Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, hafla hiyo ilifanyika chini ya uongozi wa Imamu Mkuu wa Msikiti wa Ahlulbayt, Sheikh Abdallah Hassan Zuber, ambaye aliongoza shughuli za maadhimisho hayo yaliyolenga kuwakumbusha waumini na washiriki umuhimu wa kuyazingatia mafundisho ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) katika maisha ya kila siku.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania, akiwemo Sheikh Abdulghani Khatibu kutoka Kenya, ambaye alishiriki katika kuadhimisha siku hiyo muhimu pamoja na waumini wa Msikiti wa Ahlulbayt na washiriki wengine waliojitokeza.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Sheikh Abdulrazaki Amiri kutoka Arusha, ambaye alishiriki katika kutoa ujumbe wa maadhimisho hayo na kusisitiza umuhimu wa kujifunza na kuishi kwa kuzingatia mafundisho na mwenendo mwema wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.).
Maulidi hayo yaliendeshwa chini ya kaulimbiu isemayo: “Mafundisho ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) yanamkuza mtu kiakili, kiroho na kimaadili,” huku ikisisitiza nafasi ya mafundisho ya Mtume katika kumjenga mwanadamu mwenye fikra sahihi, moyo ulioimarika kiroho na tabia njema. Kaulimbiu hiyo pia ilitoa wito kwa waumini kuifanya Sira ya Mtume kuwa msingi wa malezi na ujenzi wa jamii yenye maadili mema.




Maoni yako