Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Yasin Mousawi, Imam wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad na mmoja wa walimu mashuhuri wa Hawza ya Najaf Ashraf, katika hotuba za Swala ya Ijumaa za tarehe 19 Tir 1405 Hijria Shamsia, alisisitiza kuwa, ushiriki mkubwa na wenye hamasa wa wananchi katika mazishi ya Imam Shahidi, Hadhrat Ayatullah Sayyid Ali Husseini Khamenei, ni ujumbe wa wazi unaodhihirisha nafasi yake ya juu katika nyoyo za mataifa ya waumini, na ni ishara ya kushikamana Umma wa Kiislamu na njia ya Muqawama pamoja na kupinga mipango ya mataifa ya kigeni yenye malengo ya kutawala.
Aliongeza kuwa; umati mkubwa wa watu uliohudhuria mazishi hayo nchini Iran na Iraq uliwasilisha taswira ya kipekee ya mshikamano na umoja wa wananchi.
Ayatullah Mousawi alisisitiza kuwa, ushiriki huo mkubwa haukutokana na wito rasmi wala harakati za kisiasa, bali ulikuwa ni kielelezo cha uelewa wa wananchi, imani zao za kidini na uaminifu wao kwa njia na mafundisho ya mashahidi.
Imam wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad alisema kuwa; kaulimbiu zilizopazwa katika mazishi hayo zilionesha wazi matakwa ya wananchi ya kuwafikisha mahakamani na kuwaadhibu waliohusika na mauaji ya Imam Shahidi. Aliongeza kuwa ushiriki huo wa mamilioni ya watu ulikuwa na ujumbe wa kisiasa ulio wazi kwamba fikra ya Muqawama bado inaungwa mkono kwa kiwango kikubwa na wananchi, na juhudi zozote za kuidhoofisha hazitafanikiwa.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, huku akizungumzia maendeleo ya hivi karibuni katika eneo la Mashariki ya Kati, alisema kuwa matukio ya karibuni yanaonesha kuwa eneo hilo bado linakabiliwa na mvutano mkubwa. Kwa sababu hiyo, alisisitiza kuwa uwepo wa majeshi ya kigeni unapaswa kukomeshwa, na mataifa ya eneo hilo yaruhusiwe kuamua mustakabali wao wenyewe bila kuingiliwa na nguvu za nje.
Ayatullah Mousawi pia alisisitiza umuhimu wa kuheshimu mamlaka na uhuru wa nchi za Kiislamu, huku akisema kuwa usalama wa eneo unapaswa kulindwa kwa matakwa ya mataifa yake, si kwa misingi ya shinikizo au maagizo ya mataifa ya kigeni. Alionya kuwa kuendelea kwa migogoro hakutazaa chochote isipokuwa kuongezeka kwa hali ya kutokuwa na utulivu katika eneo hilo.
Akiendelea na hotuba yake, Ayatullah Mousawi alirejelea ushiriki mkubwa wa wananchi wa Iraq katika mazishi hayo, akisema kuwa; ushiriki huo unaonesha kina cha uelewa wa wananchi pamoja na kushikamana kwa taifa la Iraq na Marjaiyya ya Kidini na njia ya mashahidi. Aliongeza kuwa, wananchi wa Iraq wana uwezo wa kutofautisha mipango inayolenga maslahi ya taifa lao na miradi inayokusudia kupanua ushawishi wa mataifa ya kigeni.
Mwishoni mwa hotuba yake, alieleza imani yake kwa busara na uelewa wa wananchi wa Iraq, huku akiwataka kutokubali kuathiriwa na propaganda na vita vya kisaikolojia vinavyoenezwa na vyombo vya habari vinavyopotosha. Aidha, aliwataka kuunga mkono kila mpango wa kweli wa mageuzi unaolenga kulinda mamlaka ya taifa la Iraq, kuhifadhi heshima ya wananchi wake na kuhakikisha uadilifu unapatikana.
Maoni yako