Jumatatu 31 Agosti 2026 - 14:13
Maulidi ya Mtume (s.a.w.w.) Yanatufundisha Umoja na Kuepukana na Mifarakano

Hawza/ Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania, Dk. Sheikh Alhadi Mussa Salum, amesema: Maadhimisho ya Maulidi ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) yamebeba ujumbe mkubwa wa umoja wa Kiislamu, huku akisisitiza kuwa Waislamu wanapaswa kuungana na kushirikiana katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili.

Kwa mujibu wa shirika la habari la hawza, akianza hotuba yake, Sheikh Alhadi Mussa alirejea kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Qur’ani Tukufu isemayo:

 {وَإِنَّ هَـٰذِهِۦۤ أُمَّتُكُمۡ أُمَّةࣰ وَٰحِدَةࣰ وَأَنَا۠ رَبُّكُمۡ فَٱتَّقُونِ} 


Na kwa yakini huu Umma wenu ni Umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi, basi nicheni Mimi.
[Surah Al-Muʾminūn: 52]

Akiifafanua aya hiyo Sheikh Alhadi alisema: Waislamu wamekusudiwa kuwa umma mmoja, hivyo ni vyema kufuata mafundisho haya adhimu kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kuacha mifarakano isiyo na faida yeyote ile kwa Waislamu.

Maulidi Yawakutanisha Waislamu wa Madhehebu Tofauti

Sheikh Alhadi amesema hafla hiyo ya Maulidi imekuwa mfano wa wazi wa umoja wa Waislamu, baada ya masheikh na waumini wa Kisunni kuhudhuria pamoja na Waislamu wa Shia. Amesema picha hiyo ya Waislamu kukutana katika mazingira ya upendo na kuheshimiana ndiyo aina ya umoja ambao viongozi wa dini wamekuwa wakiihubiri kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa Sheikh Alhadi, hali hiyo ni ishara chanya kwamba juhudi za kuhimiza umoja wa Kiislamu zinaanza kuzaa matunda. Amesema kuwa; ni jambo la kushukuru kuona Waislamu wenye mitazamo tofauti wakikusanyika kwa pamoja kwa ajili ya kumuenzi Mtume Muhammad (s.a.w.w.) na kushirikiana katika mambo yanayowaunganisha.

Kumpenda Mtume (s.a.w.w.) ni Wajibu wa Kiimani

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Sheikh Alhadi Mussa Salum alisisitiza kuwa; kumpenda Mtume Muhammad (s.a.w.w.) si jambo la hiari kwa Muislamu, bali ni wajibu unaohusiana moja kwa moja na ukamilifu wa imani. Amesema imani ya mja haiwezi kukamilika mpaka ampende Mtume Mtukufu kuliko anavyowapenda watoto wake na familia yake.

Ameeleza kuwa; mapenzi hayo yanapaswa kudhihirika kupitia kufuata mafundisho, mwenendo na maadili ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.), badala ya kubaki katika maneno pekee. Kwa mtazamo huo, maadhimisho ya Maulidi yanapaswa kuwa fursa ya kuhuisha mapenzi kwa Mtume na kuimarisha uhusiano wa waumini na mafundisho yake.

Waislamu Waungane Katika Kutatua Changamoto Zao

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Manai Tanzania (JAMT), amewahimiza Waislamu kuungana na kushirikiana katika kutatua matatizo na changamoto zinazowakabili, akisisitiza kuwa tofauti zilizopo hazipaswi kuwa kikwazo cha ushirikiano katika mambo ya msingi yanayowahusu Waislamu wote.

Amesema umoja wa kweli unahitaji Waislamu kujenga mawasiliano, kuheshimiana na kushirikiana katika mambo yenye manufaa kwa jamii. Kwa kufanya hivyo, amesema, Waislamu wataweza kukabiliana kwa pamoja na changamoto zao badala ya kutumia nguvu zao katika migawanyiko na mivutano isiyokuwa na manufaa.

Udugu wa Kidini, Kibinadamu na Kitaifa

Aidha, Sheikh Alhadi Mussa amesisitiza kuwa umoja haupaswi kuishia kwa Waislamu pekee, bali unapaswa kuwahusisha wanadamu wote. Amesema kuna aina mbalimbali za udugu zinazowaunganisha watu, zikiwemo udugu wa kidini, udugu wa kibinadamu na udugu wa kitaifa, hivyo ni muhimu kujiuliza chanzo cha uadui kinatokana na nini wakati wanadamu waunganishwa kwa kupitia misingi hiyo.

Akihitimisha hotuba yake, Sheikh Alhadi ametoa wito kwa watu kuwa kitu kimoja, kuimarisha upendo na mshikamano na kuachana na mifarakano. Amesema ujumbe wa Maulidi unapaswa kuwa chachu ya kuijenga jamii yenye umoja, amani na kuheshimiana, huku Waislamu wakitumia mafundisho ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) kama msingi wa kuunganisha nyoyo na kuondoa migawanyiko.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha