Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, wanazuoni, Masayyid na waumini kutoka maeneo tofauti nchini Kenya, ambao walikusanyika kwa lengo la kumuenzi Imam Shahidi na kuhuisha misingi ya mapambano, haki na uadilifu aliyoiishi katika maisha yake.
Majlisi hiyo ilianza kwa kisomo cha aya za Qur'ani Tukufu, kikifuatiwa na dua na visomo maalumu vya kumuombea Imam Shahidi pamoja na mashahidi wengine wa Umma wa Kiislamu. Baadaye, wahadhiri mbalimbali walipanda jukwaani na kuzungumzia maisha, fikra na mchango wa Imam Shahidi katika kuimarisha Uislamu, kuutetea Umma wa Kiislamu na kusimama imara dhidi ya dhulma na uistikbari.
Washiriki wa hafla hiyo walieleza kuwa urithi wa Imam Shahidi utaendelea kuishi katika nyoyo za wapenda haki duniani kote. Walimuenzi kwa uongozi wake wa mfano, msimamo wake usioyumba katika kuwatetea waliodhulumiwa, pamoja na maisha yake aliyoyatoa kwa ajili ya kuitumikia dini ya Mwenyezi Mungu na kuyatetea Madhehebu ya Ahlulbayt (as).
Miongoni mwa wahadhiri waliopata fursa ya kuzungumza alikuwa Sayyid Edarusi, ambaye alimuelezea Imam Shahidi kuwa alikuwa kiongozi aliyesimama imara katika kuihami dini ya Uislamu na kutetea haki za waliodhulumiwa duniani, alisema kuwa; maisha ya Imam Shahidi yalikuwa mfano wa kujitolea, ujasiri na uongozi wa Kiislamu unaozingatia misingi ya haki na uadilifu.
Kwa upande mwingine, Hujjatul Islam wal-Muslimin Sheikh Ali Saa Moja pia alitoa hotuba huku akizungumzia nafasi ya Imam Shahidi kama kiongozi wa kidini na kisiasa. Alibainisha kuwa Imam Shahidi alitoa mchango mkubwa katika kuimarisha umoja wa Umma wa Kiislamu, kuendeleza fikra za Mapinduzi ya Kiislamu na kuhimiza kusimama kidete mbele ya madhalimu na maadui wa Uislamu.
Hafla hiyo ilihitimishwa kwa dua ya pamoja ya kumuombea Imam Shahidi na mashahidi wote wa Umma wa Kiislamu, huku washiriki wakisisitiza umuhimu wa kuendeleza njia, maadili na misingi aliyoiweka Imam Shahidi katika kuwatumikia Waislamu na kuwatetea wanyonge popote walipo.






Maoni yako