Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, matni kamili ya tamko la Ayatollah Nouri Hamedani kuhusu matukio yanayoendelea Ghaza ni kama ifuatavyo:
Bismillahir Rahmanir Rahim
Watu wa heshima wa ulimwengu wa Kiislamu!
Wanazuoni wakubwa!
Serikali za Kiislamu na watu huru wa fikra!
وَإِنِ ٱستَنصَرُوكم فِی ٱلدِّینِ فَعَلَیكُمُ ٱلنَّصرُ"Na ikiwa wataomba msaada kwenu kwa ajili ya dini, basi ni juu yenu kuwanusuru. (Al-Anfal: 72)
Kwa mara nyingine tena dhamira ya mwanadamu na asili safi za kibinadamu zimetikiswa na jinai ya kutisha na ya aibu inayotekelezwa na utawala wa Kizayuni unaoua watoto, Ghaza madhulumu, kwa sasa, si tu inateketezwa kwa moto wa mashambulizi ya mabomu yasiyo na huruma, bali pia imezingirwa kwa vizuizi vya chakula, dawa na misaada ya kibinadamu, njaa kali, kuuawa kwa dhulma kwa watoto, wanawake, wazee na wagonjwa, na picha za kusikitisha za watu wasio na ulinzi wakifariki, vinaua nyoyo za kila mtu mwenye dhamira huru.
Vitendo hivi si tu ni mfano wa wazi wa mauaji ya kimbari na jinai za kivita, bali haviwezi kuelezewa au kuhalalishwa kwa kipimo chochote cha kibinadamu, kisheria, kikanuni wala kimataifa, kilio cha kudhulumiwa cha watu wa Ghaza leo hii ni mtihani mkubwa kwa wanazuoni wa Kiislamu, viongozi wa nchi za Kiislamu na taasisi za kimataifa.
Katika zama hizi ambapo kilio cha kudhulumiwa cha taifa la Palestina—hasa Ghaza—kimefika masikioni mwa watu duniani kote, dhamira zilizoamka za kibinadamu duniani zimeghadhibika kwa dhulma iliyo wazi inayofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wasio na ulinzi, katika hali hii, jukumu zito lipo juu ya mabega ya wanazuoni wa dini na serikali za Kiislamu, kwa kuwa si tu kwa mujibu wa vigezo vya kibinadamu, bali pia kwa hukumu ya Qur’ani na Sunnah, wamewajibika kuwatetea waliodhulumiwa na kukabiliana na dhulma.
Jukumu la wanazuoni wa dini katika mazingira haya nyeti na ya kihistoria ni kutoa fatwa za kuunga mkono, na wito wa umoja dhidi ya adui wa pamoja, pamoja na kulaani kwa uwazi utawala wa Kizayuni na kila aina ya uhusiano wa kawaida nao, Kuhamasisha watu kuwasaidia kwa mali na hali watu wa Palestina, na pia kutumia mimbari za sala za Ijumaa na za jamaa, pamoja na kutumia uwezo wa vyombo vya habari, taasisi za kielimu na za kidini ili kuamsha Umma wa Kiislamu, ni miongoni mwa majukumu nyeti ya kidini, kisiasa na kijamii ya kila mmoja wetu, bila shaka uzembe na kupuuza jambo hili kutakuwa na athari mbaya katika dunia na Akhera.
Serikali za Kiislamu pia, si tu kwa msingi wa mshikamano wa kidini, bali pia kwa mtazamo wa kibinadamu na haki za binadamu, zimewajibika kuchukua msimamo thabiti dhidi ya jinai za kivita za utawala wa Kizayuni unaoikalia kwa nguvu ardhi ya Quds. Kwa masikitiko, mara nyingi tumeona ukimya au hata ushirikiano wa baadhi ya serikali na utawala huu, inatarajiwa kutoka kwa serikali za Kiislamu kwamba zivunje au zisitishe uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni, na zitumie uwezo wa taasisi za kimataifa kulaani na kuadhibu utawala huu, vilevile zitume misaada ya kibinadamu na ya kitabibu kwa watu wa Ghaza, na kuweka katika ajenda zao suala la kuiunga mkono harakati halali ya watu wa Palestina.
Kutokujali kwa wanazuoni wa dini na serikali za Kiislamu si tu kwamba kutaendeleza dhulma, bali pia kutapunguza hadhi ya Uislamu katika ngazi ya kimataifa, umoja wa Kiislamu na mwamko wa Umma hujengwa tu kwa vitendo halisi na msaada wa kweli kwa wanyonge, kizazi kipya cha Waislamu kinazifuatilia kwa karibu hatua za
wanazuoni na viongozi wa kisiasa, na ukimya huuchukulia kuwa ni ishara ya unafiki au udhaifu wa dhamira ya kidini.
Sasa ni wakati ambao watu wote waaminifu wa ulimwengu wa Kiislamu—wanazuoni, wasomi na viongozi wa serikali—waweke kando tofauti za ndani na watimize wajibu wao wa Kiislamu na kibinadamu kwa ajili ya watu wa Ghaza, mwamko wa Umma wa Kiislamu unahitaji kilio cha kudai haki na hatua ya pamoja.
Janga la Ghaza si tu ni mgogoro wa kibinadamu, bali ni mtihani wa kihistoria kwa ulimwengu wa Kiislamu, wanazuoni wa Kiislamu lazima wachukue nafasi ya kuwa vinara wa harakati hii ya kuamsha umma, na serikali za Kiislamu lazima zathibitishe kuwa zinastahili kuitwa “ za Kiislamu.” Ikiwa leo tutanyamaza kimya juu ya damu safi inayomwagika, basi kesho itakuwa zamu ya ardhi nyingine, tuna yakini kuwa ahadi ya Mwenyezi Mungu kuhusu kuwanusuru wanyonge na kuwaangamiza madhalimu ni ya hakika isiyokwenda kinyume:
.إِنَّهُۥ لَا یُفلحُ ٱلظَّـٰلِمُونَ
"Hakika madhalimu hawatafaulu." (Al-An'am: 135)
Wassalamu ‘alaykum wa rahmatullahi wa barakatuh
Hussein Nouri Hamedani
Maoni yako