Kwa mujibu wa kitengo cha kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, kikinukuu shirika la habari la NTV, msafara wa kimataifa wa “Sumud” kwa mara nyingine umeelekea Ghaza; makumi ya meli na mamia ya wanaharakati wameanza safari kwa ajili ya kuvunja mzingiro wa baharini.
Msafara wa kimataifa wa “Sumud”, katika kuendeleza juhudi za kimataifa za kuvunja mzingiro wa Ghaza na kupeleka misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa eneo hilo, kwa mara nyingine umeanza harakati zake kutoka maji ya Bahari ya Mediterania, Msafara huu ambao unajumuisha makumi ya meli na mamia ya wanaharakati wa kimataifa kutoka nchi mbalimbali, umeanza tena shughuli zake baada ya uingiliaji na mashambulizi ya awali ya vikosi vya Israel.
Muungano wa msafara wa “Sumud” umetangaza kuwa meli tano zimeondoka kutoka Ugiriki ili kuungana na takribani boti 55 nyingine ambazo zimeondoka kutoka bandari ya Marmaris nchini Uturuki kuelekea Ghaza. Vyombo hivi vya majini vikiwa na bendera za Ufaransa, Italia na Poland, na baadhi yake vimebeba kiasi cha vyakula na dawa.
Kwa mujibu wa waandaaji, katika msafara huu wapo takribani wanaharakati 500 kutoka nchi 45, na meli hizo zinaendelea na safari yao katika upande wa mashariki wa Bahari ya Mediterania karibu na kisiwa cha Rhodes.
Wanaharakati walioshiriki wamesisitiza kuwa; katika hali ambayo vyombo vya habari na fikra za umma duniani zimeelekezwa katika migogoro mingine, mzingiro wa Ghaza bado unaendelea, na hatua hii ni juhudi ya kuelekeza tena uangalizi wa dunia katika hali ya kibinadamu ya eneo hilo.
Muungano wa msafara wa “Sumud” katika taarifa yake ulisisitiza kuwa; msafara huu si kampeni ya utoaji misaada pekee, bali ni hatua ya moja kwa moja ya kiraia dhidi ya mzingiro wa baharini wa “kidhalimu na usio wa kisheria” wa Ghaza; mzingiro ambao umewekwa kwa lengo la kuitenga na kulibana taifa la Palestina.
Muungano huu pia umetangaza kuwa, ushiriki wa kimataifa katika mpango huu umeongezeka kwa kiwango kikubwa baada ya safari ya meli ya “Madeline” mwezi Juni 2025, na jambo hili linaonesha kuongezeka kwa upinzani wa kimataifa dhidi ya kuhalalishwa kwa mzingiro na vita dhidi ya Ghaza.
Msafara wa “Sumud” hapo kabla pia ulikumbana na uvamizi wa vikosi vya Israel. Tarehe 12 Aprili, meli ambazo zilikuwa zimeondoka kutoka Hispania zilisimamishwa na vikosi vya Israel, na zaidi ya wanaharakati 100 wanaoiunga mkono Palestina walipelekwa katika kisiwa cha Krete.
Muungano wa waandaaji pia umetangaza kuwa tarehe 29 Aprili, vikosi vya Israel vilishambulia meli 22 za kiraia katika pwani ya magharibi ya Ugiriki na kuwateka watu wawili miongoni mwa waandaaji wa msafara wa kimataifa wa “Sumud” na kuwafanyia vitendo vibaya. Baada ya tukio hilo, harakati za meli zilisimamishwa kwa muda ili hali ya usalama itathminiwe, lakini licha ya vitisho na mashinikizo, jukumu la msafara huo limeendelea.
“Katie Davidson”, mmoja wa wanaharakati wa ujumbe wa Uingereza katika msafara huo, akilaani ukimya wa serikali ya Uingereza kuhusu uingiliaji wa Israel alisema: Hata kama meli hazitafanikiwa kufika Ghaza, aina yoyote ya kushambuliwa kwa msafara huu inaweza tena kuelekeza macho ya umma wa dunia katika janga la kibinadamu la Ghaza.
“Shima Danli Yalvach”, mwanaharakati wa Kituruki pia akirejelea uchache wa matangazo ya vyombo vya habari kuhusu harakati hii alisema: “Hata kama hakuna chombo chochote cha habari kitakachotutangaza, hilo halina umuhimu. Tutaendelea na njia yetu.”
Mnamo Oktoba mwaka uliopita pia jeshi la Israel lilisimamisha msafara mwingine uliokuwa umeandaliwa na kundi hili hili na kuwakamata zaidi ya watu 450, akiwemo “Greta Thunberg”, mwanaharakati wa Kiswidi.
Muungano wa msafara wa “Sumud” pia umekiri kuwa Israel na Marekani kwa “madai yasiyo na msingi” wanajaribu kuipaka matope harakati hii ya kiraia na kuweka mazingira ya mashambulizi zaidi dhidi ya wanaharakati.
Waandaaji wa harakati hii walisisitiza kuwa; msafara wa “Sumud” ni alama ya mshikamano wa kibinadamu na watu wa Ghaza na pia ni aina ya “muqawama wa kiraia wa kimataifa” dhidi ya vurugu, uvamizi na mzingiro, na kwamba hatua hizi zitaendelea mpaka mwisho wa kuizingira Ghaza.

Maoni yako