Jumanne 7 Julai 2026 - 10:04
Qum Yatoa Heshima za Mwisho kwa Kiongozi Shahidi wa Umma; Ayatullah al-Udhma Jawadi Amuli Aongoza Swala ya Maiti

Hawza/ Katika mazingira yaliyogubikwa na huzuni, utiifu na mshikamano wa waumini, Ayatullah al-Udhma Jawadi Amuli leo asubuhi ameongoza Swala ya maiti juu ya mwili mtukufu wa Kiongozi Shahidi wa Umma, Imam Sayyid Ali Khamenei (ra), katika Msikiti Mtukufu wa Jamkaran, jijini Qum, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, mwili mtukufu wa Imam Khamenei (ra), ukiwa pamoja na miili ya baadhi ya wanafamilia wake, uliwasili mapema leo katika mji mtakatifu wa Qum kwa ajili ya hafla ya kuswaliwa, kuagwa rasmi na kutoa heshima za mwisho mbele ya maelfu ya wakazi wa mji huo, ambao umebarikiwa kuwa makazi ya Haram Tukufu ya Bibi Fatimah al-Ma'sumah (sa).

Mara tu baada ya kuwasili kwa msafara huo, viongozi wa ngazi za juu wa kisiasa, kidini na kijeshi walitoa heshima zao za mwisho mbele ya mwili wa kiongozi huyo shahidi, kabla ya Swala ya maiti kuongozwa na Ayatullah al-Udhma Jawadi Amuli katika mazingira yaliyotawaliwa na unyenyekevu, machozi na dua.

Maelfu ya waombolezaji waliojitokeza katika Msikiti wa Jamkaran waliinua mikono yao kumuombea rehema kiongozi huyo shahidi, huku wakionesha upendo, uaminifu na azma ya kuendeleza njia yake ya kusimamia Uislamu, haki na mapambano dhidi ya dhuluma.

Hafla hiyo ni sehemu ya ratiba rasmi ya kuaga na kuusindikiza mwili wa Kiongozi Shahidi wa Umma katika miji mbalimbali ya Iran, ambapo mamilioni ya waumini wameendelea kujitokeza kwa wingi kutoa heshima zao za mwisho kwa mmoja wa viongozi mashuhuri zaidi katika historia ya Ulimwengu wa Kiislamu.

Qum Yatoa Heshima za Mwisho kwa Kiongozi Shahidi wa Umma; Ayatullah al-Udhma Jawadi Amuli Aongoza Swala ya Maiti

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha