Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Sherehe hizo zinatarajiwa kufanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam, ambapo Waislamu kutoka maeneo mbalimbali wanatarajiwa kukusanyika kwa ajili ya kushiriki katika hafla hiyo ya kitaifa. Tukio hilo linatarajiwa kuwa miongoni mwa matukio makubwa ya Maulidi yanayofanyika nchini Tanzania kwa mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, sherehe za Maulidi ya Mtume (saww) zitafanyika siku ya Jumatatu, tarehe 24 Agosti 2026, ambapo waumini wanatarajiwa kushiriki katika hafla hiyo kwa pamoja, huku wakionesha upendo wao kwa Mtume Muhammad (saww) na kuhuisha mafundisho yake katika jamii.
Hafla hiyo inatarajiwa kuanza baada ya Swala ya Isha, huku kukiwa na vipengele mbalimbali vya kuadhimisha Maulidi, ikiwemo mawaidha na ujumbe mbalimbali unaohusiana na maisha, mwenendo na mafundisho ya Mtume Muhammad (saww). Waumini wanahimizwa kujitokeza kwa wingi na kushiriki katika tukio hilo la kiimani na kijamii.
Mgeni rasmi katika sherehe hizo anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
BAKWATA inawaalika Waislamu wote kushiriki kwa wingi katika sherehe hizo za kitaifa, katika kuadhimisha kwa pamoja kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (saww) na kuendeleza ujumbe wa upendo, amani, umoja na mshikamano katika jamii ya Tanzania.


Maoni yako