Jumapili 21 Juni 2026 - 12:14
Maadui wa Iran Hawakufanikiwa Kufikia Lengo Lolote Walilotangaza

Hawza / Mwenyekiti wa Baraza la Wanazuoni wa Ahlul-Bayt (as) nchini Uturuki, katika kipindi cha televisheni, alitoa tathmini kuhusu mwezi wa Muharram na kile alichokitaja kuwa ni ushindi wa Iran.

Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, Qadir Akaras, Mwenyekiti wa Baraza la Wanazuoni wa Ahlul-Bayt (as) nchini Uturuki, ambaye alikuwa mgeni katika kipindi cha “Pusula” (Dira) kinachorushwa na kituo cha Quds TV, alieleza maoni yake kuhusu kuanza kwa mwezi wa Muharram na tukio la Karbala.

Katika kipindi hicho, vipengele vya kihistoria, kidini na kibinadamu vya Karbala vilijadiliwa, huku ikisisitizwa kwamba ujumbe wa harakati ya Aba Abdillah Al-Hussein (as) bado una umuhimu mkubwa kwa ulimwengu wa leo. Vilevile, Akaras alitoa tathmini yake kuhusu maendeleo ya hivi karibuni kati ya Iran na Marekani.

Iran Haikuruhusu Adui Afikie Lengo Lolote la Kimkakati

Akaras alikumbushia kwamba; Qur’ani Tukufu imeunganisha ushindi na masharti maalumu, akirejelea Aya ya saba ya Suratu Muhammad (saww), alisema:

"Mwenyezi Mungu ameahidi ushindi wa hakika, lakini ushindi huo una masharti ya awali. Qur’ani inasema: ‘Mkimnusuru Mwenyezi Mungu, naye atakunusuruni na atazithibitisha nyayo zenu.’”

Akitoa tathmini kuhusu hali baada ya mivutano ya hivi karibuni, alisema kuwa; mjadala kuhusu nani aliyepata ushindi utaendelea kwa muda mrefu, lakini akaongeza: "Tukilitazama suala hili kwa mtazamo wa Kkislamu, tunaweza kusema kwamba; mchakato huu umehitimishwa kwa ushindi wa Iran na Kambi ya Muqawama."

Akaras alieleza kwamba; malengo makuu ya Israel na Marekani dhidi ya Iran yalikuwa kuudhoofisha mfumo wa Kiislamu, kuharibu uwezo wa makombora wa Iran, kudhibiti urani iliyoboreshwa na kupata utawala wa kikanda.

Alisema: "Hakuna hata lengo moja kati ya yale yaliyotangazwa na adui ambalo limefanikiwa kutekelezwa  hili peke yake ni mafanikio makubwa."

Pia alikumbusha kwamba; Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tangu kuanzishwa kwake imekuwa ikikabiliwa na mashinikizo makubwa, na baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ilikabiliwa na mzingiro wa kisiasa, vikwazo vya kiuchumi, vita na operesheni mbalimbali za kiusalama.

Akaras alisema: "Katika kipindi fulani, Iran ilikabiliwa na ugaidi wa mitaani, wanazuoni wa dini, wasomi wa vyuo vikuu, wanawake wenye hijabu na raia wengi wasiokuwa wanajeshi walilengwa. Jengo la Bunge lilishambuliwa, na viongozi wengi waandamizi wa nchi waliuawa katika operesheni za mauaji, hata hivyo, mfumo huo uliweza kusimama imara dhidi ya matukio yote hayo."

Aliongeza kuwa; kwa miaka mingi kumekuwa na nadharia mbalimbali kuhusu kubadilishwa kwa mfumo wa Iran au kugawanywa kwa nchi hiyo, lakini leo tunapotazama nyuma tunaona kwamba hakuna hata moja ya utabiri huo iliyotimia."

Teknolojia ya Nyuklia na Nafasi ya Wilayat al-Faqih

Katika kipindi hicho, shughuli za nyuklia za Iran pia zilijadiliwa. Akaras alisisitiza kwamba; teknolojia ya nyuklia haimaanishi tu utengenezaji wa silaha, bali pia ina matumizi muhimu katika nyanja za tiba, sayansi na viwanda. Akieleza kwamba mfumo wa kisiasa wa Iran umejengwa juu ya taasisi ya Wilayat al-Faqih, alisisitiza nafasi ya uongozi wa kidini katika jamii ya Iran, na akakumbusha mfano wa kihistoria wa fatwa ya tumbaku, akisema kuwa viongozi wa dini bado wana uwezo mkubwa wa kuiongoza jamii.

Akaras pia alisema: "Ayatullah Al-Udhma Khamenei anaona silaha za maangamizi ya halaiki na bomu la atomiki kuwa haramu kwa mujibu wa sheria za Kiislamu. Serikali ya Iran pia kwa miaka mingi imekuwa ikitangaza kwamba haina nia ya kutengeneza silaha za nyuklia, hata hivyo, mashinikizo ya kusimamisha kabisa shughuli za nyuklia za Iran bado yanaendelea."

Aliongeza kuwa ushindani wa kimkakati juu ya njia za usafirishaji wa nishati katika eneo hilo na Mlango wa Hormuz pia ni miongoni mwa sababu muhimu za mvutano uliopo, na akadai kuwa juhudi za kuidhibiti Iran kisiasa na kiuchumi hazijafanikiwa.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha