Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, maandamano hayo yaliyoandaliwa katika Uwanja wa Odenplan na makundi kadhaa ya wanaharakati wa asasi za kiraia nchini Sweden, yalilaani vikali mashambulizi ya Israel na jinai zinazofanywa na utawala huo wa kijeshi dhidi ya Ukingo wa Magharibi na Lebanon.
Waandamanaji walibeba mabango yaliyoandikwa kauli mbalimbali, zikiwemo:
“Watoto wanauawa Ghaza.” “Shule na hospitali zinapigwa mabomu.” “Simamisheni mashambulizi dhidi ya Lebanon.” “Komesheni njaa na uhaba wa chakula.”
Waandamanaji waliutahadharisha utawala wa Kizayuni wanaouelezea kuwa wa umwagaji damu kusitisha operesheni zake za kijeshi huko Ghaza, na wakaishinikiza serikali ya Sweden kusimamisha haraka iwezekanavyo mauzo ya silaha kwa Israel.
Kundi la washiriki kutoka Iran pia lilijiunga na maandamano hayo na kupinga sera za Marekani na Israel. Mwanaharakati wa Kiswidi mwenye asili ya Azerbaijan, Aydin Amirhashemi, ambaye pia alishiriki katika mkusanyiko huo, alisema kuwa; anaamini Israel isingeweza kutekeleza vitendo kama hivyo dhidi ya Wapalestina bila ya msaada wa nchi za Magharibi.
Alisema: “Bila uungaji mkono wa ulimwengu wa Magharibi, Israel isingeweza kufanya maafa haya dhidi ya wananchi wasio na ulinzi na dhidi ya Wapalestina. Nchi hizi zote zimekandamiza harakati za kuwaunga mkono Wapalestina ndani ya nchi zao, kote katika Umoja wa Ulaya na pia nchini Marekani.” Amirhashemi aliongeza kuwa; kwa masikitiko, katika baadhi ya majimbo ya Marekani kuisusia Israel kunaweza kuwa sababu ya kuadhibiwa kisheria.
Alisema: “Hatutaruhusu jambo kama hili litokee nchini Sweden, na tutazuia juhudi zozote za kugeuza hatua kama hizo kuwa sheria ndani ya Umoja wa Ulaya.”
Chanzo: Anadolu Agency.
Maoni yako