Alhamisi 6 Agosti 2026 - 13:25
Uhaba wa dawa Ghaza unasababisha vifo vya wagonjwa watatu wa saratani kila siku

Hawza/ Mkurugenzi wa Kituo cha Saratani cha Ghaza ameonya kuhusu mzozo mkubwa wa uhaba wa dawa na vifaa vya matibabu, akitangaza kuwa; kila siku wagonjwa watatu wa saratani katika Ukanda wa Ghaza hupoteza maisha kutokana na kukosekana kwa matibabu yanayofaa.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, kikinukuu Shirika la Habari la Anadolu, Muhammad Abundi, Mkurugenzi wa Kituo cha Saratani cha Ghaza, amesema kuwa; uhaba mkubwa wa dawa na vifaa vya matibabu umeweka maisha ya takriban wagonjwa 11,000 wa saratani katika Ukanda wa Ghaza kwenye hatari kubwa. Aidha, kila siku wagonjwa watatu hufariki dunia kutokana na madhara ya ugonjwa huo pamoja na kukosekana kwa matibabu yanayofaa.

Aliongeza kuwa; takriban wagonjwa 4,000 wamepewa vibali vya kwenda kutibiwa nje ya Ghaza, lakini vikwazo vilivyowekwa katika vivuko vya mipakani vimewazuia kuondoka. Vilevile, vituo vya matibabu vinakabiliwa na uhaba mkubwa wa dawa za kemotherapi pamoja na ukosefu wa huduma za tiba ya mionzi.

Mkurugenzi wa Kituo cha Saratani cha Gaza alisisitiza kuwa; dawa maalumu kwa wagonjwa wa saratani ndizo zinazoongoza katika orodha ya mahitaji muhimu, huku kiwango cha upungufu wake kikifikia asilimia 61. Pia alibainisha kuwa vituo vya matibabu ya saratani vimeharibiwa katika mashambulizi ya utawala wa Kizayuni.

Abundi alieleza kuwa uhaba wa huduma na vifaa vya matibabu umewalazimu wahudumu wa afya kufanya maamuzi magumu sana. Katika baadhi ya matukio, hata kwa wagonjwa wa saratani ya matiti waliokuwa katika hatua za mwanzo za ugonjwa, kutokana na kutokuwepo kwa tiba ya mionzi na ugumu wa kuwahamisha wagonjwa, madaktari wamelazimika kuondoa titi lote.

Mwishoni, aliyaomba mashirika ya kimataifa kuchukua hatua za haraka na zenye ufanisi ili kuhakikisha dawa zinazohitajika kwa wagonjwa wa saratani zinapelekwa Ghaza kwa dharura na kwa mwendelezo, pamoja na kurahisisha uhamishaji wa wagonjwa kutoka Ukanda wa Ghaza ili waweze kuendelea na matibabu yao.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha