Jumanne 27 Mei 2025 - 14:18
Tarjama ya Kwanza ya Qur'ani Tukufu kwa Lugha ya Dhatki nchini Pakistan Imetamatika

Hawza/ Bwana Haji Muhammad Sidiq Rahimun, mkazi wa kijiji cha Radhkhar kilicho karibu na eneo la Dahili, hivi karibuni amekamilisha tarjama ya Qur'ani Tukufu kwa lugha ya Dhatki. Dhatki ni lugha ya asili inayozungumzwa na watu wa eneo la mpakani kati ya Pakistan na India.

Kwa mujibu wa ripoti ya idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Bwana Haji Muhammad Sidiq Rahimun, mkazi wa kijiji cha Radhkhar kilicho karibu na eneo la Dahili katika jangwa la Tharparkar, amekamilisha tarjama ya Qur'ani Tukufu kwa lugha ya Dhatki. Dhatki huzungumzwa katika sehemu mbalimbali za jangwa la Thar, ikiwemo maeneo ya Tharparkar, Amarkot ABC, na pia katika baadhi ya maeneo ya mpakani mwa India.
Javed Jafar Rahimun, ndugu wa karibu wa mwandishi huyo, katika mazungumzo na mwandishi wa habari alisema: “Haji Muhammad, kutoakana na  juhudi za usiku na mchana kwa kipindi cha miaka miwili na nusu, ameweza kutarjumu nakala hii yenye thamani ya Qur'ani Tukufu kwa lugha ya Dhatki.”

Javed aliongeza kwa kusema: “Haji Muhammad alikuwa mfanyakazi katika Wizara ya Afya ya Serikali ya Sindh. Baada ya kustaafu kazi yake serikalini, alifuata shauku yake na akaendelea na juhudi hiyo. Baada ya kutarjumu Qur'ani Tukufu, alikuwa na hofu kwamba huenda kukawa na kasoro fulani ndani yake. Hivyo basi, alituma nakala kadhaa kwa wanazuoni wakuu wa Hawza ili waweze kuipitia. Tarjama hiyo ilipokelewa kwa pongezi na sifa kutoka kwa wote waliopokea, na hivyo mtarjumu huyo akapata utulivu wa moyo kwamba kazi hii ameitekeleza ipasavyo.”

Kwa mujibu wa wanaharakati na waandishi wa eneo hilo, mafanikio haya makubwa yatachangia kwa kiwango kikubwa kuongeza usomaji na tilawa ya Qur'ani miongoni mwa watu wanaozungumza lugha ya Dhatki.
“Hii ni hatua nzuri sana, kwani sasa tunaweza kufahamu maana ya Qur'ani kwa lugha yetu mama.”

Wakazi wa eneo hilo wamemtaja Haji Muhammad Rahimun kama mtu mashuhuri wa kielimu na kiroho katika jamii yao.
“Yeye ni mtu mkubwa ambaye amethibitisha uaminifu wake kwa watu wanaoishi pande zote mbili za mpaka. Tunawaomba viongozi wahusika wamsaidie katika uchapishaji wa tarjama hii, ili kurahisisha upatikanaji wake kwa watu wa eneo hili na wote wanaozungumza lugha ya Dhatki na wanaopenda Qur'ani."

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha