Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sheikh Issa Qassim, akilisifu tukio la mazishi makubwa ya Imam Shahidi Sayyid Ali Khamenei yaliyofanywa na wananchi wa Iraq, aliwaambia wafuasi wa Shahid Sadr na Marjaiyya Tukufu ya Iraq:
"Enyi wana wa Shahid Sadr, na enyi wana wa Marjaiyya Tukufu ya Iraq! Katika mapokezi haya makubwa, yenye utukufu na yenye kugusa hisia, pamoja na kumuaga na kumsindikiza kiongozi huyu mkuu na mshindi wa Uislamu, mmetekeleza wajibu wenu ipasavyo kwa ajili ya Uislamu, kwa ajili ya hali ya sasa, mustakabali, hadhi, dunia na Akhera yenu."
Alisisitiza kuwa; yaliyoshuhudiwa yalikuwa mapokezi ya mamilioni ya watu, yenye utukufu na yaliyojaa roho ya kweli ya Wilaya kwa Mwenyezi Mungu, dini Yake na Mtume Mtukufu (saww).
Ujumbe wa Ayatullah Sheikh Issa Qassim:
Kwa Jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.
Ewe Mwenyezi Mungu! Mrehemu Muhammad na Aali zake.
Mapokezi ya Iraq yenye imani, heshima na ushujaa kwa Ayatullah Mtukufu, Imam Sayyid Ali Khamenei, baada ya kuuawa kwake kishahidi kwa heshima katika njia ya Mwenyezi Mungu, ilhali hadi pumzi yake ya mwisho alikuwa katika jihadi kubwa ya kuinua dini, kulinda heshima ya Waislamu, kuvunja nguvu za madhalimu na mabeberu, kuwasaidia waliodhulumiwa na kulinda utu wa mwanadamu pamoja na uhuru safi, mtukufu na wenye kujenga, yalikuwa mapokezi makubwa sana.
Sherehe hiyo ilikuwa mapokezi ya mamilioni ya watu, yenye utukufu na yaliyojaa roho ya kweli ya Wilaya kwa Mwenyezi Mungu, dini Yake, Mtume Wake Mteule na Ahlul-Bayt wake watoharifu (as), pamoja na kuwafuata warithi wao miongoni mwa Marajii wakubwa, Mafaqihi waongozaji, wanazuoni wema, walinzi wa dini na heshima ya waumini, na wabeba bendera ya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu waliopigania kutawala kwa neno la haki duniani na kuwaokoa wanadamu kutoka katika makucha ya madhalimu na mabeberu.
Mapokezi haya yalikuwa ni sauti ya wazi ya roho ya kujitolea na kujitoa muhanga kwa ajili ya "kadhia kuu ya Tawhid", ambayo ndiyo siri ya kila uongofu, uimara, heshima, utu, ushindi, uadilifu, usalama, amani, maadili mema na ihsani. Pia yalidhihirisha kiwango cha juu cha utambuzi wa kina, mwamko wa kisiasa, uwezo sahihi wa kutambua mambo, na yalisisitiza udugu wa kweli wa kibinadamu unaofungua njia ya kushirikiana kwa manufaa ya wote.
Mapokezi haya yaliweka mkazo mkubwa juu ya uchaguzi sahihi wa nguzo muhimu zaidi inayolinda mfumo wa jamii dhidi ya upotovu, ufisadi, machafuko, unyonyaji, kusambaratika na udhaifu; nayo ni kumchagua kiongozi mwenye elimu, mwenye ujuzi, mwenye uwezo na aliyejaa uchamungu, heshima, usafi wa nafsi na aliyejitenga na udhalili, batili na matamanio ya kidunia.
Huu ndio mfano ambao Mwenyezi Mungu Amewaongoza nao waja Wake; kwamba kiongozi wa jamii awe Mtume wa Mwisho (saww), na baada yake Maimamu Maasumu (as) kutoka katika kizazi chake, na wakati wa ghaiba ya Imam Maasumu, watu walio bora na wanaostahili washike usukani wa uongozi.
Mapokezi haya, ambayo kwa ukubwa wake na ushiriki wa mamilioni ya watu yalivuta macho ya ulimwengu mzima, yalitoa wito kwa mataifa kwamba Wilaya ya Umma kwa uongozi wake – ambayo Mwenyezi Mungu Ameifanya kuwa rehema kwa Umma – ni Wilaya kwa kielelezo chema kilichokamilisha masharti ya Mwenyezi Mungu katika kiwango cha juu kabisa, iwe katika uwepo wa Imam Maasumu au wakati wa ghaiba. Ni Wilaya ambayo inaendelea kwa kuendelea kwa uongozi mwema, wala haiwi dhaifu, bali hubakia hai, madhubuti na tayari kujitolea daima.
Mapokezi haya yanasimulia kwa nguvu zote mafunzo na miongozo kwa ajili ya sasa na siku zijazo; mafunzo ambayo kila zama na kila mahali yanahitajika.
Mapokezi haya yanapaza sauti yakisema: "Unganeni na machozi yao, sauti zao, ishara zao, dua zao, ahadi zao na tahadhari zao. Sisi sote ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu, wasaidizi wa dini Yake na wasaidizi wa uongozi Anaouridhia. Hatutabadilisha njia hii kwa kitu chochote wala hatutatafuta mbadala mwingine isipokuwa Mwenyezi Mungu. Hii ndio dhamira ambayo tunaishikilia kwa imani ya kweli na ya dhati, na itaendelea kuwa lengo letu maadam tuko hai."
Sisi sote – wanaume na wanawake, wazee na vijana, balehe na watoto – hii ndio dhamira yetu. Tutasimama imara juu ya njia hii na tutakikusanya kizazi chetu chote katika njia hii iliyo wazi.
Enyi waumini katika ardhi ya Rafidayn, enyi wana wa shule ya Mtume, shule ya Qur'ani na Sunna ya Mtume Mustafa (saww), shule ya Imam Ali, Imam Hussein na Maimamu waongofu kutoka katika kizazi chake (as); enyi wana wa Shahid Sadr, enyi wana wa Marjaiyya Tukufu ya Najaf Ashraf, na enyi nguzo madhubuti ya Marajii wa dini pamoja na Mafaqihi na wanazuoni wapigania haki katika njia ya Mwenyezi Mungu.
Katika mapokezi haya makubwa, yenye utukufu na yenye kugusa hisia, na katika kuuaga na kumsindikiza kiongozi mkuu na mshindi wa Uislamu, Imam Sayyid Ali Khamenei, mmetoa huduma kubwa kwa Uislamu, kwa hali ya sasa, mustakabali, hadhi, dunia na Akhera yenu. Inshaallah, jambo hili limefanyika kwa ikhlasi inayoridhiwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Ijapokuwa kitendo hiki, pamoja na ukubwa wake, ni kidogo mbele ya matokeo makubwa na mema kitakayowaletea nyinyi na Umma wenu, thawabu za Mwenyezi Mungu ni kubwa zaidi. Mbele ya yale Aliyowaahidi watenda mema – malipo makubwa, rehema pana, ukarimu mzuri, nusura kubwa na neema zisizokatika – kitendo hiki kina thamani kubwa mno.
Kwa niaba ya waumini wote, waliodhulumiwa na watu wote huru na waaminifu, ninawashukuruni; kwa sababu manufaa ya yale yaliyotekelezwa kwa mikono yenu yenye ukarimu na azma yenu kubwa yanawahusu wote, na kila mmoja atanufaika nayo kwa kadiri ya uelewa wake sahihi na kutekeleza haki yake.
Na amani, rehema na baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu yenu.
Maoni yako