Kwa mujibu wa Kitengo cha Habari za Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanazuoni wa Iraq ametuma ujumbe maalum kwa Jumuiya ya Kimataifa ya Qadimun, akiwasilisha rambirambi zake kwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa sababu ya kuuawa kwa baadhi ya makamanda wa muqawama. Sheikh Dkt. Khalid Abdulwahab al‑Mulla, katika ujumbe huu amesema kuwa; uthabiti wa taifa la Iran umeirejeshea dunia maana ya heshima na hadhi, na akasisitiza: “Tupo pamoja nanyi kwa mioyo na sauti zetu katika jihad ya kuelemisha, na ushindi wa mwisho ni ahadi ya Mwenyezi Mungu.”
Matini ya ujumbe huo ni kama ifuatavyo:
Bismillahir Rahmanir Rahim
Taarifa ya rambirambi na mshikamano, iliyotolewa na Jumuiya ya Wanazuoni wa Iraq
Mtukufu Ayatullah Mujtaba Husseini Khamenei (Mwenyezi Mungu amlinde), Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran
Sisi, Jumuiya ya Wanazuoni wa Iraq, tunawasilisha rambirambi zetu za dhati kabisa kwa ajili ya mashahidi ambao Jamhuri ya Kiislamu imewatoa, hususan shahidi mtukufu wa Uislamu, Ayatullah al‑Udhma Sayyid Ali Husseini Khamenei, na makamanda wengine. Tunaamini kwa yakini kwamba leo taifa la Iran na uongozi wake wanapambana kwa niaba ya Umma wote wa Kiislamu dhidi ya nguvu za ubeberu wa kimataifa, ambapo kilele chake ni utawala wa Kizayuni na Marekani.
Jamhuri ya Kiislamu imeuvunja uwezo wa adui wa Kizayuni na kurejesha heshima na utambulisho wa Umma wa Kiislamu.
Tunaona kuwa; ni wajibu kusimama pamoja nanyi, na kutangaza mshikamano huu kwa nguvu zetu zote kupitia "jihad ya kuelemisha" ambayo shahidi wa Uislamu Khamenei aliihimiza. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
«وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِناتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِیاءُ بَعْضٍ یأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَیَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنْکَرِ»
“Na Waumini wanaume na Waumini wanawake wao kwa wao ni marafiki walinzi. Huamrisha mema na hukataza maovu.”
Mtukufu Ayatullah al‑Udhma, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu!
Tunawaandikia huku maneno yakihisi haya mbele ya ukubwa wa kujitolea kwenu, na kalamu ikitetemeka mbele ya uthabiti wenu katika kukabiliana na dhuluma na uvamizi wa Kizayuni na Marekani. Yale mnayovumilia si tu mtihani kwenu, bali ni jaribio la dhamiri ya wanadamu wote.
Tuna yakini kwamba haki haifi maadamu ina watetezi; na hata kama usiku wa dhuluma ukawa mrefu kiasi gani, asubuhi ya haki na ukweli lazima itachomoza. Kusimama kwenu dhidi ya uvamizi wa Wazayuni na Marekani kumeirejeshea dunia maana ya heshima na kuthibitisha kwamba irada ya mataifa ni kubwa kuliko silaha au nguvu ya mabavu.
Kwa hivyo tupo pamoja nanyi kwa mioyo yetu—mioyo inayouma kwa kila tone la damu la mwananchi wa Iran linalomwagika, na kwa kila kilio cha mtoto asiye na hatia. Tupo pamoja nanyi kwa sauti zetu ambazo hazitakoma kusema ukweli, kufichua uongo wa Wazayuni na Marekani, na kudai haki na ukombozi wa Quds kutoka katika na mikono ya wanyanyasaji.
Tupo pamoja nanyi kwa imani kwamba; historia kamwe haiungi mkono wanyanyasaji, na ushindi huja kwa wale wanaovumilia, wenye uaminifu katika ardhi yao na wanaotetea haki yao.
Katika uwanja huu hamko peke yenu; kila muumini wa kweli yuko pamoja nanyi, na kila mtu huru duniani anaona jambo lenu kama lake na maumivu yenu kama yake. Mshikamano wetu nanyi si wa hisani au mapenzi, bali ni wajibu wa kisheria, kibinadamu na kimaadili uliowekwa na dhamiri safi na dini tukufu.
Mtukufu Ayatullah al‑Udhma, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu!
Hadhi yenu itaendelea kuwa juu daima, na hadithi za uthabiti wenu zitakuwa msukumo kwa vizazi vyote vijavyo vinavyojifunza kutoka kwenu namna ya kusimama imara na kurejesha haki. Tutaushuhudia ushindi kwa macho yetu, na tutasali pamoja huko Tehran, Baghdad na Quds; kwa kuwa ushindi unakuja kwa subira, na faraja hupatikana baada ya taabu, na hakika pamoja na uzito kuna wepesi.
Alhamdulillahi Rabbil Aalamin
Sheikh Dkt. Khalid Abdulwahab al‑Mulla
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanazuoni wa Iraq / Baghdad
Maoni yako