Jumapili 25 Mei 2025 - 23:42
Mafanikio ya Dola ya Imam Mahdi (a.s)

Hawza | Mafanikio ya serikali ya Imam Mahdi (a.s) ni ya kuvutia sana na yenye umuhimu mkubwa. Kwa kifupi, tunaweza kusema kuwa mafanikio haya yatakidhi mahitaji yote ya kiroho na kimwili ya mwanadamu ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu ameyaweka ndani ya nafsi yake kwa amana.

Shirika la Habari la Hawza - Malengo ya serikali ya Imam Mahdi (a.s) ni malengo halisi na asili ambayo mizizi yake imo ndani kabisa ya dhamira ya mwanadamu, kila mtu amekuwa akitamani kuyafikia, na mipango yake imepangwa kwa mujibu wa mafundisho ya Qur'ani na Sunna za Ma'sumina (a.s). Vilevile, katika kila sekta, kuna dhamana ya utekelezaji wa mipango hii. Kwa hiyo, mafanikio ya mapinduzi haya makubwa ni ya kustaajabisha na ya kuvutia sana. Kwa kifupi, mafanikio ya serikali ya Imam Mahdi (a.s) yanakidhi mahitaji yote ya kiroho na kimwili ya mwanadamu ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu ameyaweka ndani ya nafsi yake kwa amana.

Hapa, kwa kuzingatia riwaya, tutaelezea baadhi ya mafanikio haya:

1. Uadilifu wa Kina
Katika riwaya nyingi, jambo muhimu zaidi linalotajwa kama matokeo ya harakati na mapinduzi ya Imam Mahdi (a.s) ni kuenea kwa haki na uadilifu duniani kote. Katika utawala wa Qaim wa Aal-Muhammad (a.j), uadilifu utakuwa ni jambo linalopatikana katika jamii yote, na hakutakuwa na taasisi ndogo au kubwa isipokuwa uadilifu utatawala humo, na uhusiano kati ya watu utawekwa juu ya msingi wa uadilifu huo.

Imam Swadiq (a.s) anasema kuhusu hili:

«أَمَا وَ اللَّهِ لَیَدْخُلَنَّ عَلَیْهِمْ عَدْلُهُ جَوْفَ بُیُوتِهِمْ كَمَا یَدْخُلُ الْحَرُّ وَ الْقُرُّ.»

Naapa kwa Mwenyezi Mungu, ataiingiza haki yake hadi ndani ya nyumba za watu, kama vile joto na baridi vinavyoingia ndani ya nyumba zao. (Ghaybat Nu'mani, Juz. 1, uk. 296)

2. Ukuaji wa Kiakili, Kimaadili na Kiimani
Katika riwaya zetu, tumeashiriwa kuwa watu watapata maendeleo ya kiakili, kimaadili na kiimani katika utawala wa Imam Mahdi (a.s).

Imam Baqir (a.s) anasema:

«إِذَا قَامَ قَائِمُنَا وَضَعَ اللَّهُ یَدَهُ عَلَى رُءُوسِ الْعِبَادِ فَجَمَعَ بِهَا عُقُولَهُمْ وَكَمَّلَتْ بِهِ أَحْلَامُهُمْ.»

Wakati Qaim wetu atakaposimama, Mwenyezi Mungu ataweka mkono wake wa rehema juu ya vichwa vya waja wake, na kwa hiyo atayakusanya akili zao, na atazikamilisha ndoto zao. (Kafi, Juz. 1, uk. 25)

Inafaa kutambua kwamba mambo yote mema na mazuri hupatikana kutokana na ukamilifu wa akili ya mwanadamu, kwani akili ni Mtume wa ndani wa mwanadamu, na ikiwa itatawala juu ya ufalme wa mwili na roho ya mwanadamu, basi fikra na vitendo vya mwanadamu vitakwenda kwenye usawa na uongofu, na njia ya ibada kwa Mola na kupata ufanisi itarahisishwa.

3. Umoja na Mshikamano
Kwa mujibu wa riwaya, watu walio chini ya utawala wa dunia wa Imam Mahdi (a.s) watakuwa wamoja na wenye mapenzi kwa kila mmoja. Wakati wa kuanzishwa kwa dola ya Mahdi, chuki na uadui havitakuwa na nafasi kwa waja wa Mwenyezi Mungu.

Imam Ali (a.s) anasema kuhusu hili:

«وَلَوْ قَدْ قَامَ قَائِمُنَا... لَذَهَبَتِ الشَّحْنَاءُ، مِنْ قُلُوبِ الْعِبَادِ..

Wakati Qaim wetu atakaposimama... chuki zitaondoka kwenye mioyo ya waja. (Bihar al-Anwar, Juz. 52, uk. 316)

Pia Imam Swadiq (a.s) katika kuelezea enzi ya Mahdi anasema:

«... وَ یَجْمَعَ اللَّهُ الْكَلِمَةَ وَ یُؤَلِّفَ بَیْنَ قُلُوبٍ مُخْتَلِفَةٍ...»

[Katika siku hizo] Mwenyezi Mungu ataunganisha tamko la watu wote na kuleta mapatano kati ya mioyo iliyotengana na kutawanyika. (Kamal al-Din, Juz. 2, uk. 645)

4. Afya ya Mwili na Akili
Katika serikali tukufu ya Mahdawi, ambayo itakuwa zama za kutawala kwa uadilifu, na utawala wa maadili na uzuri, na mahusiano hujengeka juu ya msingi wa udugu na usawa, maradhi ya mwili na akili ya mwanadamu yatatoweka, na nguvu za kimwili na kiroho za mwanadamu zitakuwa zenye nguvu na uimara wa ajabu.

Imam Sajjad (as) anasema:

«إِذَا قَامَ الْقَائِمُ أَذْهَبَ اللَّهُ عَنْ كُلِّ مُؤْمِنٍ الْعَاهَةَ وَ رَدَّ إِلَيْهِ قُوَّتَهُ.»

"Wakati Qa'im (as) atakaposimama, Allah atawaondolea waumini kila aina ya ugonjwa na atawarudishia nguvu zao." (Ghaybat Nu'mani, Juzuu ya 1, uk. 317)

Katika serikali ya Bwana huyo mtukufu, ambapo elimu inakua kwa namna ya kustaajabisha, hakutabaki maradhi yoyote yasiyo na tiba, na afya na tiba vitapiga hatua kubwa, na pia kwa baraka ya kuwepo kwake, wagonjwa wengi watapona.

5. Kheri na Baraka Tele
Miongoni mwa matunda makubwa ya serikali ya Qa'im Aal-Muhammad (as) ni kheri na baraka tele zisizo na mfano. Katika kipindi cha dola yake, kila mahali patakuwa na uhai na uchangamfu, na maisha yatanawiri. Mbingu itamimina mvua, na ardhi itatoa mazao, na baraka za Allah zitakuwa nyingi na zisizo na mwisho.

Imam Swadiq (as) anasema:

«یَسُوقُ اللَّهُ تَعَالَی بِهِ بَرَکَاتِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ فَیُنْزِلُ السَّمَاءُ قَطْرَهَا وَ یُخْرِجُ الْأَرْضُ بَذْرَهَا

Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa baraka yake (Imam Mahdi - amani iwe juu yake), atateremsha baraka za mbingu na ardhi. [Katika zama za serikali yake], mbingu itamimina mvua na ardhi itatoa mbegu." (Ghaybat Shaykh T'usi, Juzuu ya 1, uk. 188)

6. Kukomeshwa kwa Umaskini
Wakati rasilimali zote za ardhi zitakapofunuliwa kwa Imam Mahdi (as), na baraka za mbingu na ardhi zitakapomiminwa kwa watu wa zama zake, na zikasambazwa kwa uadilifu, hakutabakia nafasi yoyote kwa umaskini na uhitaji. Ulimwengu katika serikali ya Imam Mahdi (as) utasalimika milele kutokana na makucha ya umaskini na uhitaji.

Katika zama zake, uhusiano wa kiuchumi utajengwa juu ya msingi wa udugu na usawa, na dhana ya kutafuta faida binafsi na kujinufaisha itapotea, na badala yake, moyo wa huruma, kujali na kushirikiana na udugu wa kidini utatawala, na kwa hali hii, kila mtu atamtazama mwenzake kama mshiriki wa familia moja. Hivyo basi, harufu ya umoja na mshikamano itasikika kila mahali.

Imam Baaqir (as) anasema katika suala hili:

«وَ یُعْطِی النَّاسَ عَطَایَا مَرَّتَیْنِ فِی السَّنَةِ وَیَرْزُقُهُمْ فِی الشَّهْرِ رِزْقَیْنِ وَ یُسَوِّی بَیْنَ النَّاسِ حَتَّی لاَ تَرَی مُحْتَاجاً إِلَی اَلزَّکَاةِ.»

Na atawapa watu kipawa mara mbili kwa mwaka, na atawapa riziki mara mbili kwa mwezi, na atafanya usawa kati ya watu kiasi kwamba hutamwona mtu yeyote anayeihitaji zaka." (Bihar al-Anwar, Juzuu ya 52, uk. 390)

7. Utawala wa Uislamu na Kutokomezwa kwa Ukafiri
Katika aya tatu za Qur'ani Tukufu, Allah Mtukufu ameahidi kwamba dini tukufu ya Uislamu itakuwa ya ulimwenguni kote:

«هُوَالَّذی اَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدی وَ دِینِ الْحَقِّ لِیظْهِرَهُ عَلَی الدِّینِ کُلِّهِ.»

Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uongofu na dini ya haki, ili kuifanya ishinde juu ya dini zote. (Surah Tawba, aya 33; Surah Fath, aya 28; Surah Saf, aya 9)

Na hapana shaka kwamba ahadi ya Allah ni ya kutekelezwa na haiwezi kuvunjwa, kama Qur'ani inavyosema:

«اِنَّ اللّهَ لایخْلِفُ الْمیعادَ.»

Hakika Allah havunji ahadi yake. (Surah Aal Imran, aya 9)

Hata hivyo, ni wazi kwamba pamoja na jitihada zote na juhudi zisizo na mfano za Mtume (saw) na waja wema wa Allah (as) hadi sasa, jambo hili la heri halijawahi kutokea, na Waislamu wote wanaitarajis kwa shauku kubwa siku hiyo ifike.

Hivyo basi, chini ya utawala wa yule Mteule wa Allah, sauti ya "Ash-hadu an la ilaha illa Allah" ambayo ni bendera ya Tawhid, na sauti ya "Ash-hadu anna Muhammadan Rasulullah" ambayo ni alama ya Uislamu, zitakuwa zinasikika kila mahali, na hakutabaki dalili yoyote ya shirki na ukafiri.

Na hakika, utawala huu wa Uislamu ulimwenguni utakuwa kwa sababu ya haki na uhalisia wa Uislamu, ambao katika zama za Imam Mahdi (as) utadhihirika zaidi na vizuri zaidi, na utavutia mioyo yote kwake.

8. Amani kwa viumbe wote
Katika utawala wa Imam Mahdi (as), ambao ni zama za kustawi kwa kila wema katika kila nyanja ya maisha, usalama, ambao ni moja ya neema kubwa za Allah na ni miongoni mwa matarajio makuu ya mwanadamu, utapatikana.

Imam Ali (as) anasema katika suala hili:

«وَ لَوْ قَدْ قَامَ قَائِمُنَا ... لَذَهَبَتِ الشَّحْنَاءُ مِنْ قُلُوبِ الْعِبَادِ وَ اصْطَلَحَتِ السِّبَاعُ وَ الْبَهَائِمُ حَتَّی تَمْشِیَ الْمَرْأَةُ بَیْنَ الْعِرَاقِ إِلَی الشَّامِ لَا تَضَعُ قَدَمَیْهَا إِلَّا عَلَی النَّبَاتِ وَ عَلَی رَأْسِهَا زِینَتُهَا لَا یُهَیِّجُهَا سَبُعٌ وَ لَا تَخَافُهُ.»

"Iwapo Qa'im wetu (as) atasimama, chuki na uhasama vitaondoka katika nyoyo za waja, na wanyama wakali na wanyama wa kufugwa wataishi kwa amani na maelewano, kiasi kwamba mwanamke atatembea kutoka Iraq hadi Shaam (Syria) pasi na kukanyaga isipokuwa kwenye majani, na akiwa amevaa mapambo yake juu ya kichwa chake, hakuna mnyama mkali atakayemletea hofu, wala hatakuwa na khofu yoyote." (Al - Khisaal, Juzuu ya 2, uk. 626)

9. Ueneaji wa Elimu
Katika zama za utawala wa Imam Mahdi (as), siri nyingi za kielimu katika fani za Kiislamu na ubinadamu zitafunuliwa, na elimu ya mwanadamu itapiga hatua kubwa na isiyo na kifano.

Imam Swadiq (as) anasema kuhusiana na hili:

«اَلْعِلْمُ سَبْعَةٌ وَ عِشْرُونَ حَرْفاً فَجَمِیعُ مَا جَاءَتْ بِهِ الرُّسُلُ حَرْفَانِ فَلَمْ یَعْرِفِ النَّاسُ حَتَّی الْیَوْمِ غَیْرَ الْحَرْفَیْنِ فَإِذَا قَامَ قَائِمُنَا أَخْرَجَ الْخَمْسَةَ وَالْعِشْرِینَ حَرْفاً فَبَثَّهَا فِی اَلنَّاسِ وَ ضَمَّ إِلَیْهَا الْحَرْفَیْنِ حَتَّی یَبُثَّهَا سَبْعَةً وَ عِشْرِینَ حَرْفاً.»

"Elimu na maarifa ni herufi ishirini na saba. Yote yaliyokuja na Mitume ni herufi mbili tu. Na watu hadi leo hawajafahamu isipokuwa hizo herufi mbili. Na wakati Qa'im wetu atakaposimama, atazifunua zile herufi ishirini na tano zilizobakia na kuzieneza kwa watu, na ataziunganisha na zile herufi mbili, hadi atazieneza zote, herufi ishirini na saba." (Bihar al-Anwar, Juzuu ya 52, uk. 336)


Utafiti huu unaendelea...

Imenukuliwa kutoka katika kitabu cha “Negin-e Āfarinish” (Lulu ya Uumbaji) huku ikifanyiwa marekebisho kiasi

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha