Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, kongamano hilo lilifanyika katika mazingira ya heshima na majonzi, ambapo washiriki walipata fursa ya kusikiliza mihadhara mbalimbali iliyojikita katika maisha ya Imam Shahidi, uongozi wake wa kimkakati, msimamo wake dhidi ya ubeberu na mchango wake katika kuimarisha umoja wa Umma wa Kiislamu. Washiriki walieleza kuwa urithi aliouacha Imam Shahidi utaendelea kuwa chachu ya kuhamasisha vizazi vijavyo kusimama imara katika kutetea haki, uadilifu na heshima ya Waislamu.
Miongoni mwa wahadhiri mashuhuri waliohudhuria kongamano hilo alikuwa Sheikh Shaban Pembe, Imamu wa Msikiti wa Mtambani uliopo jijini Dar es Salaam. Katika hotuba yake alimuelezea Imam Shahidi kuwa alikuwa nuru kubwa ambayo Umma wa Kiislamu umeipoteza katika kipindi ambacho dunia ilikuwa inahitaji zaidi viongozi wenye ujasiri, hekima na msimamo thabiti. Alizungumzia kwa kina juhudi za Imam Shahidi katika kuwatetea wanyonge, kusimama bega kwa bega na waliodhulumiwa, pamoja na kujitolea kwake bila kuchoka katika kuilinda dini ya Uislamu na maslahi ya Umma wa Kiislamu.
Aidha, Sheikh Shafii Basalim naye alipata nafasi ya kutoa muhadhara ambapo alielezea mchango mkubwa wa Imam Shahidi katika kuimarisha fikra za Kiislamu, kuhuisha utamaduni wa kujitegemea na kuhamasisha mshikamano wa Waislamu. Alisisitiza kuwa maisha ya Imam Shahidi yalikuwa mfano wa uongozi unaojengwa juu ya elimu, uchamungu, uadilifu na kujitoa kwa ajili ya maslahi ya dini na jamii.
Kwa upande wake, Sheikh Hussein Zuberi alizungumzia kwa kina uzalendo, ujasiri na moyo wa kujitolea uliomtambulisha Imam Shahidi katika maisha yake yote. Alieleza kuwa: Imam Shahidi alisimama kidete kuwatetea wanyonge na waliodhulumiwa popote walipokuwa, bila kujali mipaka ya mataifa, na kwamba msimamo huo ulimfanya kuwa alama ya mapambano dhidi ya dhulma na uistikbari katika zama za sasa.
Washiriki wa kongamano hilo walieleza kuwa; mafunzo yaliyotolewa yamewapa hamasa mpya ya kuendelea kushikamana na maadili ya Uislamu, kuimarisha umoja wa Waislamu na kuendeleza misingi ya haki, uadilifu na kujitolea ambayo Imam Shahidi aliisimamia kwa maisha yake yote. Walisisitiza kuwa kumbukumbu za viongozi waadilifu zinapaswa kuhuishwa kwa kuyafanyia kazi mafunzo na misingi waliyoiacha.
Mwishoni mwa kongamano hilo, waandaaji walimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kufanikisha mkusanyiko huo wa kielimu na kiroho, na kutoa shukrani za dhati kwa wanazuoni, wageni waalikwa, washiriki na wote waliotoa mchango wao kwa namna mbalimbali kufanikisha kongamano hilo, huku wakiahidi kuendelea kuandaa programu zinazolenga kueneza elimu, kuimarisha umoja wa Umma wa Kiislamu na kuwaenzi viongozi waliotoa maisha yao katika kutetea dini na haki.







Maoni yako