Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Hafla hiyo inatarajiwa kufanyika siku ya Jumapili, tarehe 30 Agosti 2026, inayolingana na 17 Rabiul-Awwal 1448 Hijria. Waandaaji wa hafla hiyo wamewaomba waumini kujitokeza kwa wingi ili kushiriki katika kuadhimisha siku hii tukufu na kujifunza zaidi kuhusu maisha, mwenendo na mafundisho ya Mtume Muhammad (saww).
Kwa mujibu wa taarifa ya waandaaji, hafla hiyo itaanza saa 20:00 usiku hadi saa 23:00 usiku, ambapo kutakuwa na vipengele mbalimbali vya kusherehekea Maulidi ya Mtume (saww), yakitanguliwa na zafa, katika mazingira ya furaha na mshikamano wa Kiislamu. Hafla hiyo pia inatarajiwa kuwa fursa ya kuwakutanisha waumini katika kushirikiana katika kheri na kuhuisha mapenzi yao kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww).
Mgeni rasmi anayetarajiwa kuhudhuria hafla hiyo ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Patrobas Katambi, ambaye anatarajiwa kuwa sehemu ya tukio hilo muhimu pamoja na viongozi wa dini, waumini na wadau mbalimbali. Uwepo wa viongozi katika hafla kama hiyo unatarajiwa kuongeza umuhimu na uzito wa sherehe hiyo, huku ukitoa nafasi ya kuimarisha mahusiano na ushirikiano katika jamii.
Uongozi wa Hawza ya Imam Swa’diq (as) na Jumuiya ya Shia Ithnaasharia Tanzania (TIC) unawakaribisha waumini wote kushiriki kwa wingi katika sherehe hii adhimu ya Maulidi ya Mtume Muhammad (saww). Hafla hiyo inatarajiwa kuwa ya kipekee, yenye ujumbe wa upendo, umoja, furaha na kumuenzi Mtume (saww), hivyo waumini wanahimizwa kuitumia fursa hiyo kusherehekea kwa pamoja siku hii yenye heshima na baraka.

Maoni yako