Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Jawadi Amoli aliyasema hayo katika darsa yake ya fiqhi, akirejea maadhimisho ya siku ya kuzaliwa kwa heri ya Hadhrat Walii wa Zama (a.j). Alisema: Matukio kama vile kuzaliwa kwa Walii wa Zama (a.j) yanapaswa kuadhimishwa kwa njia sahihi. Tunapaswa kuitazama sikukuu hii kama ibada na sehemu ya ibana ya kweli; ingawa furaha, shangwe, bashasha na mashairi katika nyakati hizi ni mambo mazuri na yanapendekezwa, lakini ni lazima pia tufikie maarifa ya kina kuhusu nafasi ya Imam — Imam ambaye tunamtumia salamu katika hali na nyanja zote za maisha:
“Amani iwe juu yako wakati unaposimama, amani iwe juu yako wakati unakaa, amani iwe juu yako wakati unasoma na kufafanua”
Katika muendelezo wa hotuba yake, alisisitiza juu ya nafasi ya misingi ya ‘akili’ katika utamaduni na ustaarabu wa Kiislamu, akisema: Marehemu Kulayni ana utangulizi katika mwanzo wa kitabu chake Al-Kafi ambapo katika mstari wa mwisho wa utangulizi huo anasema kuwa; mhili wa kitamaduni kwa umma wowote ni akili yake: “Kwa kuwa akili ndiyo mhimili ambao mzunguko wote unmeegemea juu yake; kwa akili hoja husimama, thawabu hupatikana na adhabu hutolewa.” Nusu ya mstari huu tu una maana kubwa sana; yaani mhili wa kitamaduni wa Uislamu ni uelewa na ufahamu.
Ayatullah Jawadi Amoli, akirejea nafasi ya usimamizi wa busara katika maendeleo ya kielimu ya hawza, alizungumzia historia ya Hawza ya Najaf, na kusema: Najaf, kabla ya kutambulika kama mji, ilikuwa ni hawza ya elimu. Abu Hamza Thumali, mmoja wa wanafunzi wa Imam Sajjad (a.s), alikuwa kila siku akitoka na kurejea nje ya mji wa Kufa. Baadaye iligundulika kuwa alikuwa akielekea katika kaburi tukufu la Amirul Mu’minin Ali (a.s), ambako alikuwa akifundisha na kusoma pamoja na kundi la wanafunzi wake.
Kuanzia zama za Imam Sajjad (a.s) na wanafunzi wake kama Abu Hamza Thumali, eneo hilo lilikuwa mahali pa elimu na malezi ya wanafunzi maalumu. Katika kipindi cha Imam Sw'adiq (a.s), na baada ya kubainika mahali pa kaburi tukufu la Amirul Mu’minin Ali (a.s), ilidhihirika wazi kwa nini Imam Sajjad (a.s) alikuwa akimuongoza mwanafunzi wake Abu Hamza Thumali kwenda kusoma katika eneo hilo.
Kiongozi huyo wa juu wa kidini, akinukuu kumbukumbu za marehemu Bahrul Ulum, alieleza kuwa; nafasi ya usimamizi wa kifedha na kielimu wa watu kama Sayyid Murtadha na Sayyid Radhiy, ilikuwa na mchango mkubwa sana katika kustawi kwa Hawza ya Najaf. Aliongeza kuwa: Hawza haipaswi kuwa kama kitalu cha kuuza miche, bali inapaswa kuwatambua wanafunzi wenye vipaji na kuwalea kwa uangalifu, ili kutoka ndani ya hawza wapatikane wanazuoni wakubwa kama vile Sahib al-Jawaher na Sheikh Ansari. Hili ndilo walilolifanya Sayyid Murtadha na Sayyid Radhiy, ambao walikuwa mfano wazi wa usimamizi sahihi na utambuzi wa vipaji. Msaada wao ulipelekea kulelewa kwa shakhsia kama Sheikh Tusi, ambaye ni mwandishi wa vitabu viwili kati ya vitabu vinne mashuhuri vya hadithi (Kutub al-Arba‘a). Elimu na aina hii ya uongozi si kila mtu anaweza kuipata.
Marji' huyu wa taqlid, akisisitiza nafasi ya kutosheleza na kujinasibisha kwa Ahlul Bayt wa Ismah na Tohara (a.s), alibainisha kuwa: Sio elimu zote hupatikana kwa kujifunza, kusoma na kufanya utafiti. Muujiza, Uimamu na Ismah havina njia ya kufikiri ya kawaida, na hakuna mtu anayeweza kuvifikia kwa masomo ya kawaida. Hivyo, elimu aliyonayo Imam haipatikani kwa kusoma na kujifunza, bali ni elimu ya kimungu, ukweli wa Mwenyezi Mungu ulio juu na nje ya njia za kawaida za maarifa.
Mwishoni, Ayatullah Jawadi Amoli, huku akigusia wajibu wa wanazuoni na viongozi wa dini sambamba na uandishi wa vitabu na kazi za kielimu, alisisitiza umuhimu wa mwenendo wao wa vitendo, na akaeleza matumaini yake kwamba jamii, viongozi na wananchi kwa ujumla waendelee kuwa chini ya dua na uangalizi wa Walii wa Zama (a.j).
Maoni yako