Jumatatu 31 Agosti 2026 - 09:28
Khatibu Mashuhuri wa Kishia Nchini Bahrain Akamatwa; Kisingizio cha Usalama au Kukabiliana na Mimbari za Kidini?

Hawza/ Hakuna akaunti yoyote au jukwaa lolote la habari linalounga mkono na kuhusishwa na serikali nchini Bahrain ambalo halijachapisha tena habari za kukamatwa kwa mhubiri wa Husaini, “Sheikh Jasim Al-Haddad”.

Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, likinukuu “Mir’at Bahrain”, hakuna akaunti yoyote au jukwaa lolote la habari linalounga mkono na kuhusishwa na serikali nchini Bahrain ambalo halijachapisha tena habari za kukamatwa kwa mhubiri wa Husaini, “Sheikh Jasim Al-Haddad”.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Bahrain haikulitaja jina la Sheikh Al-Haddad, lakini ilikabidhi jukumu hilo kwa vibaraka wake wa kielektroniki, ambao walianzisha kampeni kali na yenye uchochezi dhidi ya mhubiri huyo.

Kutafuta tusi au tuhuma katika maneno yake ni karibu kuwa kazi isiyowezekana. Baadhi ya akaunti zenye chuki na misimamo mikali zilichapisha kipande cha video ambacho, kwa mujibu wa madai yao, kilidai kwamba Sheikh Al-Haddad “wakati wa kusimulia riwaya kuhusu hitilafu iliyotokea miaka 1,400 iliyopita, aliwatukana Maswahaba”. Wengine pia walifanya juhudi kubwa za kuwatukana moja kwa moja wahudumu na wahubiri wa Husaini.

Tukio hili limeonesha kiwango cha chuki ambacho kimejikita miongoni mwa watu wanaohusishwa na serikali ya Bahrain, na limeonesha jinsi uadui huu wote dhidi ya Mashia unavyoendeshwa na namna wanavyousukuma mbele; jambo ambalo Sheikh Jasim ni mfano hai wake, kwa sababu tu itikadi na mitazamo ya kundi hili haiendani na maoni ya watawala.

Tukio hili linathibitisha kwamba suala hili, katika kiini chake, halihusiani na kauli iliyotolewa katika majlisi ya kidini wala na kulinda “usalama na utulivu wa umma”, kama ilivyoelezwa katika taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Bali linahusiana na namna tofauti za kidini zinavyoshughulikiwa kwa mtazamo na mkabala wa kiusalama; mkabala ambao baadaye hufungua mlango kwa kampeni za uchochezi na kumchafua mhusika mbele ya jamii dhidi ya mwanazuoni wa dini, kwa sababu tu amesimulia tukio la kihistoria au amechukua msimamo wa kidini ambao unaweza kutumiwa kama mwanya wa kumlenga mhubiri.

Jambo hatari zaidi ni kwamba kukamatwa kwa Sheikh Jasim Al-Haddad hakukuishia katika hatua ya kiusalama pekee. Mara tu baada ya kutolewa kwa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani, wimbi kubwa lililoendeshwa na akaunti na majukwaa yanayohusishwa na serikali lilianza; katika hali inayoonesha kwamba tuhuma ya kiusalama ilikuwa utangulizi wa kampeni ya vyombo vya habari iliyoratibiwa sambamba nayo, kwa lengo la kumtambulisha mwanazuoni huyo kwa umma kama mtu anayestahili kulaaniwa na kuhukumiwa, na kumweka mbele ya hadhira pana ya kidini kwa kutumia lugha iliyojaa chuki na uchochezi.

Maana na hatari ya tukio hili iko hasa hapa. Wakati Wizara ya Mambo ya Ndani inapotangaza kukamatwa kwa mtu bila kutaja jina lake, kisha akaunti zinazohusishwa na serikali zikapewa jukumu la kufichua utambulisho wake, kutafsiri tuhuma zinazodaiwa kumkabili na kuhamasisha maoni ya umma dhidi yake, basi hatuko tena mbele ya mchakato wa kisheria pekee; bali tunakabiliana na operesheni iliyounganishwa ambayo huanza kwa kukamatwa kwa kiusalama na kukamilishwa kwa uchochezi wa kielektroniki na kumchafua mtu mbele ya umma.

Kisa cha Sheikh Jasim Al-Haddad kinakwenda mbali zaidi ya suala la kukamatwa kwa mtu mmoja; tukio hili linaonesha ni kwa kiwango gani tofauti za kiitikadi zinaweza kubadilishwa kuwa chombo cha shinikizo la kiusalama dhidi ya wanazuoni wa Kishia nchini Bahrain. Swali ambalo daima hujitokeza katika mfululizo huu wa kukamatwa na kuzuiliwa ni hili: Je, serikali nchini Bahrain imefikia hatua ya kumuwekea mwananchi mipaka ya kuamua kile anachoruhusiwa kukiamini na kile anachoruhusiwa kukisimulia katika hafla ya kidini?

Uchochezi ambao Sheikh Al-Haddad alikabiliwa nao baada ya kukamatwa si jambo la pembeni katika suala hili, bali ni sehemu ya maana na dhana yake kuu; kwa sababu unaonesha kwamba lengo la adhabu si kukamatwa au kutolewa hukumu ya mahakama pekee, bali pia inakusudiwa kutekelezwa adhabu ya kijamii na ya vyombo vya habari kabla na wakati mmoja na hatua hiyo: kuharibu sura yake, kumvunjia heshima, kuchochea na kusababisha mvutano wa kidini.

Kwa upande mwingine, uhamasishaji huu mpana dhidi ya Sheikh Al-Haddad huenda ukawa umechangia zaidi katika kueneza uwepo wake na kulifanya jina lake lifahamike kwa watu wengi zaidi. Uzoefu unaonesha kwamba jaribio la kuinyamazisha sauti ya mhubiri wa Husaini kwa njia ya kumkamata na kumchochea umma dhidi yake halikomeshi uwepo wake; badala yake, linawasukuma watu kumuulizia, kusikiliza hotuba zake na kutafuta vipande vya video pamoja na mihadhara yake. Kadiri kampeni dhidi yake inavyokuwa kali zaidi, ndivyo udadisi wa umma wa kutaka kufahamu kile alichokisema kwa hakika—mbali na simulizi linaloundwa na akaunti zinazohusishwa na serikali—unavyoongezeka.

Kwa hiyo, huenda serikali ikajikuta ikikabiliwa na matokeo yaliyo kinyume kabisa na yale iliyotaka kuyaona: Sheikh mwenye uwepo mkubwa zaidi, majlisi zenye mahitaji makubwa zaidi ya yeye kuhudhuria, na hadhira pana zaidi inayofuatilia mihadhara na hotuba zake. Kwa sababu Husainia haziendeshwi kwa mantiki ya marufuku za kiusalama, na mimbari ya Husaini hupata umaarufu zaidi pale watu wanapohisi kwamba mwenye mimbari hiyo analengwa kwa sababu ya maneno anayoyasema.

Kile ambacho kampeni hii ililenga kukifikia, yaani kuifikisha sauti ya Sheikh Jasim Al-Haddad kwenye ukimya, huenda kutokana na propaganda hizi dhidi yake kikageuka kuwa jukwaa pana zaidi la kufikisha sauti yake na uwepo mkubwa zaidi wa jina lake katika hafla, makhatibu na wasikilizaji.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha