Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam Sheikh Ali Al-Khatib, Naibu Rais wa Baraza Kuu la Kiislamu la Kishia nchini Lebanon, katika ujumbe wake wa Ramadhani mwaka huu alisema: Tuko katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, mwezi wa rehema, wema na baraka. Kwa mnasaba huu tunawapongeza wananchi wote wa Lebanon na Waislamu wote, na tunamuomba Mwenyezi Mungu Atuwekee heshima na umoja kwa Umma wa Kiarabu na Kiislamu; umma ambao sasa uko katika hatua hatari zaidi katika historia yake na unahitaji zaidi kuliko wakati mwingine wowote kushikamana na kamba ya Mwenyezi Mungu na kurejea Kwake, ili umoja katika misimamo uwe miongoni mwa dhihirisho muhimu zaidi za uchamungu na sharti la kukubaliwa na Mwenyezi Mungu.
Aliongeza kuwa: Umoja unaosisitizwa, ndugu zangu wapendwa, ni umoja wa kitaifa katika masuala yetu ya ndani, chini ya kivuli cha umoja wa jumla wa Umma katika masuala ya kimkakati na ya hatima. Umoja wa Umma ni amri ya Mwenyezi Mungu, si chaguo la kibinadamu linalotokana na maslahi binafsi au ya kisiasa. Hapa ndipo Umma unapojaribiwa katika kiwango cha uchamungu wake — iwe katika ngazi ya mataifa au serikali — na Ramadhani hupata maana yake katika maisha ya Umma huo, na Mwenyezi Mungu hubariki juhudi zake, uwepo wake na mustakabali wake.
Sheikh Al-Khatib aliendelea kusema kuwa; ingawa hapo zamani Umma wa Kiislamu uligawanyika katika nchi nyingi kutokana na mazingira ya kulazimishwa, na ukakubali hali hiyo kupitia mifumo kama vile Umoja wa Waarabu na Muunganiko wa Waislamu ili kulinda maslahi yake ya kimkakati, baadaye kutokana na njama za nje, nchi zilielekezwa kuweka mbele maslahi ya kitaifa kuliko maslahi ya kimkakati ya Umma, na taasisi hizo zikashindwa kufikia malengo yake.
Alisema kuwa; Magharibi ya kikoloni ilitumia fursa hiyo kuendeleza mpango wake wa kuugawa Umma wa Kiislamu, ikitumia tofauti za kimadhehebu na kikabila kuusukuma Umma hadi ukingoni mwa maangamizi, kiasi kwamba si maslahi ya kitaifa wala ya kimkakati yaliweza kulindwa.
Naibu Rais huyo alisisitiza kuwa; lau si mabaki ya uhai yaliyojitokeza katika kundi la wana wa watu waliokuwa na uelewa na walioshikamana na misingi yao, hali ingefikia janga lisiloweza kurekebishwa. Kundi hilo lilifanikiwa kuutahadharisha Umma juu ya hatari kubwa inayoukabili — hatari inayolenga kuugawa si tu katika umoja wake tu, bali pia kuugawanya katika nchi zenye mielekeo ya kimadhehebu na kikabila na kuzipandikiza chuki baina yao.
Alitaja mifano ya hali kama ilivyotokea hukk Sudan, Libya, Syria na Qatar, pamoja na vitisho dhidi ya Egypt, Turkey na Saudi Arabia, uchochezi kati ya Pakistan na Afghanistan, pamoja na vita vya maangamizi huko Ghaza na Lebanon, na vitisho dhidi ya Iran kwa msaada wa moja kwa moja wa Marekani.
Aliongeza kuwa; sasa baadhi ya nchi zimeanza kutambua kiini cha njama hizi na kuelewa kuwa zote zinakabiliwa na hatari ya pamoja, lakini msimamo uliopo bado haujatosha kukabiliana kikamilifu na hatari hiyo.
Sheikh Al-Khatib alieleza matumaini kuwa; msimamo huo utaelekea katika kuunda muungano wa Kiarabu na Kiislamu ili kukabiliana na hatari hii kubwa na kuweka mwamvuli wa ulinzi kwa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu. Pia aliomba baraka za mwezi huu mtukufu ziteremke juu ya Umma na nchi zao na kuwafanya watambue kikamilifu wajibu wao katika hatua hii nyeti.
Mwisho, alimwomba Mwenyezi Mungu awajaalie watu wake, hasa jamii ya muqawama, rehema Zake; awafariji waliotaabika na awapokee mashahidi kwa rehema. Akasisitiza kuwa, wao kwa subira na kujitoa kwao wanajenga heshima na utukufu wa Umma, na kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni faraja baada ya dhiki, ushindi baada ya subira.
Alikumbusha kuwa Ramadhani ni mwezi wa ushindi wa Badri — ushindi wa kihistoria uliokuwa msingi wa ushindi wote wa Waislamu — na akasema: Leo ninyi ndio Badri wa zama hizi, na ninyi ndio watengenezaji wa ushindi, utukufu na historia.
Maoni yako