Shirika la Habari la Hawza - Baada ya ulimwengu wa mwanadamu kupitia kipindi kirefu sana cha utawala wa dhulma na uonevu, dunia, kwa kudhihiri kwa hoja wa mwisho wa Mola Mlezi, itasogea kuelekea kwenye utawala wenye wema na mema, na serikali itakuwa mikononi mwa watawala wema. Na hii ni ahadi ya Mwenyezi Mungu isiyo na shaka.
Utawala wa watu wema ambao utaanza kwa uongozi wa Imam Mahdi (a.s), utaendelea hadi mwisho wa dunia, na zama za dhulma na madhalimu hazitapatikana tena.
Mwenyezi Mungu Mtukufu amembashiria Mtume wa Uislamu (s.a.w) kuhusu utawala wa mwisho wa kiongozi huyo wa mwisho asiyekosea, amesema:
«لأُدِیمَنَّ مُلْکَهُ وَ لَأُدَاوِلَنَّ الْأَیَّامَ بَیْنَ أَوْلِیَائِی إِلَی یَوْمِ الْقِیَامَةِ.»
Hakika nitauendeleza utawala wake na nitazirudisha siku na zama mikononi mwa marafiki na wapenzi wangu hadi Siku ya Kiyama. (Kamaal ad-Din, Juzuu ya 1, uk. 256)
Kwa hivyo, mfumo wa haki na uadilifu ambao Imam Mahdi (a.s) atauanzisha utakuwa ni serikali ambayo baada yake hakutakuwa na serikali nyingine yoyote, na kwa hakika, historia mpya ya maisha ya mwanadamu itaanza, historia ambayo yote itakuwa chini ya utawala wa Mwenyezi Mungu.
Imam Baqir (a.s) anasema:
«دوْلَتُنَا آخِرُ الدُّوَلِ وَ لَنْ یَبْقَ أَهْلُ بَیْتٍ لَهُمْ دَوْلَةٌ إِلَّا مُلِّکُوا قَبْلَنَا لِئَلَّا یَقُولُوا إِذَا رَأَوْا سِیرَتَنَا إِذَا مُلِّکْنَا سِرْنَا مِثْلَ سِیرَةِ هَؤُلَاءِ.»
Dola yetu ndiyo serikali ya mwisho, na hakuna familia yoyote yenye utawala itakayobaki ila kwamba itapewa utawala kabla yetu, ili pale watakapoona mwenendo wetu wa uongozi, wasiseme: ‘Kama sisi tungepewa utawala, tungeongoza kama walivyoongoza hawa.’ (al-Ghaybah, Shaykh Tusi, uk. 473)
Hivyo basi, muda wa kuendelea kwa mfumo wa uongozi wa Mwenyezi Mungu baada ya kudhihiri Imam Mahdi (a.s) ni jambo lililo tofauti na muda wa uhai wa Imam Mahdi (a.s) mwenyewe. Kwa mujibu wa riwaya, Imam Mahdi (a.s) atatawala katika kipindi kilichosalia cha maisha yake, na hatimaye atafumba macho na kuaga dunia.
Hakuna shaka kuwa muda wa utawala wa Imam Mahdi (a.s) utakuwa ni wa kutosha kiasi kwamba mabadiliko ya kimataifa na kuimarika kwa haki na uadilifu katika maeneo yote ya dunia yawezekane. Hata hivyo, kubaini kama lengo hili linaweza kufikiwa ndani ya muda wa miaka michache au hapana, jambo hili haliwezi kukadiriwa kwa maoni binafsi. Badala yake, lazima kurejea kwenye riwaya za Maimamu (a.s). Bila shaka, kwa kuzingatia uwezo wa kiongozi huyo wa Mwenyezi Mungu, msaada na nusra ya ghaibu kwa Imam na wafuasi wake waaminifu, pamoja na maandalizi ya dunia kwa ajili ya kukubali utawala wa thamani na uzuri katika zama za kudhihiri, inawezekana kwamba risala ya Mahdi al-Muntadhir (a.s) ikakamilika katika muda mfupi kidogo.
Riwaya zinazotaja muda wa utawala wa Imam Mahdi (a.s) zinatofautiana sana. Baadhi ya riwaya zimetaja kuwa muda wa utawala huo utakuwa miaka 5, baadhi zinasema miaka 7, zingine zikitaja miaka 8, 9 na 10. Kuna riwaya chache pia zinazosema muda huo ni miaka 19 na miezi kadhaa, miaka 40, na hata miaka 309.
Kupata muda wa kweli wa utawala wa Imam Mahdi (a.s) miongoni mwa riwaya hizi ni jambo gumu, lakini baadhi ya wanazuoni wa Kishia, kwa kuzingatia wingi na umaarufu wa riwaya za miaka 7, wamelichukua hili kama msimamo wao. Na baadhi yao, kwa mujibu wa baadhi ya riwaya, wamesema kwamba muda wa utawala wa Imam Mahdi (a.s) ni miaka 7, lakini kila mwaka kati ya miaka hiyo 7 utakuwa sawa na miaka 10 ya miaka yetu ya sasa.
Utafiti huu unaendelea...
Imenukuliwa kutoka kitabu “Negin-e Afarinish” (Lulu ya Uumbaji) huku ikifanyiwa marekebisho kidogo
Maoni yako