Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Naim Qassem, Katibu Mkuu wa Hizbullah, katika hotuba yake kwenye tamasha kuu la Kinabii la “Mtume wa Walio Huru”, lililoandaliwa na Hizbullah katika Uwanja wa Ashura, katika vitongoji vya kusini mwa Beirut, alisisitiza: Mtume wetu, Mtukufu Muhammad (s.a.w.w.), ni Mtume wa watu walio huru; watu hao walio huru ambao hufungua akili na nyoyo zao zilizo safi na angavu ili kufahamu ukweli unaowaletea saada duniani na Akhera.
Alisema: “Leo tunaadhimisha Maulid ya Mtume wa Walio Huru, Mtukufu Muhammad (s.a.w.w.), na kwa mnasaba wa tukio hili, tutazungumzia kuzaliwa huku kulikobarikiwa na nafasi kubwa ya Bwana wa Mitume na Manabii kwa wanadamu wote, na pia tutazungumzia baadhi ya mambo, likiwemo suala la kisiasa la nchi yetu.”
Aliendelea kusema: “Leo tunaona kwamba Marekani na wote wanaotembea katika mstari wa ushirikina, upotovu na ukafiri, ni umma mmoja (upande mmoja).
Sheikh Qassem alisema: “Kuweni na umoja, na tunaposema umoja wa Kiislamu, hatumaanishi tu umoja wa dhamira, hisia na umoja katika maneno na istilahi, bali tunakusudia umoja unaosababisha Waislamu kupata nguvu na unaowezesha kufikiwa kwa maendeleo, ushirikiano na mshikamano miongoni mwao, hususan baina ya nchi na mataifa.” Alifafanua: “Umoja ni kwa ajili ya kuukomboa Umma kutokana na kufuata ukoloni, upotovu na ubeberu; ni kwa ajili ya kuukomboa Umma kutokana na kunyang’anywa utambulisho wake wa kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa; umoja ni kwa ajili ya kukabiliana na miradi ya kuchochea fitina miongoni mwa Waislamu, na kwa ajili ya kukabiliana na lugha ya chuki na kinyongo, pamoja na wale wanaoweka vikwazo vya kimadhehebu, kidini na kisiasa baina ya Waislamu.”
Aliongeza: “Umoja ni kwa ajili ya kukabiliana na miradi ya kuigawanya nchi ambayo serikali dhalimu ya Marekani inaifuatilia, huku ikisaidiwa na Israel mhalifu, ili kuisambaratisha na kulivuruga eneo letu.”
Sheikh Qassem aliendelea: “Kwa upande wa umoja, kuna matokeo mawili ya kivitendo tunayoyahitaji. Kwanza, tuwe na umoja katika kuzuia fitina, na umoja huu upanuke kutoka umoja wa Kiislamu kwenda umoja wa kitaifa na kisha umoja wa kibinadamu, na hakuna kizuizi chochote cha umoja huu kuwahusisha watu wote huru duniani. Matokeo ya pili ya umoja ni kuwa na umoja kuhusiana na suala kuu, yaani suala la Palestina, ukombozi wa Palestina na Msikiti wa Al-Aqsa.”
Katibu Mkuu wa Hizbullah alisisitiza: “Suala la Palestina ni suala la umoja wa Kiislamu, wala si suala la Masunni, Mashia au watu wa madhehebu fulani; bali ni suala la Kiislamu, kitaifa, kikabila, Kiarabu na kibinadamu.”
Sheikh Qassem aliziomba nchi za Kiarabu na Kiislamu pamoja na mataifa yao kujitahidi kufikia umoja, akisema: “Wakati umefika wa kuwa pamoja, na eneo letu liwe salama kupitia maelewano baina ya nchi za eneo hili, na kukomeshwe ubeberu na zana zake zote katika eneo letu.”
Sheikh Qassem: Imam Musa Sadr alikuwa mfano wa uadilifu na ubinadamu
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Sheikh Naim Qassem alisema: “Imam Musa Sadr alikuwa alama, bendera na mfano, na alikuwa na uwezo na nyenzo mbalimbali.” Alieleza kwamba shakhsia ya Imam Sadr ilikuwa na nyanja za kidini, kijamii, kiutamaduni, kisiasa na kibinadamu, na akabainisha: “Imam Musa Sadr tangu mwanzo alikuwa macho dhidi ya hatari za utawala wa Kizayuni, na aliibua kauli yake maarufu: ‘Israel ni shari tupu.’”
Alifafanua: “Imam Musa Sadr pia alitaka kufanyika kwa mageuzi ya kisiasa nchini, na tangu mwanzo kabisa aliibua wazo la kuwasaidia watu waliodhulumiwa na wenye mahitaji. Aidha, aliipa kusini mwa Lebanon umuhimu wa kipekee na akawaambia wote: ‘Lebanon na kusini yake haiwezi kutabasamu wakati inateswa.’”
Katibu Mkuu wa Hizbullah aliendelea: “Wakati Imam Sadr alipokuwa akijitahidi kuikomboa kusini kutokana na uvamizi wa ‘Israel’ na mashambulizi yake, pia alizingatia mageuzi ya kisiasa na kijamii. Hivyo, tunaelewa kwa nini Imam Sadr alitekwa nyara, kwa sababu alikuwa mfano wa uadilifu na ubinadamu.”
Aliongeza: “Tunamkumbuka kwa heshima na fahari Sayyid wa Mashahidi wa Umma, Sayyid Hassan Nasrullah; mtu ambaye daima alikuwa akikumbusha sifa na upekee wa Imam wa Muqawama nchini Lebanon, yaani Imam Sadr. Sayyid wa Mashahidi wa Umma daima alisisitiza umoja wa Kiislamu na umoja wa kitaifa, na hii ndiyo njia ambayo, Inshaallah, tutaendelea nayo.”
Sheikh Qassem: Muqawama katika eneo ulisimama dhidi ya miradi ya kugawanya nchi na kuikalia kwa mabavu
Aidha, Sheikh Qassem alisisitiza: “Eneo hili leo lipo katikati ya mchakato wa kihistoria wa kuijenga upya taswira yake na uwiano wa nguvu. Tunashuhudia matukio yasiyo ya kawaida; Marekani inaandaa njia ya kuongeza utawala wake na kuweka misingi muhimu kwa ajili ya kuibuka kwa ‘Israel Kubwa’, huku ikitumia uwezo wake na hali ya kujisalimisha iliyopo katika eneo letu.”
Aliendelea: “Katika kukabiliana na Marekani, Iran ilisimama. Harakati iliyobarikiwa ya Jamhuri ya Kiislamu, pamoja na Muqawama nchini Palestina, Lebanon, Iraq, Yemen na katika eneo lote, zimesimama dhidi ya miradi ya kugawanya nchi, ukaliaji wa mabavu, ubeberu na udhamini wa kigeni.”
Alibainisha: “Maadui hawakuacha fursa yoyote ya kufanya mashambulizi, lakini hawakufanikiwa na hawatafanikiwa. Hawakufanikiwa kwa mauaji, wala kwa mzingiro wa kiuchumi, wala kwa shinikizo la kutaka kujisalimisha, wala kwa jitihada za kuwahamisha watu kwa lazima, wala kwa jitihada za kuwatenganisha watu na Muqawama; kwa sababu maadui walishangazwa na kuwaona watu wakiwa wameungana na tayari kujitolea mhanga kukubwa.”
Sheikh Naim Qassem alisisitiza katika muktadha huu: “Ingawa kujitolea ni kukubwa, lakini ni kujitolea huku ndiko kulikosimamisha mradi wa uchokozi. Tumeyatoa muhanga mambo mengi, lakini hatukushindwa; kwa sababu kushindwa kunatokea pale tunapojisalimisha. Marekani inakabiliwa na kushindwa katika hali yake ya kiuchumi na katika mtazamo wa dunia kuhusu uhalisia wake.”
Sheikh Qassem pia alisema: “Marekani leo si tena mfano wala alama, bali mataifa ya dunia yanaitazama kama mkoloni, dhalimu na muuaji, na hasara zake pia zinazidi kujitokeza hatua kwa hatua; kiasi kwamba leo deni la Marekani limefikia dola trilioni 40.”
Alisisitiza: “Utawala wa Israel pia unakabiliwa na kushindwa, kwa sababu uhamiaji (kutoka nchini) unaongezeka, hali ya uchumi inazidi kuwa mbaya, na hasara zitakuwa kubwa zaidi.”
Sheikh Qassem: Serekali ya Lebanon imechagua njia ambayo si ya fahari kwa Lebanon
Katibu Mkuu wa Hizbullah, alipokuwa akizungumzia uongozi wa Lebanon na “mazungumzo ya moja kwa moja” na adui, alisema kwamba uongozi wa Lebanon umechagua njia ambayo si ya heshima kwao, wala si ya fahari kwa Lebanon, wala si ya fahari kwa kujitolea kwa Walebanon, na umeingia katika mazungumzo ya moja kwa moja na adui Mwisraeli na kumpa kila alichotaka.
Sheikh Qassem aliuelekezea uongozi huo maneno haya: “Niambieni, mmepata nini kutokana na mazungumzo ya moja kwa moja?” Alisisitiza: “Wale waliopigana na kujitolea, pamoja na wale walioandamana nao na kupata msaada kutoka katika makundi yote ya Walebanon, wanachukizwa na makubaliano haya ya kutoa ushawishi na matokeo haya.”
Sheikh Qassem aliwauliza wale wanaosema “mazungumzo ni bora kuliko vita” swali hili: “Je, mazungumzo yenu yalisimamisha vita?”
Aliendelea kusema: “Mazungumzo yanafanyika chini ya moto wa vita na yanavipa vita uhalali, na mazungumzo haya si ya kukabiliana na vita, bali ni mazungumzo ambayo jina lake ni kujisalimisha kwenye udhalili, bila kupata mafanikio yoyote.”
Katibu Mkuu wa Hizbullah alirejea kulielekeza tena neno lake kwa uongozi na kusema: “Mngelikwenda katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na kuweka masharti. Tafuteni mpatanishi mwingine badala ya mpatanishi wa Marekani.”
Alisema: “Sisi pia hatutaki vita, na sababu ya hilo ni kwamba tulitia saini makubaliano tarehe 27 Novemba 2024 (7 Azar 1403), na kile kinachoendelea leo ni uchokozi wa wazi wa Israel.”
Sheikh Qassem alisisitiza: “‘Makubaliano ya Mfumo’ ni kinyume cha sheria ya Kiislamu na ni kinyume cha sheria, na ni makubaliano ya udhalili yanayouangamiza uongozi wa Lebanon na hayarejeshi haki. Sisi tunapinga ‘Makubaliano ya Mfumo’ na tunataka yafutwe.”
Sheikh Qassem: Tutaendelea kubaki katika uwanja wa mapambano na tumeuvunja “Mradi wa Israel Kubwa”
Aidha, Sheikh Qassem alisisitiza: “Tutaendelea kubaki katika uwanja wa mapambano, na hatutakubali miradi hii wanayoizungumzia; kwa sababu tumeuvunja ‘Mradi wa Israel Kubwa’, na tumefanikisha kuzuia wasifike katika mji mkuu, Beirut. Pia tumefanikisha kuzuia wasituvue nguvu na silaha zetu, ili Lebanon isidhoofike na wao wasiweze kuitawala na kuanza kujenga makazi yao.”
Alisisitiza: “Pamoja na kuwepo kwa Muqawama huu, pamoja na watu wake, pamoja na watu wenye heshima, pamoja na mashahidi na pamoja na kujitolea huku, hawawezi kufanikisha chochote.” Alisema: “Tumewaambia na tunarudia kuwa sisi, katika kutimiza malengo, tunafuata shule ya Karbala.”
Aidha, Sheikh Qassem alizisemesha familia za Muqawama akisema: “Tutashirikiana na kuwasaidia kwa kadiri tuwezavyo kwa ajili ya kulinda heshima yenu, na Inshaallah, kila jambo lina suluhisho. Tutaendelea kuwa na fahari na hatutajisalimisha, kwa sababu sisi ni wana wa heshima, sisi ni wana wa utukufu, na udhalili uko mbali nasi.”
Mwisho alisema: “Nawapongeza Waislamu na watu wote duniani kwa mnasaba wa Maulid ya Mtume Mtukufu, Muhammad, Bwana wa Manabii na Mitume (s.a.w.w.).”
Maoni yako