Jumatano 15 Julai 2026 - 15:35
Wananchi Kuwepo Uwanjani ni Miongoni mwa Vielelezo vya Nusura ya Mwenyezi Mungu/ Marekani na Israel Wamedhalilika Mbele ya Iran

Hawza/ Ayatullah Jawadi Amuli amesema kuwa; hakuna aliyedhani kwamba kwa miezi kadhaa wanawake na wanaume wangekuwa na uwepo mkubwa kiasi hicho katika maeneo mbalimbali na kuwa watetezi wa Mapinduzi ya Kiislamu na Uislamu. Alisisitiza kuwa, pamoja na mchango mkubwa wa Kiongozi Shahidi, uwepo wa wananchi barabarani haupaswi kubezwa kwa kuwa ni miongoni mwa vielelezo vya nusura ya Mwenyezi Mungu.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Mkuu Jawadi Amuli, siku ya Jumatatu, alipokutana na kundi la wazalishaji na wafadhili wa shughuli za kheri, aliwashukuru kwa juhudi zao katika uzalishaji na huduma za kijamii. Alisema kuwa, ushindi na mafanikio ya Mapinduzi ya Kiislamu viametokana na imani ya wananchi, uongozi wa Mwenyezi Mungu na juhudi za dhati za wapigania haki.

Alisema: "Mwenyezi Mungu wakati mwingine huiokoa dini Yake kwa msaada wa ghaibu, na wakati mwingine kupitia uwepo wa wananchi. Hakuna aliyedhani kwamba kwa miezi kadhaa wanawake na wanaume hawa wangekuwepo mitaani kwa namna hii na kuwa watangazaji wa Mapinduzi na Uislamu. Ingawa Kiongozi wetu mpendwa alifanya kazi kubwa, kisha akanywa sharbati ya ushahidi na akaondoka duniani akiwa shahidi, lakini pia hatupaswi kudharau harakati hizi za wananchi na uwepo wao."

Israel na Marekani Wamedhalilika Mbele ya Iran

Ayatullah Jawadi Amuli, akizungumzia mabadiliko yaliyotokea katika miongo ya hivi karibuni, alisema: "Zamani nchini Iran haikuwezekana hata kufanya kikao cha dua kwa ajili ya ushindi wa Waislamu dhidi ya utawala wa Kizayuni. Lakini leo, kwa baraka za Mapinduzi za Kiislamu, kusimama imara kwa wananchi, kujitolea kwa mashahidi na kutegemea nguvu za Mwenyezi Mungu, Israel na Marekani wamedhalilika mbele ya Iran."

Litumikieni Taifa kwa Ari ya Jihadi na Dhamira ya Juu

Akikumbusha miaka ya mwanzo ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuanzishwa kwa mfumo wa mahakama wa Jamhuri ya Kiislamu, Ayatullah Jawadi Amuli alisisitiza umuhimu wa kulitumikia taifa kwa ikhlasi bila kutarajia maslahi ya kidunia.

Alisema: "Katika mwanzo wa Mapinduzi, majukumu mengi mazito yalitekelezwa kwa uwezo mdogo sana na bila matarajio ya faida za kifedha. Katika mfumo wa mahakama kulikuwepo watu wakubwa waliobeba jukumu hilo kwa ikhlasi na ari ya jihadi bila kutarajia chochote. Hivyo hata leo inawezekana kuwatumikia wananchi kwa roho hiyo hiyo."

Tulishinda Vita vya Miaka Minane kwa Ushujaa wa Wananchi

Ayatullah Jawadi Amuli alisema kuwa usalama na heshima ya Iran ya leo ni matokeo ya kujitolea kwa watu waliotoa maisha yao kwa ajili ya kulinda Uislamu, Iran na heshima ya taifa.

Alisema: "Tulikuwa na wapendwa ambao katika baridi kali ya Kurdistan walibaki wakilinda ngome zao kwa uthabiti hadi wakaganda kwa baridi na wakapata shahada. Miili yao ilipoletwa katika Msikiti Mkuu wa Qom, kwa kawaida katika vikao vya maombolezo tunasoma Qur'ani na Al-Fatiha na kuondoka mapema, lakini usiku huo nilibaki hadi mwisho wa kikao nikilia; si kwa ajili ya thawabu, bali kwa sababu ya aibu. Tunapaswa kutambua kuwa katika vita vya miaka nane hatukuwa na vifaa vya kutosha, bali tulishinda kwa ujasiri wa kimungu uliokuwamo kwa wananchi."

Kuwa na Dhamira ya Juu katika Kumtumikia Mwenyezi Mungu na Jamii

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, alisisitiza umuhimu wa kuwa na malengo makubwa na kuwajibika mbele ya dini na jamii.

Alisema: "Kamwe tusiwe watu wa kulalamika. Tunapaswa kuwa na dhamira ya juu, kwa kuwa tunaweza kuwa wawakilishi na makhalifa wa Mwenyezi Mungu duniani. Daima tumuombe Mwenyezi Mungu tukisema: Wewe unayeilinda dini Yako, kwa nini isiwe kupitia mimi?"

Kisha akasoma dua:

«اللَّهُمَّ اجْعَلْنِی مِمَّنْ تَنْتَصِرُ بِهِ لِدِینِکَ... وَلَا تَسْتَبْدِلْ بِی غَیْرِی»

na kueleza kuwa muumini anatakiwa kumuomba Mwenyezi Mungu amfanye kuwa chombo cha kuinusuru dini Yake na atamani daima kuwa miongoni mwa wanaowatumikia waja wa Mwenyezi Mungu, badala ya jukumu hilo kupewa mtu mwingine.

Umuhimu wa Kukuza Utamaduni wa Kazi, Uzalishaji na Huduma kwa Jamii

Ayatullah Jawadi Amuli pia alisisitiza umuhimu wa kukuza utamaduni wa kufanya kazi, uzalishaji na kuwahudumia wananchi. Alisema umaskini ni miongoni mwa matatizo makubwa zaidi ya kijamii.

Akinukuu kauli ya Amirul-Muuminin Ali (as), alisema:

«هیچ تازیانه‌ای دردناک‌تر از فقر نیست»

na kueleza kuwa kila mmoja ana wajibu, pamoja na kueneza maadili ya dini, kujitahidi kupunguza umaskini, kuwasaidia wahitaji, kuimarisha uzalishaji na kuongeza ajira ili kusiwe na familia yoyote inayorudi nyumbani mikono mitupu na ikiwa na fedheha.

Mwishoni mwa mkutano huo, Marjaa huyo alimuomba Mwenyezi Mungu awajalie wote wanaolitumikia jamii ya Kiislamu kheri, mafanikio na uongofu, pamoja na kuwapa uelewa wa kina, uwezo na busara nyingi.

Msichoke Kuwatumikia Wananchi

Akihitimisha hotuba yake, Ayatullah Jawadi Amuli alisema:

"Msiruhusu maneno ya watu yawatoe katika uwanja wa huduma, wala msichoke kamwe. Daima mwelekeo wenu mkuu uwe kwa Mwenyezi Mungu; zungumzeni Naye na fanyeni kazi kwa ajili ya radhi Zake."

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha