Alhamisi 6 Agosti 2026 - 14:26
Harakati ya Imam Hussein (as) ni chachu ya kuwaamsha watu huru duniani na ni siri ya umoja wa Umma wa Kiislamu

Hawza/ Hujjatul Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi, Mwenyekiti wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia Pakistan, amesema katika ujumbe wake kwamba majlisi za maombolezo ndiyo njia muhimu zaidi ya kueneza utamaduni na fikra za Imam Hussein (as). Aidha, akisisitiza umuhimu wa umoja na mshikamano wa Umma wa Kiislamu, ametoa wito kwa Waislamu kusimama kwa umoja dhidi ya Uzayuni, ubeberu na maadui wa Uislamu.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi, Mwenyekiti wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia Pakistan, amesema katika ujumbe wake kuwa; maombolezo ndilo jukwaa muhimu zaidi la kueneza fikra na utamaduni wa Husseiniyya. Alisisitiza kuwa; harakati ya Imam Hussein (as) katika kipindi cha karne kumi na nne zilizopita imekuwa chanzo cha msukumo si kwa ulimwengu wa Kiislamu pekee, bali pia kwa watu wote huru na wapenda haki duniani.

Aliongeza kuwa; Imam Hussein (as) pamoja na mashahidi wa Karbala, kupitia kujitolea na kujitoa kwao kwa kiwango kisicho na mfano, wamejipatia nafasi ya kudumu katika dhamiri ya wanadamu. Kwa sababu hiyo, watu huru kutoka mataifa, makabila na dini mbalimbali wameendelea kupata msukumo kutoka katika mwenendo, maadili na mafundisho ya Imam Hussein (as), na kuyafanya kuwa taa ya kuwaongoza maishani.

Mwanazuoni huyo mashuhuri wa Pakistan, akizungumzia hali ya sasa ya dunia alisema kuwa; leo makundi yanayotetea haki na uadilifu, ambayo yamesimama dhidi ya Uzayuni na ubeberu, yameonesha kwa vitendo roho ya umoja, kuwatetea wanaodhulumiwa na kupambana na dhulma na ukandamizaji, kwa kupata elimu na msukumo kutoka katika harakati ya ukombozi ya Sayyid al-Shuhadaa (as).

Akinukuu mafundisho ya Wahyi, alibainisha kuwa; Waislamu ni sehemu ya Umma mmoja. Kwa msingi huo, ni lazima wafuasi wote wa madhehebu ya Kiislamu wadumishe kuheshimiana, udugu, mshikamano, uvumilivu na kuzingatia hisia za wenzao ili kuimarisha umoja wa Kiislamu.

Mwenyekiti wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia Pakistan alisisitiza kuwa; Umma wa Kiislamu unapaswa kuiga mapinduzi ya Imam Hussein (as) na kushikamana na mafundisho yake, ili kuimarisha umoja na mshikamano wake, na kusimama imara mbele ya maadui wa Uislamu kama ukuta thabiti usiopenyeka.

Mwishoni alisisitiza kuwa; mataifa ya Kiislamu, kwa kudumisha umoja na mshikamano, yanaweza kuyavunja njama na malengo maovu ya madola ya kibeberu, na kuuonesha ulimwengu nguvu, mwamko na umoja wa Umma wa Kiislamu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha