Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Yasin Mousawi, Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad na mmoja wa walimu mashuhuri wa Hawza ya Najaf, alisema katika khutba za Swala ya Ijumaa mjini Baghdad kwamba; Iraq ipo katika hatua nyeti ya mabadiliko ya kisiasa na ya kikanda, hali ambayo inalazimu kulindwa kwa mamlaka ya kitaifa na kupambana na aina yoyote ya uingiliaji wa kigeni.
Akiwaonya watu kuhusu juhudi za kutaka kulazimisha matakwa ya madola ya kigeni katika maamuzi ya Iraq, alisema: “Baadhi ya mikondo ya kisiasa inajaribu kuunda upya mizania ya kisiasa ya eneo hili kwa namna inayohudumia maslahi ya Marekani na utawala wa Kizayuni.”
Ayatullah Mousawi, akirejelea mchakato wa kisiasa wa Iraq baada ya uchaguzi wa hivi karibuni, alisema: “Mchakato wa kisiasa bado unakabiliwa na matatizo makubwa katika namna ya kuchagua viongozi wa mihimili mitatu ya dola na kuunda serikali, na mbinu zilizotumika katika miaka iliyopita zimesababisha migogoro mingi ya kisiasa na kiutawala nchini.”
Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad pia alisisitiza umuhimu wa kuandaa sera ya mambo ya nje yenye uwiano na kusema: “Serikali mpya inapaswa kujenga uhusiano mzuri na wa uwiano na nchi zote jirani na ijiepushe na kuingia katika migogoro na mivutano ya kikanda.”
Aliongeza kuwa: “Kupanua mahusiano na nchi za Kiarabu na za kikanda hakupaswi kufanyika kwa gharama ya kudhoofisha mamlaka ya Iraq na uhuru wa maamuzi ya kisiasa ya nchi hii.”
Ayatullah Mousawi alikosoa kile alichokiita “kujisalimisha kisiasa” mbele ya baadhi ya miradi ya kigeni na kusisitiza kwamba: “Iraq ina nafasi muhimu ya kihistoria na ya ustaarabu, na inaweza kutekeleza jukumu la msingi katika eneo hili.”
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, alitoa wito wa kuwepo kwa uwiano katika mahusiano ya Iraq na madola makubwa duniani, yakiwemo Marekani, Urusi, China na Uingereza, na akasisitiza: “Baghdad haipaswi kuwa chini ya shinikizo la kigeni, na maamuzi ya kisiasa ya Iraq yanapaswa kuwa huru kabisa na kujengwa juu ya msingi wa mamlaka ya kitaifa.”
Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad pia alikosoa uingiliaji wa moja kwa moja wa Marekani katika mchakato wa kuunda serikali nchini Iraq na kusema: “Baadhi ya mikondo ya kisiasa imekuwa chini ya shinikizo la kigeni katika mchakato wa kuchagua viongozi na kuunda serikali; jambo ambalo linatishia uhuru wa maamuzi ya kitaifa ya Iraq.”
Ayatullah Mousawi, katika sehemu ya kiuchumi ya khutba zake, aliitaka serikali mpya kuwasilisha mipango ya vitendo ya kutatua matatizo ya maisha ya wananchi, kupunguza pengo la kitabaka na kupambana na ukosefu wa ajira na umaskini, pia alisisitiza umuhimu wa kuimarisha tabaka la kati ili kudumisha uthabiti wa kijamii.
Vilevile alisisitiza haja ya kuijenga upya na kuimarisha nguvu za kijeshi za Iraq na kusema: “Iraq inahitaji jeshi lenye nguvu na vifaa vya kisasa ili iweze kulinda mamlaka na usalama wa nchi bila kutegemea majeshi ya kigeni.”
Akiendelea na mazungumzo yake kuhusu maendeleo ya eneo hili, Imamu wa Sala ya Ijumaa wa Baghdad alieleza kwamba; sera za Marekani zinalenga kuunda upya muundo wa kisiasa wa eneo na kudhoofisha mikondo ya Muqawama na harakati za kutetea uhuru, aliongeza: “Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ulikuwa hatua muhimu katika kufufua ari ya kujitegemea miongoni mwa mataifa ya eneo hili.”
Pia alieleza kwamba; sera za kuchochea tofauti za kimadhehebu na kikabila ni miongoni mwa nyenzo zinazotumiwa na Marekani kudhoofisha umoja wa Umma wa Kiislamu, na akasisitiza kwamba; vita na migogoro mingi ya eneo hili inaweza kutathminiwa katika mfumo huo.
Ayatullah Mousawi, kuhusu maendeleo ya Lebanon, alisema: “Marekani na utawala wa Kizayuni wanajaribu kudhoofisha harakati za Muqawama na Hizbullah na kubadilisha mizania ya kisiasa ya Lebanon kwa manufaa yao, lakini baadhi ya mipango hiyo imekumbana na upinzani kutoka kwa taasisi rasmi za Lebanon.”
Pia alionya kuhusu juhudi za kuzuia na kudhoofisha harakati za Muqawama nchini Iraq na kusisitiza kwamba: “Suala la kuweka silaha mikononi mwa serikali pekee halipaswi kutumiwa kama chombo cha kudhoofisha mikondo inayopinga ushawishi wa Marekani.”
Mwishoni mwa hotuba yake, Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad aliwataka wananchi wa Iraq kuulinda utambulisho wao wa kitaifa, kuimarisha mamlaka ya nchi na kupambana na utawala wa kigeni, alibainisha kwamba: “Iraq ina hazina kubwa ya kihistoria na ya kiustaarabu, na inaweza kurejesha nafasi yake ya msingi katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu.”
Maoni yako