Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Jumuiya hiyo inajumuisha wanafunzi na waumini kutoka nchi kadhaa za Afrika Mashariki na Kati, zikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rwanda, Malawi na nchi nyingine. Hafla hiyo ilifanyika usiku wa kuamkia Jumapili katika mazingira yaliyojaa furaha, upendo na kumbukumbu ya maisha na mafundisho ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.).
Akizungumza katika hafla hiyo, Hujjatul-Islam Sheikh Hashiri Zakaria aliwahimiza waumini kumfanya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) kuwa kigezo chema na mfano wa kuigwa katika maisha yao, akisisitiza kwamba mafundisho yake hayakuwa kwa ajili ya zama zake pekee, bali yanaendelea kuwa mwongozo muhimu kwenye jamii ya leo.
Sheikh Hashiri pia alitoa wito kwa wazazi kuwalea watoto wao kwa kuwafundisha maisha, tabia na mwenendo wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.), ili waweze kumtambua na kumchagua kuwa mfano wao katika maisha. Alieleza kuwa; iwapo wazazi hawatawapa watoto wao mwongozo sahihi na kuwafundisha kuhusu mifano bora ya kuigwa, watoto wanaweza kujitafutia wenyewe watu wengine wa kuwaiga na kuwafuata katika maisha yao.
Katika sehemu nyingine ya mawaidha yake, Sheikh Hashiri alisisitiza wajibu wa Waislamu na wanajamii kwa ujumla kuwatetea watu wanaodhulumiwa, kupinga ufisadi na kukabiliana na vitendo vya watu mafisadi, akieleza kuwa msimamo huo ni miongoni mwa mafundisho muhimu yanayopatikana katika mwenendo wa Mtume Mtukufu (s.a.w.w.).
Akifafanua zaidi, alisema miongoni mwa sifa kubwa za Mtume Muhammad (s.a.w.w.) ilikuwa ni kuwakumbatia wanyonge na kuwajali watu waliokuwa katika mazingira magumu. Alibainisha kuwa Mtume alikuwa na mapenzi makubwa kwa mayatima na aliwasimamia watu waliodhulumiwa, hususan wanawake, katika kipindi ambacho baadhi ya jamii zilikuwa zikiwafanyia ukatili mkubwa, ikiwemo kuwazika watoto wa kike wakiwa hai. Mtume (s.a.w.w.) alisimama dhidi ya dhuluma hizo na kuhimiza heshima, utu na haki kwa mwanadamu.
Aidha, Sheikh Hashiri alizungumzia kwa kina umuhimu wa umoja, mshikamano na amani katika jamii, akiwahimiza waumini kuishi pamoja kwa upole, kuheshimiana na kushirikiana, bila kujali tofauti zao za kiitikadi na kimtazamo. Alisisitiza kwamba; tofauti za kiimani hazipaswi kuwa chanzo cha chuki, uhasama au kuvunjika kwa mshikamano wa jamii.
Hafla hiyo ilihitimishwa kwa kutolewa shukrani kutoka kwa waandaaji kwa waumini wote waliojitokeza kushiriki katika maadhimisho hayo ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Waandaaji pia waliwaombea wahudhuriaji na familia zao kwa Mwenyezi Mungu, wakimtaka awajaalie kheri, baraka, umoja na mafanikio katika maisha yao.
Maadhimisho hayo yamekuwa sehemu ya juhudi za Jumuiya ya Afrika Mashariki Qum katika kuimarisha umoja, mshikamano, malezi ya kiroho na kuhuisha mafundisho ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) miongoni mwa wanafunzi na waumini kutoka Afrika Mashariki wanaoishi na kusoma katika mji wa Qum.
Maoni yako