Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Jumuiya ya Haki za Binadamu ya Bahrain, katika taarifa iliyotolewa baada ya kikao cha kwanza cha mahakama, ilizituhumu mamlaka za Bahrain kwa kufanya ukiukaji mkubwa wa sheria na haki za binadamu katika kesi ya wanazuoni 19 wa dini, wakiwemo washtakiwa wanane wanaohukumiwa bila kuwepo mahakamani, akiwemo Ayatullah Sheikh Isa Qassim.
Jumuiya hiyo ilisema kuwa, kauli zilizotolewa na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu kuhusu kesi hiyo zilikuwa na hukumu ya awali dhidi ya washtakiwa na zilikiuka kanuni ya dhana ya kutokuwa na hatia kabla ya kutolewa kwa uamuzi wowote wa mahakama.
Jumuiya hiyo ilieleza kuwa, kesi hii ni mwendelezo wa hatua zilizoanza tarehe 9 Mei 2026 (1 Ordibehesht 1405 Hijria Shamsia), wakati mamlaka zilipotangaza kukamatwa kwa watu 41, kisha zikachukua hatua mbalimbali dhidi yao, zikiwemo kuwaweka rumande, kutaifisha mali zao na kukagua akaunti zao za benki.
Jumuiya hiyo ilisema imebaini ukiukaji mbalimbali unaodhoofisha dhamana za kesi ya haki. Miongoni mwa ukiukaji huo ni matumizi ya lugha ya moja kwa moja na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu ya kuwataja watu kuwa magaidi kabla ya hukumu ya mahakama, pamoja na kuwasilisha simulizi rasmi kana kwamba ni ukweli uliothibitishwa. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hatua hizo zimeathiri uhuru wa mahakama na maoni ya umma, na zinapingana na viwango vya kimataifa vinavyohusu uhuru wa mahakama na kanuni ya kutokuwa na hatia.
Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa, mamlaka zimeunganisha imani za kidini na kisiasa, hususan dhana ya Wilayat al-Faqih, na vitendo vya uhalifu. Jumuiya hiyo ilisema; hatua hiyo ni sawa na kuhalalisha jinai dhidi ya uhuru wa fikra na imani, jambo linalokwenda kinyume na Katiba ya Bahrain pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa.
Aidha, Jumuiya hiyo ilikosoa kile ilichokiita "kuingiza siasa mapema katika kesi" kwa kuwahusisha washtakiwa na Iran kabla ya ushahidi kuwasilishwa mahakamani. Ilisisitiza kuwa; tuhuma kama hizo zinapaswa kujadiliwa ndani ya mahakama kwa mujibu wa taratibu za kisheria za kuthibitisha kosa, badala ya kutolewa kupitia taarifa za vyombo vya habari.
Katika sehemu ya utekelezaji wa kesi, Jumuiya hiyo ilieleza wasiwasi wake kuhusu baadhi ya washtakiwa kuwekwa kizuizini wakiwa wametengwa kabisa na dunia ya nje, hali inayoongeza hatari ya mateso na vitendo vya unyanyasaji. Pia ilieleza wasiwasi kuhusu kufanyika kwa kikao cha kwanza cha mahakama kwa njia ya mtandao, kutokana na hofu ya kutokuwepo kwa ushiriki wa maana wa mawakili wa utetezi na familia za washtakiwa.
Ripoti hiyo pia ilisisitiza kuwa, haki ya utetezi imekiukwa, ikieleza kwamba baadhi ya waliokamatwa walinyimwa mawasiliano ya kutosha na mawakili wao. Aidha, ilibainisha kuwa maungamo yoyote yaliyopatikana wakati mtuhumiwa amenyimwa msaada wa kisheria au akiwa chini ya shinikizo hayana uhalali wa kisheria.
Jumuiya ya Bahrain inaamini kuwa, kuonesha vitabu vya dini na mali zilizokamatwa kwa umma kama ushahidi wa "shughuli za kigaidi" kabla ya tathmini ya mahakama ni ukiukaji wa uhuru wa fikra na imani. Pia ilisema kuwa kuwafungulia kesi kwa pamoja wanazuoni wengi wakuu wa Kishia na kuhusisha taasisi zao za kidini na ugaidi kunaongeza wasiwasi kuhusu uwepo wa ubaguzi na kulengwa kwa misingi ya dini na madhehebu.
Jumuiya hiyo pia ilieleza wasiwasi kuhusu kuwafungulia kesi watu ambao tayari walinyang'anywa uraia wao, ikisema hali hiyo inapunguza uwezo wao wa kutumia haki za utetezi na kudhoofisha fursa ya kupata kesi ya haki.
Mwishoni, Jumuiya ya Haki za Binadamu ya Bahrain iliitaka Serikali ya Bahrain kuwaachilia mara moja wanazuoni wa dini waliokamatwa, kuheshimu kanuni ya kutokuwa na hatia, kuhakikisha kesi zinaendeshwa kwa haki na kwa mahakama huru, kuacha kuhalalisha jinai dhidi ya imani na shughuli za kidini za amani, na kusitisha matumizi ya kunyang'anya uraia kama chombo cha adhabu za kisiasa.
Vilevile, taasisi hiyo ililitaka Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa pamoja na Wataalamu Maalumu wa Umoja wa Mataifa wanaoshughulikia uhuru wa dini, imani na uhuru wa mahakama kufuatilia kesi hiyo na kuanzisha uchunguzi huru wa kimataifa kuhusu kile ilichokiita kuendelea kuwafuatilia na kuwashitaki raia kutokana na maoni na imani zao.
Maoni yako