Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Ahmad Qabalan, Mufti mashuhuri wa Ja‘fari, kutokana na mnasaba wa kumbukumbu ya kutekwa Imam Sayyid Musa Sadr na wenzake wawili, alitoa ujumbe na kusema: “Walebanoni wapendwa, katika siku ya Imam Sayyid Musa Sadr nasema: Hakuna mtu yeyote aliyeuzima kwa mikono yake miwili moto wa vita vya ndani na ukatili wa Israel, kama alivyofanya Imam Sayyid Musa Sadr.”
Akaongeza kusema: “Dhamira ya Imam Musa Sadr ilikuwa ni Lebanon, mamlaka yake, ushirikiano wake wa Kiislamu na Kikristo, maelewano yake, na jitihada za kutengeneza mfumo wa kisiasa wa kuiondoa Lebanon kutoka katika dimbwi la upendeleo wa kisiasa wa kimadhehebu kwa manufaa ya Lebanon na kwa muunganiko wa dini mbalimbali, pamoja na yote yale ambayo dini zinahimiza kuhusu adabu za ushirikiano na kujitolea kwa maslahi ya kibinadamu, na yale yote yanayohusiana na kujitolea na damu takatifu kwa kadiri ya heshima ya taifa hili na ukubwa wa ushirikiano wake wa kihistoria.”
Sheikh Qabalan akaendelea kusema: “Wakati huu ni kwa ajili ya Lebanon, ujumbe na mshikamano wa kitaifa katika muundo wa Lebanon mmoja, si wa kimadhehebu, mbali na mizozo ya kipuuzi ya kimataifa na ya kikanda. Lebanon bila mamlaka yake, mshikamano wa wananchi wake na kujitolea kwa nguvu za kisiasa kwa ajili ya kulitumikia azimio lake la kitaifa lenye kujumuisha wote, haina thamani yoyote, hili linapatikana tu kwa kulinda nguvu za ndani, si kwa kuziharibu, na kwa kusisitiza juu ya umoja, si kuvunja mshikamano huo.”
Mufti wa Ja‘fari alibainisha: “Katika mwelekeo huu, jeshi na muqawama ni kielelezo cha nguvu za mamlaka ya Lebanon, na haja ya Lebanon kwenye nguvu hizi mbili za kidhati ni dharura muhimu kwa nchi hii, katikati ya mchezo wa kimataifa unaowasha moto katika eneo hili na kuangamiza ramani za taasisi za kisiasa machoni mwetu, Kwa hivyo, macho yetu yameelekezwa kwenye harakati kubwa ya kisiasa itakayoijenga upya Lebanon ndani ya mfumo wa vipaumbele vyake vya kitaifa, mbali na michezo ya kulazimisha, migawanyiko, kudhoofisha na vitisho.”
Alisisitiza kwa kusema: “Katika kumbukumbu ya kutoweka Imam Musa Sadr na wenzake wawili, Mheshimiwa Nabih Berri ndiye mlango wa suluhu na ufunguo wa wokovu wa kitaifa, pamoja na uwepo wa Nabih Berri, ndani hushinda na nje hushindwa, umoja hushinda na mgawanyiko hushindwa, jeshi na muqawama hushinda na Israel na fitna hushindwa, Lebanon hupata mamlaka yake na miradi ya kikoloni hushindwa.”
Sheikh Qabalan alihitimisha kwa kusema: “Imam Sayyid Musa Sadr hakuwa na wasia mkubwa zaidi ya kuihifadhi Lebanon, ushirikiano wake, mamlaka yake na urithi wake wa kihistoria uliojengeka juu ya mshikamano wa mwisho kati ya Ukristo na Uislamu.”
Maoni yako