Kwa mujibu wa sShirika la Habari la Hawza, Hafla hiyo iliandaliwa na Sheikh wa Mkoa wa Mwanza wa Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC), Sheikh Hashim Ramadhani, na ilihudhuriwa na waumini pamoja na viongozi mbalimbali wa dini.
Akizungumza katika hafla hiyo, Sheikh Jalala amewataka Waislamu kutambua na kuthamini nafasi muhimu ya vikao vya Maulidi katika kuimarisha mapenzi kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w.), kumkumbuka na kumswalia, sambamba na kujifunza mwenendo, maadili na mafundisho yake matukufu.
Amesema kuwa; vikao hivyo si fursa ya kusherehekea pekee, bali pia ni nafasi muhimu ya kutafakari ujumbe wa Mtume (s.a.w.w.) na kuufanya kuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya Waislamu.
Aidha, Sheikh Jalala amesisitiza umuhimu wa kudumisha vikao vya dua na dhikri, huku akieleza kuwa ni miongoni mwa njia zinazochangia kuimarisha imani, kumuomba Mwenyezi Mungu msamaha na rehema, pamoja na kuleta utulivu na baraka katika jamii.
Amewahimiza Waislamu kuendeleza utamaduni huo kwa kuzingatia mafundisho sahihi ya dini, huku wakitumia mikusanyiko hiyo kama fursa ya kuimarisha umoja, upendo, mshikamano na udugu miongoni mwa waumini.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini kutoka maeneo tofauti, wakiongozwa na mwenyeji wao, Sheikh wa Mkoa wa Mwanza wa BAKWATA, Sheikh Hassan Kabeke.
Maadhimisho hayo yameendelea kuwa sehemu muhimu ya kuwakumbusha Waislamu juu ya maisha na mafundisho ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.), pamoja na umuhimu wa kuyaendeleza katika familia na jamii kwa ujumla.







Maoni yako