
Marekani na Utawala wa Kizayuni Hawana Dhamira ya Kufanikisha Usitishaji Vita wa Kudumu

Hawza/ Mchambuzi wa masuala ya kisiasa amesema kuwa, utawala wa Kizayuni umeonesha tena kwamba hauheshimu makubaliano wala maazimio yoyote. Alisisitiza kuwa kuendelea kwa uvamizi na uharibifu wa vijiji vya kusini mwa Lebanon pamoja na mashambulizi ya hivi karibuni ya Marekani dhidi ya kusini mwa Iran ni ushahidi wa ukiukaji wa makubaliano yaliyopo, na iwapo hali hii itaendelea, eneo hilo litakabiliwa na mgogoro mpya na mpana zaidi.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Hasan Hani-Zadeh, mchambuzi wa masuala ya kisiasa, katika mahojiano na mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, akizungumzia maendeleo ya hivi karibuni kusini mwa Lebanon na Syria, alisema kuwa katika siku za karibuni ndege za kivita, ndege zisizo na rubani na vikosi vya kijeshi vya utawala wa Kizayuni vimefanya mashambulizi na kusonga mbele katika maeneo ya kusini mwa Lebanon. Aliongeza kuwa kwa sasa zaidi ya vijiji 180 vya kusini mwa Lebanon vimeharibiwa na kukaliwa kwa mabavu, jambo linaloonyesha kuwa makubaliano yoyote ya kisiasa, kiusalama au kijeshi na utawala wa Kizayuni hayana uhalali wa kweli, kwa kuwa utawala huo umethibitisha mara kadhaa kwamba hauzingatii makubaliano wala maazimio ya Umoja wa Mataifa.

Aliongeza kuwa, katika miezi ya karibuni kulifanyika duru tano za mazungumzo kati ya Serikali ya Lebanon na utawala wa Kizayuni chini ya usimamizi wa Marekani mjini Washington, na makubaliano yakatiwa saini. Hata hivyo, alisema kuwa Serikali ya Lebanon ndiyo iliyotekeleza makubaliano hayo, ilhali utawala wa Kizayuni umeendelea kuwaua wananchi wa kusini mwa Lebanon na kusonga mbele kuelekea kaskazini mwa Mto Litani.

Hani-Zadeh alisisitiza kuwa, uwepo wa Hizbullah kama nguvu ya kuzuia uchokozi wa utawala wa Kizayuni ni jambo la lazima kwa usalama na ulinzi wa Lebanon. Alisema kwa masikitiko kuwa Serikali ya Lebanon, bila kuzingatia matakwa ya wananchi, imechagua kunyamaza mbele ya uhalifu huo na imeizuia Hizbullah kukabiliana na utawala wa Kizayuni. Kwa mujibu wake, hali hiyo imeipa Israel nafasi ya kuendelea na uvamizi na mauaji ya wananchi wa kusini mwa Lebanon huku Serikali ya Lebanon ikishindwa kuzuia uchokozi huo.

Akizungumzia hali ya usalama na kibinadamu kusini mwa Lebanon, Hani-Zadeh alisema kuwa, kutokana na mashambulizi ya miezi ya karibuni, zaidi ya watu milioni moja wamekimbia makazi yao, na hali ya usalama pamoja na maisha ya kijamii katika eneo hilo, hasa karibu na Nabatieh, imezorota kwa kiwango kikubwa.

Aliendelea kusema kuwa; mashambulizi ya mizinga, ndege zisizo na rubani na mabomu ya angani vimewafanya wananchi washindwe kurejea katika makazi yao. Aliongeza kuwa kiwango cha uharibifu ni kikubwa sana na kwamba wala Umoja wa Mataifa, taasisi za kikanda au Serikali ya Lebanon hazijaweza kuzuia mashambulizi hayo.

Hani-Zadeh alisema pia kuwa; tahadhari ya hivi karibuni ya Sheikh Naim Qassem, Katibu Mkuu wa Hizbullah nchini Lebanon, inaweza kubadili mwelekeo wa hali ya mapambano. Hata hivyo, kutokana na makubaliano yaliyofikiwa kati ya Serikali ya Lebanon na utawala wa Kizayuni, Hizbullah hadi sasa haijapata nafasi ya kujihusisha kikamilifu katika kuwatetea wananchi wa kusini mwa Lebanon. Alibainisha kuwa kwa sasa vijiji 180 vimeharibiwa na kukaliwa kwa mabavu, huku sehemu kubwa ya wakazi wa kusini mwa Lebanon wakiishi katika mahema na barabarani katika eneo la Dahieh mjini Beirut.

Akizungumzia namna Hizbullah ilivyojibu mashambulizi hayo alisema kuwa, harakati hiyo inaendelea na mipango yake maalumu na inawatetea wananchi kwa uwezo wake wote, lakini uwepo wa Jeshi la Lebanon karibu na kile kinachoitwa "Mstari wa Njano", uliowekwa na utawala wa Kizayuni, umeifanya kazi ya Hizbullah kuwa ngumu zaidi.

Aliongeza kuwa, kwa sasa Hizbullah inafanya operesheni zake kwa mbinu za kivita za msituni na za kushtukiza kusini mwa Lebanon, lakini mazingira si kama yalivyokuwa hapo awali kwa sababu inajaribu kuheshimu makubaliano yaliyopo.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa iwapo hali hii itaendelea na Serikali ya Lebanon ishindwe kuhakikisha usalama wa wananchi wa kusini, Hizbullah italazimika kuingilia kati na kuwatetea wananchi hao.

Akirejelea mashambulizi ya hivi karibuni ya Marekani dhidi ya kusini mwa Iran, Hani-Zadeh alisema kuwa, maelewano yaliyokuwa yamefikiwa kati ya Iran na Marekani yamekiukwa kupitia mashambulizi hayo.

Aliongeza kuwa; kuendelea kwa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon, wakati moja ya matakwa makuu ya Iran ni kuondoka kwa utawala huo nchini Lebanon, kutakuwa na athari mbaya kwa utulivu wa eneo zima.

Hani-Zadeh alisisitiza kuwa sera za Marekani na utawala wa Kizayuni zinaendana kikamilifu, na lengo lao ni kuendeleza mgogoro katika eneo ili kufanya makubaliano yaliyosainiwa kati ya marais wa Iran na Marekani, ambayo yanaweza kuwa msingi wa amani ya kudumu, yasizae matunda. Aliongeza kuwa Iran inasisitiza kuwa usitishaji vita unapaswa kujumuisha eneo lote, ikiwemo kusini mwa Lebanon.

Kwa mujibu wa mchambuzi huyo, Marekani haijatekeleza ahadi zake zozote, huku Umoja wa Mataifa, kutokana na kuipendelea Marekani na utawala wa Kizayuni, ukishindwa kusimamia ipasavyo juhudi za kuleta amani ya kudumu.

Hani-Zadeh alisema kuwa, Benjamin Netanyahu anaona kuendelea kwake kubaki madarakani kunategemea kuhamisha mgogoro kutoka ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kwenda nje ya maeneo hayo, ndiyo maana anaendelea kujaribu kulifanya eneo zima libaki katika hali ya mvutano.

Aliongeza kuwa; hakuna sababu yoyote inayoweza kuhalalisha kuendelea kwa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa kusini mwa Lebanon baada ya kutiwa saini kwa makubaliano kati yake na Serikali ya Lebanon.

Akizungumzia nafasi ya nchi za eneo hilo, alisema kuwa mataifa kama Pakistan na Qatar yanaendelea kufanya juhudi za kupunguza mvutano na kuweka mazingira ya kurejea kwa usalama wa kiasi, lakini kutokana na kukosekana kwa dhamira ya kisiasa kutoka Marekani na utawala wa Kizayuni, juhudi hizo bado hazijazaa matunda.

Hani-Zadeh alisema kuwa, Donald Trump na Benjamin Netanyahu bado wanaendelea kutafuta namna ya kuongeza shinikizo dhidi ya Iran na Lebanon ili kupata manufaa zaidi. Hata hivyo, kutokana na jibu la hivi karibuni la Iran, Marekani italazimika kuelekea kukubali usitishaji vita wa kudumu; vinginevyo eneo hilo litashuhudia mapigano makubwa zaidi.

Mwishoni, alisisitiza kuwa; ikiwa Marekani kwa upande mmoja itaendelea kukiuka usitishaji vita kupitia mashambulizi yake dhidi ya kusini mwa Iran, na kwa upande mwingine utawala wa Kizayuni ukaendelea na uchokozi wake dhidi ya kusini mwa Lebanon, basi hakutakuwa na usitishaji vita wa kweli, na eneo hilo litaingia katika hatua mpya ya mgogoro ambao hautakuwa na manufaa kwa nchi yoyote ya eneo hilo.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha