Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Naim Qassem, Katibu Mkuu wa Hizbullah, katika hotuba yake kwa mnasaba wa “Sikukuu ya Muqawama na Ukombozi”, alisisitiza kwamba: Muqawama ni zao na matunda ya harakati za watu wote wenye heshima, wapinzani wa dhulma na wazalendo, alieleza kuwa; ukombozi ni matokeo ya juhudi za wote hao, na pia ni matunda ya mchango mkubwa wa Imam Sayyid Musa al-Sadr — Mwenyezi Mungu amrejeshe yeye na wenzake wawili wakiwa salama — pamoja na matunda ya uongozi mkubwa wa Imam Khomeini (r.a.), pale alipotangaza kwamba “Israel ni shari ya kiwango cha juu kabisa,” na Hizbullah tangu kuanzishwa kwake ilijikita kupambana na adui kwa ajili ya kuikomboa ardhi.
Aliongeza kuwa: Ukombozi huu ni miongoni mwa matunda ya shahidi Imam Khamenei, ambaye aliendeleza njia hii, akaisimamia kwa uthabiti, akaunga mkono, na akaongoza mwelekeo huu ndani ya Palestina na Lebanon. Pia alisema: Muqawama ni matokeo ya uongozi wa Sayyid Hassan, bwana wa mashahidi wa umma huu… uongozi ambao ulianza hapo awali na Sheikh Ragheb Harb, ukapitia kwa Katibu Mkuu wa zamani Sayyid Abbas Mousawi, na ukaendelea kupitia vijana mujahidi, akiwemo Hajj Imad Mughniyeh — Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake — pamoja na wenzake, makada na wapiganaji.
Sheikh Qassem pia alikumbusha kwamba; ushindi ulikuwa ni matokeo ya ushirikiano wa jeshi, wananchi na Muqawama, alisema kuwa; kulikuwepo aina ya uratibu kati ya serikali na Muqawama, jambo ambalo lilikuwa sababu muhimu na yenye athari kubwa katika kufanikisha ukombozi, alisisitiza kwamba; kuvuliwa silaha za Muqawama ni kuondolewa kwa uwezo wa kujihami wa Lebanon na ni hatua ya awali ya maangamizi, jambo ambalo hawatalikubali.
Katibu Mkuu wa Hizbullah alianza hotuba yake kwa kuwapongeza Waislamu kwa kuwasili kwa Sikukuu ya Eid al-Adhha na kusisitiza kwamba; tukio hili ni sikukuu ya Walebanoni wote, watu wote huru duniani, na pia ni sikukuu ya Palestina, katika muktadha huo alitaja mchango wa Emile Lahoud, Nabih Berri na Salim al-Hoss, akiwataja kuwa miongoni mwa waungaji mkono na walinzi wa ukombozi.
Aliongeza kuwa; vikwazo ambavyo Marekani imeviweka dhidi ya baadhi ya wabunge wa Hizbullah, baadhi ya ndugu katika Harakati ya Amal, pamoja na maafisa wa jeshi na usalama wa umma, vina lengo la kuweka shinikizo dhidi ya Muqawama, alisisitiza: Vikwazo hivi vitatufanya tuwe imara zaidi.
Akiashiria kwamba serikali ilipaswa kusema jambo kuhusu suala hilo, aliongeza: Ikiwa Marekani itaongeza zaidi ukatili wake, basi haitabaki na chochote nchini Lebanon, kwa sababu itaibomoa Lebanon juu ya vichwa vya watoto wake na hata juu ya kichwa cha Marekani yenyewe.
Sheikh Qassem alirejelea miaka 15 ya ukaliaji wa mabavu na kuundwa kwa kile kilichoitwa wakati huo “Jeshi la Kusini mwa Lebanon”, akisema kwamba; adui alitaka kupitia njia hiyo kufanikisha tamaa zake nchini Lebanon, lakini mapigo ya Muqawama yalimlazimisha kuondoka katika eneo la mpaka mwaka 2000.
Pia alizungumzia “Mkataba wa Mei 17” (1983), ambao aliuita mkataba wa fedheha, na kukumbusha kwamba; haukutekelezwa na ulivunjika mwaka 1984, alisema kwamba; hiyo ilikuwa hatua katika njia ya ukombozi ambao ulitimia mwaka 2000.
Alisema: Tarehe 24 Novemba 2024, serikali ya Lebanon ilifikia makubaliano yasiyo ya moja kwa moja ambayo yalipaswa kumaliza ukaliaji wa mabavu na kusimamisha mashambulizi, lakini katika kipindi cha miezi 15 baada ya hapo, mashambulizi ya Israel yaliendelea na serikali ya Lebanon haikuweza kuyasimamia.
Katibu Mkuu wa Hizbullah aliendelea kusema: Tunaelewa udhaifu wa serikali ya Lebanon, lakini inapaswa kuwaambia Wamarekani kwamba haiwezi. Akirejelea mfululizo wa misimamo ya kujitoa muhanga kwa upande wa serikali ya Lebanon, aliongeza kwamba; mwenendo huu ulifikia hatua ya kuhalalisha kuhesabu Muqawama kuwa kosa ifikapo tarehe 2 Machi 2026.
Alifafanua kwa kusema: Hatuiombi serikali ipambane na mradi wa Marekani na Israel, lakini haipaswi kusimama dhidi ya wananchi wake, mpango wa Israel ni mpango wa kuangamiza Muqawama na kuikalia Lebanon hatua kwa hatua ndani ya mfumo wa mradi huu, kwa hiyo tunaitaka serikali ya Lebanon kuachana na uamuzi wa kuhodhi silaha mikononi mwa serikali pekee ili iweze kusimama pamoja na wananchi wake.
Sheikh Qassem alisema: Kuwavua silaha Muqawama ni kuondoa uwezo wa kujihami wa Lebanon na ni utangulizi wa maangamizi, Maafisa wa Lebanon wanatuambia: Tusaidieni tuwanyang’anye silaha ili baadaye Israel aje, awaue na kuwafanya watu wenu wakimbie makwao, Maafisa wa Lebanon wana wajibu wa kulinda mamlaka ya taifa na ulinzi wake; je, wanashikamana na yale ambayo katiba imeyaeleza?
Alisisitiza kwamba; Israel ni adui mwenye tabia ya upanuzi wa kikoloni, anayefanya mashambulizi na anayetaka kujitanua katika eneo hili, na kwamba hakuna afisa yeyote mwenye haki ya kuhudumia mradi wa Kizayuni.
Sheikh Qassem alitaka kusimamishwa kwa mashambulizi, kuondoka kikamilifu kwa Israel, kuachiwa huru kwa wafungwa na kurejea kwa wananchi makwao, akisema: Baada ya hapo tutazungumza kuhusu mkakati wa kujihami.
Katibu Mkuu wa Hizbullah alieleza wazi kwamba; Muqawama utailinda ardhi, heshima na kila atakayesimama dhidi yetu, na kwamba kama wanavyopambana na Israel, ndivyo watakavyopambana na yeyote anayesimama dhidi yao, silaha zitabaki mikononi mwao mpaka serikali ya Lebanon iweze kutekeleza majukumu yake.
Aliendelea kusema kwamba; kinachotokea leo ni kuimarishwa kwa uwepo wa Lebanon yenye nguvu na iliyokombolewa, na kwamba kinachoendelea kusini ni mwanzo wa kuporomoka kwa Israel, akirejelea hasara halisi za Israel kusini mwa Lebanon, aliongeza kwamba; adui kwa kujibu analenga raia na nyumba zao.
Sheikh Qassem pia alizungumzia nafasi ya vyombo vya habari vya Muqawama wa Kiislamu vinavyorekodi operesheni za jihadi dhidi ya ukaliaji wa Kizayuni katika maeneo yaliyokaliwa kwa mabavu, alisema kwamba; kama si vyombo hivyo, Israel isingekubali hasara hizo, alisisitiza kwamba ndege zisizo na rubani za Muqawama zitaendelea kuwafuatilia wanajeshi wa adui.
Alisisitiza kwamba; mamlaka ya taifa si suala la usalama pekee, bali pia ni la kiuchumi, kisiasa na kijamii, na kwamba kuhodhi silaha ni mradi wa Kizayuni, ikiwa serikali haiwezi kulinda mamlaka ya taifa, basi inapaswa kuondoka.
Sheikh Qassem aliongeza: Nchini Lebanon hakuna mamlaka ya kisiasa ya kweli, bali nchi iko chini ya ushawishi wa Marekani, mazungumzo ya moja kwa moja hayakubaliki na ni faida tupu kwa Israel, hivyo basi; tunaitaka serikali ya Lebanon kuyaacha mazungumzo ya moja kwa moja na kutotoa kile ambacho Marekani inakitaka.
Alisema: Rejeeni kwenye maelewano ya kitaifa, kwa sababu hamtapata chochote, tunakabiliwa na tishio la kiuwepo, na tutaendelea kujihami mpaka tufikie mojawapo ya hatima mbili: ushindi au shahada. Kila kujitolea ni kwa ajili ya kujenga mustakabali, na mauaji yote pamoja na uharibifu wote vina lengo la kutulazimisha kupiga magoti; lakini sisi hatutapiga magoti kamwe, tutabaki uwanjani na tutatoka vitani tukiwa tumenyanyua vichwa vyetu juu.
Katibu Mkuu wa Hizbullah aliongeza: Tutazijenga upya nyumba, watu wetu watarejea makwao, tutamfukuza adui akiwa ameshindwa, na hivi karibuni Inshaallah, tutatangaza ukombozi wa tatu.
Sheikh Qassem aliendelea: Mauaji yote na uharibifu wote vina lengo la kutulazimisha kupiga magoti, lakini sisi hatutapiga magoti kamwe, tutabaki uwanjani na tutatoka vitani tukiwa na vichwa vilivyoinuliwa juu, akizungumza na wapiganaji alisema: Ninyi mnaivunja simulizi ya “ngano ya adui wa Kizayuni kuwa hawezi kushindwa” na ninyi mtashinda.
Alisema kwamba; kushambuliwa taasisi ya Qardh al-Hasan ni kushambuliwa kwa mamia ya maelfu ya maskini na wenye kipato cha chini, huku akifafanua kwamba Qardh al-Hasan ni taasisi huru ya kijamii, alisisitiza kwamba mradi wa kuiangamiza Qardh al-Hasan ni mradi wa Marekani na kwamba wataukabili.
Sheikh Qassem anaamini kwamba wananchi wana haki ya kutoka mitaani na kuiangusha serikali pamoja na mradi wa Marekani na Israel.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, alisisitiza kwamba Palestina itaendelea kuwa dira ya uelekeo, na akasema: Tutaendelea kuwa miongoni mwa waungaji mkono wake, kisha akauliza: Israel inazuia kufika kwa “Msafara wa Uhuru” wa kiraia; dunia iko wapi?
Kuhusu Iran, Sheikh Qassem aliuliza: Iran imefanya nini hadi Marekani na Israel zipigane nayo? Alieleza kwamba; Iran itatoka vitani ikiwa na kichwa kilichoinuliwa, kwa sababu imeweza kuidhalilisha Marekani na Israel, na ndiyo nguvu pekee inayokabiliana na dola kubwa zaidi ya ukandamizaji duniani.
Alisema kwamba; Iran itageuka kuwa nguvu ya kipekee yenye nafasi ya kimataifa, ambayo watu wote huru duniani watakuwa wakikimbilia kwake.
Sheikh Qassem pia alionesha matumaini kwamba makubaliano kamili ya kusitisha uhasama yatafikiwa na kwamba Lebanon nayo itajumuishwa katika makubaliano hayo.
Kwa upande mwingine, aliitaka Bahrain kuwaachia huru wanazuoni na raia waliowekwa gerezani kutokana na imani zao za kidini na kisiasa.
Mwishoni, Sheikh Qassem alisema: Tutabaki kuwa wabeba bendera hii mpaka tutakapomkabidhi Imam Mahdi (a.f.).
Maoni yako