Jumamosi 11 Julai 2026 - 10:25
Nukta Tano Muhimu Tunazojifunza Kutokana na Mazishi Makubwa ya Imam Shahidi Khamenei (ra)

Hawza/ Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania, Maulana Sheikh Hemed Jalala, amesema kuwa; maisha na mazishi ya Imam Shahidi Sayyid Ali Khamenei (ra) yamebeba mafunzo makubwa kwa Waislamu na wanadamu kwa ujumla, huku akisisitiza kuwa urithi wake wa kiimani, huduma kwa jamii na mshikamano vinapaswa kuigwa na vizazi vya sasa na vijavyo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Maulana Sheikh Hemed Jalala aliyasema hayo katika khutuba ya Ijumaa ya jana aliyoitoa katika Msikiti wa Ghadir, uliopo Kigogo Post, jijini Dar es Salaam, ambapo alizungumza kuhusu mada yenye anuani isemayo: "Je! Tunajifunza Nini Kutokana na Mazishi ya Imam Shahidi Khamenei (ra)?"

Akianza khutuba yake, Sheikh alisoma aya tukufu ya Qur'ani isemayo:

﴿وَتَوَكَّلْ عَلَى الْحَيِّ الَّذِي لَا يَمُوتُ﴾

Na mtegemee alie hai ambae hafi

Akiifafanua mada hiyo alisema kuwa: Imam Shahidi Khamenei (ra) alikuwa na nafasi mbili muhimu zilizomfanya kuwa kiongozi mwenye ushawishi mkubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Kwa upande mmoja alikuwa Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na kwa upande mwingine alikuwa kiongozi wa Waislamu wengi duniani, hususan wafuasi wa Ahlul-Bayt (as). Alisema nafasi hizo mbili zilidhihirisha namna alivyounganisha uongozi wa dola na uongozi wa kidini, huku akibeba jukumu la kuiongoza jamii katika masuala ya kisiasa, kijamii na kidini kwa wakati mmoja.

Akizungumzia nukta ya kwanza, Maulana Sheikh Jalala alisema kuwa: Kumtegemea Mwenyezi Mungu ndilo somo kubwa zaidi linalopatikana kutokana na maisha na mazishi ya Imam Shahidi Khamenei (ra). Alieleza kuwa; Imam hakujenga matumaini yake juu ya nguvu za kijeshi, utajiri wala uungwaji mkono wa mataifa yenye nguvu, bali alimtegemea Mwenyezi Mungu katika kila hatua ya maisha yake na katika kila uamuzi alioufanya, aliongeza kuwa; tawakkul hiyo ndiyo iliyomfanya abaki imara mbele ya vitisho, vikwazo na shinikizo mbalimbali kwa miongo kadhaa ya uongozi wake. Kwa mujibu wa Sheikh, muumini anapotegemea Mwenyezi Mungu kwa ikhlasi, huwa na uthabiti wa kusimamia haki bila kuyumbishwa na mazingira yanayomzunguka.

Akielezea nukta ya pili, alisema kuwa: Kuwahudumia watu ni msingi mwingine uliojitokeza wazi katika maisha ya Imam Shahidi Khamenei (ra), alifafanua kuwa: Imam aliutumia uongozi wake kuwahudumia wananchi na Umma wa Kiislamu kwa ujumla, akitanguliza maslahi ya watu mbele ya maslahi binafsi, alisema; mtu anayejitolea kuwahudumia watu kwa uaminifu na ikhlasi hujenga nafasi ya kudumu katika nyoyo zao, na hata anapofariki huendelea kukumbukwa kwa mema aliyoyaacha, alisema: Mamilioni ya watu waliojitokeza kushiriki katika mazishi ya Imam ni ushahidi kwamba huduma ya kweli kwa jamii ndiyo inayojenga heshima na mapenzi ya kudumu miongoni mwa wananchi.

Katika khutuba hiyo, Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania alielezea nukta ya tatu kwa kusema kuwa: Kuvumiliana na kuishi kwa mshikamano ni miongoni mwa mafunzo makubwa yaliyoonekana katika mazishi ya Imam Shahidi Khamenei (ra). Alisema: Ingawa Imam alikuwa mfuasi wa madhehebu ya Shia, hakuwahi kujenga misingi ya uadui dhidi ya Waislamu wengine, bali aliongozwa na mafundisho ya Mtume Muhammad (saww) yanayohimiza upendo, uvumilivu na kuheshimiana. Alibainisha kuwa; kutokana na mwenendo huo, mamilioni ya watu kutoka madhehebu mbalimbali walishiriki katika mazishi yake, jambo lililoonesha kwamba tabia njema na kuheshimu wengine hujenga umoja na kuvuka mipaka ya tofauti za kimadhehebu.

Vilevile, Maulana Sheikh Jalala aliashiria nukta ya nne kwa kusema: Mazishi ya Imam Shahidi Khamenei (ra) yameonesha kwa vitendo umuhimu wa umoja wa kitaifa. Alieleza kuwa; licha ya kuwepo kwa tofauti mbalimbali za kisiasa, mitazamo na fikra ndani ya jamii ya Iran, wananchi waliamua kuweka pembeni tofauti hizo na kuungana katika kumuenzi kiongozi wao. Alisema mshikamano huo umeonesha kuwa; masuala yanayolihusu taifa yanahitaji umoja na uzalendo badala ya migawanyiko, alisisitiza kuwa mataifa mengine yanaweza kujifunza kutokana na mfano huo kwa kutanguliza maslahi ya taifa mbele ya tofauti zao za kisiasa na kijamii.

Akizungumzia umuhimu wa amani na kusimama pamoja na wanaodhulumiwa kama nukta ya tano, Maulana Sheikh Jalala alisema kuwa: Imam Shahidi Khamenei (ra) alikuwa miongoni mwa viongozi waliosimama bega kwa bega na wananchi wa Iraq walipokuwa wakikabiliwa na makundi ya kigaidi, alisema: Msimamo huo uliwapa moyo na matumaini Wairaqi katika kipindi kigumu cha historia yao. Kwa mujibu wake, ndiyo sababu iliyopelekea mamilioni ya wananchi wa Iraq kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mazishi yake, wakionesha shukrani na kuthamini mchango wake katika kusimama pamoja nao wakati wa matatizo.

Akihitimisha khutuba yake, Maulana Sheikh Hemed Jalala aliwapongeza na kuwashukuru waandishi wote wa habari waliokwenda nchini Iran kufuatilia na kuripoti matukio ya mazishi ya Imam Shahidi Khamenei (ra). Alisema; kazi yao imewezesha Waislamu na jamii kwa ujumla kupata taarifa sahihi kuhusu tukio hilo muhimu la kihistoria, huku akiwataka waendelee kutekeleza wajibu wao wa kuuhabarisha umma kwa weledi, uaminifu na kujitolea kwa ajili ya ukweli.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha