Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Asadullah Bahto, Mwenyekiti wa Baraza la Mshikamano wa Kitaifa la Jimbo la Sindh na mbunge wa zamani wa Pakistan, katika hotuba yake akigusia kuendelea uvamizi wa utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza, alitaja siasa ya Israeli ya kutumia njaa kama silaha dhidi ya watu wa Palestina kuwa ni kitendo cha kikatili na kijinai.
Ameongeza: Wakati ambapo katika nchi za Magharibi kunazungumzwa sana kuhusu haki za wanyama kama mbwa na paka, madola yanayodai haki za binadamu kama Marekani na Ulaya yamechagua kunyamaza kwa aibu mbele ya mauaji ya halaiki ya wazi ya taifa la Palestina.
Asadullah Bahto, akibainisha kwamba Palestina ni ardhi ya Mitume, alisema: uvamizi wa ardhi hii na kutekelezwa kwa ndoto ya kufikirika ya Israeli Kubwa katu haitawezekana, pia makubaliano yajulikanayo kama Abrahamu si chochote ila ni udanganyifu na mtego wa adui kwa ajili ya umma wa Kiislamu, na Waislamu wanapaswa wawe na tahadhari juu yake.
Akaendelea kubainisha: kujitolea na mapambano ya viongozi wa Kipalestina kama Yahya Sinwar na Ismail Haniyeh, pamoja na kujitoa muhanga kwa maelfu ya watoto, wanawake na wanaume huko Ghaza, kumeingiza roho ya jihad na mapambano katika kizazi kipya cha Waislamu, na miale yake leo inaangaza katika nyoyo za watu wote huru duniani.
Mwenyekiti wa Baraza la Mshikamano wa Kitaifa la Sindh akiashiria mapambano ya miezi 22 ya watu wa Ghaza tangia kuanza kwa uvamizi wa Israeli mnamo Oktoba 2023, alisisitiza: pamoja na kuuawa kishahidi kwa makumi ya maelfu ya Wapalestina na uharibifu mkubwa, msimamo imara wa taifa la Ghaza umeondosha kiburi cha utawala wa Kizayuni na mandhari ya mapambano yao yamekuwa ni kumbu kumbu ya ushujaa wa masahaba wa Mtume wa Uislamu katika vita vya Badr. Hadi sasa zaidi ya watu 62,895 wameuawa kishahidi na takriban 158,895 wamejeruhiwa.
Asadullah Bahto, akilaani vitendo vya utawala wa Kizayuni vya kuweka vikwazo kwenye kupeleka misaada ya kibinadamu, alisema: leo Umoja wa Mataifa pia rasmi umeitaja Ghaza kama eneo lililokumbwa na njaa; zaidi ya nusu milioni ya Wapalestina wanakabiliwa na njaa na mgogoro mkali wa chakula, na Israeli kwa makusudi inazuia kuingia kwa bidhaa za msingi za chakula kama nyama, samaki, maziwa, mboga na matunda katika eneo hili.
Akaendelea katika hotuba yake akigusia maandamano na upinzani mkubwa kote duniani dhidi ya jinai za Wazayuni na vilevile kulaaniwa kwa utawala huu kwa kutenda jinai za kivita katika mahakama za kimataifa, akabainisha: pamoja na kulaaniwa kote huku, Israeli bado inasisitiza tamaa zake na inafuata mpango wake wa uovu wa kuitawala kikamilifu Ghaza na kutekeleza mradi hatari wa Israeli Kubwa; jambo ambalo si tu usalama wa Mashariki ya Kati, bali pia amani na uthabiti wa dunia nzima vimekabiliwa na tishio kubwa.
Mwenyekiti wa Baraza la Mshikamano wa Kitaifa la Sindh mwishoni alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, hususan nchi za Kiislamu, kwamba zitoke zaidi ya kubakia kwenye misimamo na kutoa taarifa za kulaani, na kwa kuchukua mkakati wa kivitendo na wenye taathira, ziwasaidie watu wa Palestina na pia ziweke wazi njia ya ukombozi wa Quds Tukufu.
Maoni yako