Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Jumuiya ya Kitaifa ya Kiislamu ya Al-Wifaq ya Bahrain, ambayo ni moja ya harakati kubwa za mapinduzi nchini humo, imelaani Amri ya Kifalme Na. 38 ya mwaka 2026. Amri hiyo imeongeza vifungu vipya katika Sheria ya Mikoa, vinavyoruhusu kuteuliwa kwa “Mukhtar mmoja au zaidi” (kiongozi wa eneo) katika kila mkoa kwa uamuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani.
Katika taarifa yake, jumuiya hiyo imesema kuwa uamuzi huo unaonyesha kurudi nyuma utawala kutoka katika mfumo wa “dola yenye taasisi za kisasa” na kuelekea kwenye “mifumo ya kikabila/masheikh.” Aidha, imesisitiza kwamba, mamlaka za Bahrain zinaendelea na mtazamo wao wa kipolisi na kiusalama.
Jumuiya hiyo imeeleza kuwa licha ya majukumu ya kihistoria ya Mukhtar kuhusishwa zaidi na masuala ya kijamii, amri hiyo ya kifalme imewaweka Mukhtar chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hali hii inaonyesha kuwa utawala unaendelea kufuata njia mpya za kuiweka dola katika mfumo wa kijeshi na kuimarisha udhibiti wa kiusalama juu ya mambo ya kila siku ya maisha katika jamii.
Jumuiya hiyo imeongeza kuwa, jambo hilo linaashiria dhima ya kiusalama ambayo mfumo mpya wa Mukhtar utakuwa nayo, hasa kwa kuwa amri hiyo imeeleza wazi katika Kifungu Na. 11 kwamba Waziri wa Mambo ya Ndani ndiye atakayeamua mamlaka, majukumu na namna ya kusimamia shughuli za kazi za Mukhtar.
Jumuiya ya Al-Wifaq imeendelea kusema kuwa, wakati nchi mbalimbali zinaelekea katika mifumo ya kiutawala ya kidemokrasia, mamlaka nchini Bahrain imejitenga na muktadha wake wa kihistoria na kuirejesha nchi katika zama zilizotangulia kuanzishwa kwa dola ya kisasa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, amri ya kifalme inamtaka Waziri wa Mambo ya Ndani kuwateua Mukhtar moja kwa moja na bila kushauriana na wakazi wa maeneo husika, achilia mbali kuwapa wananchi haki ya kuwachagua au kugombea nafasi hizo kwa njia za kawaida za kidemokrasia.
Shirika rasmi la habari la Bahrain, BNA, liliripoti kuwa Mfalme wa Bahrain, Hamad Isa Al Khalifa, ametoa amri ya kurekebisha baadhi ya vifungu vya Amri ya Sheria Na. 17 ya mwaka 2002, kupitia Amri Na. 38 ya mwaka 2026.
Kwa mujibu wa marekebisho hayo, Mukhtar mmoja au zaidi watateuliwa katika kila mkoa kwa uamuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani, kutoka miongoni mwa majina yatakayopendekezwa na Gavana wa mkoa husika.
Muda wa uteuzi wao utakuwa miaka minne, na unaweza kuongezwa kwa kipindi kimoja au zaidi. Aidha, Waziri wa Mambo ya Ndani anaweza, kwa pendekezo la Gavana husika, kumuondoa Mukhtar katika nafasi yake kabla ya kumalizika muda wake wa uteuzi.
Maoni yako