Shirika la Habari la Hawza - Katika utafiti wa faida za Imam aliye ghaiba, tulizungumzia kuhusiana na athari za uwepo wa Hadhrat huyo na tukafafanua kwamba kudumu kwa ulimwengu na kuendelea kwa maisha ya viumbe vyote kunategemea uwepo wa huyo mtukufu, na katika sehem hii, mazungumzo yetu ni kuhusiana na mapenzi yasiyo na kikomo ya Imam aliye ghaiba, ambayo imejidhihirisha kwa namna mbali mbali ili iwe wazi kwa wote kwamba ni Imam mwenye wema na huruma, licha ya kuwa ghaiba na kufichika kwake, miale ya mapenzi yake imetanda kila mahali na kulingana na nafasi na uwezo wa kila mmoja, imemfunika kila mtu na fadhila na ukarimu wake ni mithili ya chemchemi yenye msukumo mkali, yenye mfululizo wa kudumu na endelevu.
Miongoni mwa sifa muhimu na bora zaidi za muumini ni mshikamano na kushirikiana katika huzuni na shida za ndugu zake wa kidini, waumini katika jamii ya Kiislamu ni kama kiwiliwili kimoja, ambapo maumivu na huzuni ya mmoja huwasababishia wengine matatizo, na raha na furaha ya mmoja huleta furaha kwa wengine, kwa sababu wao, kwa bayana ya Qur’ani, ni ndugu.
Katika riwaya nyingi, Maimamu Maasumina (as) wameeleza hisia zao katika kushirikiana kwenye matatizo ya mashia wao, na hisia hizi nzuri huwa sababu ya utulivu na faraja kwenye nyoyo za wapenzi wao, na ni nguvu ya moyo inayowapa moyo wa ujasiri katika changamoto za maisha, na huimarisha uvumilivu na ustahamilivu wao.
Imam Ridha (as) anasema:
«مَا مِنْ أَحَدٍ مِنْ شِیعَتِنَا یمْرَضُ إِلَّا مَرِضْنَا لِمَرَضِهِ وَ لَا اغْتَمَّ إِلَّا اغْتَمَمْنَا لِغَمِّهِ وَ لَا یفْرَحُ إِلَّا فَرِحْنَا لِفَرَحِه»
“Hakuna yeyote kati ya mashia wetu anaugua isipokuwa nasi pia tunaumwa kutokana na kuugua kwake, wala hahuzuniki isipokuwa nasi pia tunahuzunika kwa huzuni yake, wala hafurahii isipokuwa nasi pia tunafurahi kwa furaha yake.”
(Bihar al-Anwar, j. 65, uk. 167)
Kwa hiyo, Imam kwa sababu ya wingi wa huruma na mapenzi aliyo nayo kwa wafuasi wake, ana mafungamano makubwa zaidi nao, na kutokana na mapenzi na urafiki huu, hushiriki katika matatizo na huzuni zao; kama vile mama ambaye, kutokana na mapenzi makubwa na mafungamano yake na mwanawe, huugua anapougua, na hufurahi kwa afya na furaha yake, kwa sababu mwana ni mpendwa na mpenzi kwake kama roho tamu.
Na pia Imam Sadiq (as) anasema:
«وَ اللَّهِ إِنِّی أَرْحَمُ بِکُمْ مِنْ أَنْفُسِکُم»
“Naapa kwa Mwenyezi Mungu, mimi ni mwenye huruma kwenu zaidi kuliko nafsi zenu wenyewe".
(Basā’ir al-Darajāt, uk. 265)
Hitimisho ni kwamba aina ya mapenzi ya Imam ni tofauti na mapenzi mengine yeyote, ni mapenzi yaliyo safi, yasiyo na masimbulizi, yasiyo na kikomo; mapenzi ambayo si kwa maneno bali yamejikita moyoni na katika undani wa nafsi yake, na kwa sababu hiyo, kwa nafsi nzima, mwili na roho, ana uhusiano thabiti na mashia wake.
Miongoni mwa mifano ya wazi ya mapenzi haya ya kimungu katika nafsi tukufu ya Imam wa zama (as) imesimuliwa kwa maneno yake hivi:
«إِنَّهُ أُنْهِی إِلَی ارْتِیابُ جَمَاعَه مِنْکُمْ فِی الدِّینِ وَ مَا دَخَلَهُمْ مِنَ الشَّکِّ وَ الْحَیرَه فِی وُلَاه أَمْرِهِمْ فَغَمَّنَا ذَلِکَ لَکُمْ لَا لَنَا وَ سَأَوْنَا فِیکُمْ لَا فِینَا لِأَنَّ اللَّهَ مَعَنَا فَلَا فَاقَه بِنَا إِلَی غَیرِه»
“Kwangu kumeripotiwa kwamba kundi miongoni mwenu limeingia katika shaka kuhusu dini, na shaka na kuchanganyikiwa kumeingia mioyoni mwao kuhusu viongozi wao wa mambo, hili lilituletea huzuni, lakini kwa ajili yenu na siyo kwa ajili yetu, na likawa ni sababu ya majonzi yetu kuhusu ninyi na siyo kuhusu sisi, kwa sababu Mwenyezi Mungu yupo pamoja nasi, na kwa uwepo wake, hatuna haja ya mwingine yeyote.”
(Bihar al-Anwar, j. 53, uk. 178)
Utafiti huu unaendelea…
Imenukuliwa kutoka kwenye Kitabu “Nagini Āfarinish” huku ikifanyiwa mabadiliko kiasi.
Maoni yako