Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Naim Qassem, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, amechaguliwa kuwa Msaidizi wa Mahdi wa Mwaka wa Haram Tukufu ya Msikiti wa Jamkaran kutokana na mchango wake mkubwa na wa kipekee katika kueneza fikra ya Mahdawiyya (imani ya Imam Mahdi) pamoja na kusimama imara katika njia ya Muqawama.
Uteuzi huu umefanyika kama ishara ya kuthamini juhudi zake endelevu katika kuwatetea wanyonge, kupambana na mikondo ya kibabe na kibeberu, pamoja na kuimarisha safu ya haki.
Hafla ya kumtangaza Msaidizi wa Mahdi wa Mwaka wa Jamkaran hufanyika kwa lengo la kuwaheshimu watu mashuhuri wanaofanya kazi katika njia ya kufufua fikra ya Mahdawiyya na utamaduni wa kusubiri (Intidhār). Katika hafla hizi, watu wenye mchango mkubwa katika kueneza utamaduni wa kusubiri na kuandaa mazingira ya kudhihiri kwa Imam Mahdi (a.j) hutunukiwa heshima maalumu.
Katika miaka ya hivi karibuni, shakhsia kadhaa mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu wametangazwa kuwa wasaidizi wa Mahdi, miongoni mwao wakiwemo: Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah, Sheikh Ibrahim Zakzaky, Jenerali Shahidi Haj Qassim Soleimani, Shahidi Abu Mahdi al-Muhandis, Ayatullah Sheikh Isa Qassim, Jenerali Ali Fazli, pamoja na Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Hashim al-Haydari.
Kulazimiana na Uongozi wa Walii Fiqihi ni Miongoni mwa Misingi ya Subira ya Kweli
Katika hotuba yake ya video aliyotoa kwenye hafla ya sherehe ya usiku wa Nusu ya Shaaban na pia katika hafla ya kumtunuku “Msaidizi wa Mahdi wa Mwaka” wa Haram Tukufu ya Msikiti wa Jamkaran, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Naim Qassem, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, alisisitiza nafasi ya Mahdawiyya katika kuwaokoa wanadamu, akisema: Imam Mahdi (a.j) ni tumaini la wanyonge wote duniani na ni ahadi ya hakika ya Mwenyezi Mungu ya kusimamisha uadilifu katika ardhi yote.
Akinukuu Aya za Qur’ani Tukufu na hadithi za Mtume (s.a.w), alieleza kuwa: Wanadamu wa leo wanamhitaji Imam Mahdi (a.j) zaidi kuliko wakati mwingine wowote, kwani dunia imejaa dhulma, ujeuri na uistikbari; na njia pekee ya wokovu ni kutimia kwa ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kudhihiri kwa Muokozi.
Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, akisisitiza kuwa Umma wa Kiislamu unapaswa kuwa tayari kabla ya kudhihiri, aliongeza kuwa: Waumini wanapaswa kuwa imara, kujitolea na kuwa wapiganaji wa jihadi, na viongozi wanapaswa kuwa wasafi, jasiri na wenye kujitoa mhanga uwanjani; na hii ndiyo njia ambayo leo, kwa fadhila za Mwenyezi Mungu, inaendelea kutimia ndani ya Umma wa Kiislamu.
Sheikh Naim Qassem, akirejea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, aliyaelezea kama mafanikio ya kipekee katika njia ya kusubiri kudhihiri, na akasema: Kuanzishwa kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran chini ya uongozi wa Imam Khomeini (r.a) katika kilele cha dhulma ya kimataifa, ilikuwa ni hatua kubwa katika kuandaa mazingira ya kudhihiri. Leo hii, njia hii inaendelea kwa nguvu chini ya uongozi wa busara wa Ayatullah al-Udhma Imam Khamenei (Mola amuendeleze).
Alisisitiza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni dola ya Imam wa Zama, na bendera ya Mapinduzi haya hatimaye itakabidhiwa mikononi mwa Imam Mahdi (a.j). Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, akizungumzia kuundwa kwa safu ya Muqawama nchini Lebanon, Palestina na maeneo mengine ya kanda, alisema: Muqawama ulizaliwa chini ya uongozi wa Imam Khomeini (r.a), na leo kila mpiganaji wa Muqawama hutamka jina la Imam Mahdi (a.j) kwa ulimi wake na hujiona kuwa askari wa Imam huyo. Akikumbusha nafasi ya mashahidi na makamanda wa Muqawama, Sheikh Naim Qassem alisema: Mashahidi wa Muqawama, kwa kumwaga damu zao, wamethibitisha uaminifu wao kwa Imam wa Zama (a.j), na damu yao ndiyo inayofungua njia kwa Umma kujiunga na msafara wa kudhihiri.
Sheikh Naim Qassem alisisitiza kuwa njia ya Imam Mahdi (a.j) ni njia ya Wilayah, na akaongeza kuwa: Kulazimiana na uongozi wa Walii Fiqihi, kusimama dhidi ya madhalimu, Marekani na utawala wa Kizayuni, pamoja na kujitolea katika njia ya Muqawama, ni miongoni mwa mifano muhimu zaidi ya kusubiri kwa kweli na kuharakisha faraja (faraj).
Akigusia nafasi ya Msikiti wa Jamkaran, alieleza kuwa; Haram hii Tukufu ni miongoni mwa maeneo yaliyo karibu zaidi na uwepo wa kiroho wa Imam wa Zama (a.j), na akawahimiza waumini kudumisha kuhudhuria, kuomba dua na kushikamana na eneo hilo takatifu.
Mwisho, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, kwa kutoa shukrani kwa viongozi wa Haram Tukufu ya Msikiti wa Jamkaran kwa kumtangaza kuwa “Msaidizi wa Mahdi wa Mwaka”, aliomba dua akisema: Mwenyezi Mungu Mtukufu aharakishe faraja ya Walii Wake, na atujalie kuwa miongoni mwa wasaidizi, wafuasi na mashahidi katika safu ya Imam Mahdi (a.j).
Maoni yako