Jumamosi 5 Septemba 2026 - 14:33
Marjaiya, Maombolezo ya Ashura na Wilaya ni Nguzo Tatu Imara za Ushia Dhidi ya Ukoloni

Hawza/ Ayatullah Hafiz Riyadh Hussein Najafi, Mkuu wa Shirikisho la Madrasa za Kishia Pakistan (Wifaq al-Madaris al-Shia Pakistan), amesisitiza kwamba Marjaiya, maombolezo ya Ashura na Wilaya ya Amirul-Muuminina (as) ni miongoni mwa nguzo muhimu zinazolinda na kuimarisha madhehebu ya Shia. Amesema vipengele hivyo vitatu ni miongoni mwa sababu kuu zilizowawezesha Mashia kusimama imara na kupambana na njama za ukoloni, huku maadui wakiendelea kujaribu kuudhoofisha Ushia kwa kulenga nguzo hizo.

Kwa mujibu wa idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Hafiz Riyadh Hussein Najafi alisema hayo katika khutuba za Swala ya Ijumaa iliyofanyika katika Msikiti Mkuu wa Ali (as), uliopo katika Chuo cha Kiislamu cha Jamiatul Muntazar mjini Lahore, Pakistan.

Alisema kwamba, baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, maadui walitambua ukweli kwamba moja ya nguvu kubwa zaidi za Mashia ni Marjaiya, nguvu ambayo katika kipindi chote cha historia imekuwa na nafasi muhimu katika kulinda na kuhifadhi madhehebu ya Shia.

Rais huyo wa Shirikisho la Madrasa za Shia Pakistan, aliongeza kuwa; nguvu ya pili kubwa ya Ushia ni maombolezo, huku nguvu ya tatu na yenye nguvu zaidi ikiwa ni Wilaya ya Amirul-Muuminina (as).

Alisema uwepo wa nguzo hizo tatu umeifanya jamii ya Mashia leo kusimama imara mbele ya ukoloni. Kwa sababu hiyo, alisema, nguvu za kikoloni zimekuwa zikibuni njama mbalimbali kwa lengo la kuudhoofisha Ushia kwa kulenga nguzo hizo tatu.

Uislamu Unaendelea Kuenea Duniani

Akizungumzia kuenea kwa Uislamu duniani, Ayatullah Riyadh Najafi alisema: “Karne ya sasa ni karne ya Waislamu, na Uislamu ni miongoni mwa dini zinazoenea kwa kasi zaidi duniani.”

Alisema Waislamu leo wako katika njia ya maendeleo na kwamba, kwa mujibu wa aya za Qur’ani na riwaya, Uislamu utaendelea kuenea zaidi katika siku zijazo, hususan katika nchi za Ulaya, ikiwemo Uingereza.

Karbala ni Alama ya Kudumu Katika Dini na Uislamu

Ayatullah Riyadh Najafi pia alizungumzia nafasi ya Mapambano ya Ashura, huku akisema: “Karbala ni alama ya kubaki hai dini na madhehebu ya Uislamu.”

Alieleza kwamba; kumbukumbu na jina la Karbala lilifikia kilele wakati wa Imam Muhammad al-Baqir (as) na Imam Jaafar al-Sadiq (as). Alisema Maimamu hao wawili wakubwa walikuwa wakiwaalika washairi katika vikao vya maombolezo, kusikiliza mashairi yao kuhusu Ahlulbayt (as) na tukio la Karbala, na kisha kuwapatia zawadi.

Alifafanua kwamba, misingi ya kwanza ya kueneza na kuhuisha kumbukumbu ya Karbala iliwekwa kupitia juhudi za Maimamu hao wawili wakuu. Ndiyo maana, alisema, leo jina na kumbukumbu ya Karbala vinasikika na kuenea katika maeneo mbalimbali duniani.

Misingi ya Ijtihadi Iliimarishwa Katika Enzi ya Imam Jaafar al-Sadiq (as)

Ayatullah Hafiz Riyadh Najafi pia alizungumzia nafasi ya kielimu ya Imam Jaafar al-Sadiq (as), huku akisema kwamba misingi ya Ijtihadi iliimarishwa katika zama zake.

Alisema Imam Jaafar al-Sadiq (as) aliwafundisha wanafunzi wake namna ya kutoa na kubaini hukumu za kisheria kutoka katika Qur’ani na Hadithi, huku wanafunzi wake wengi wakibobea katika elimu za fiqhi.

Mkuu huyo wa Shirikisho la Madrasa za Shia Pakistan aliongeza kuwa, Mtume Muhammad (saww) alianza mchakato wa elimu na malezi katika Msikiti wa Mtume (saww), lakini Imam Jaafar al-Sadiq (as) aliendeleza mchakato huo wa kielimu na kuupeleka katika kiwango cha taasisi kubwa ya elimu kama chuo kikuu.

Alisema takribani wanafunzi 4,000 walikuwa wakishiriki katika darsa za Imam Jaafar al-Sadiq (as), huku hata wanafunzi kutoka maeneo ya India na Sindh wakihudhuria masomo mbele ya Imam huyo.

Jabir bin Hayyan, Mwanasayansi Maarufu, Alikuwa Mwanafunzi wa Imam Jaafar (as)

Katika sehemu nyingine ya khutuba yake, Ayatullah Riyadh Najafi alizungumzia mchango wa Imam Jaafar al-Sadiq (as) katika kuchanua elimu mbalimbali.

Alisema Jabir bin Hayyan, ambaye hutajwa kama baba wa elimu ya Kemia, alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa Imam Jaafar al-Sadiq (as), na kwamba urithi wake wa kielimu ulikuwa na mchango mkubwa katika kuibuka na kuendelea maendeleo ya taaluma mbalimbali za kisayansi.

Rabiul-Awwal, Mwezi wa Furaha na Shangwe

Akihitimisha hotuba yake, Ayatullah Riyadh Najafi alizungumzia fadhila za mwezi wa Rabiul-Awwal, akisema tarehe 17 Rabiul-Awwal ni kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume Mtukufu Muhammad (saww) pamoja na Imam Jaafar al-Sadiq (as).

Kwa sababu hiyo, alisema, Rabiul-Awwal ni mwezi wa furaha na shangwe kwa Waislamu. Aidha, alieleza kwamba, Hijra ya Mtume Mtukufu (saww) kutoka Makka kwenda Madina, pamoja na mkataba wa udugu baina ya Waislamu mjini Madina, pia vilitokea katika mwezi huu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha