Shirika la Habari la Hawza | Harakati na mapinduzi ya kimataifa ya Imamu Mahdi (a.s.) ina alama maalum. Kujua alama hizi kuna athari muhimu. Kwa kuwa ishara hizi ni bishara ya faraji ya Mahdi kizazi Mtume (s.a.w), basi kutokea kwa kila mojawapo ya ishara hizi huangazia zaidi nuru ya matumaini katika nyoyo za wanaosubiri, na kwa wapinzani na waasi, huwa ni njia yenye onyo na ukumbusho ili waache uovu na upotovu, na vilevile huwaandaa wanaosubiri kwa ajili ya kuelekea kujitokeza huku na kupata ustahiki wa kuwa pamoja na Ma’sum (a.s.).
Mbali na hayo, kujua matukio yajayo kunaweza kutusaidia kupanga mikakati bora ya kukabiliana nayo. Vivyo hivyo, ishara hizi ni kigezo bora cha kuwabaini wanaodai kwa uwongo kuwa wao ni Mahdi; kwani endapo mtu atadai kuwa ni Mahdi ilhali harakati yake haikuambatana na alama hizi, basi kwa urahisi tunaweza kuutambua uwongo wake.
Katika riwaya za Ma’sumina (a.s.), alama nyingi za kujitokeza kwa Imamu Mahdi (a.s.) zimetajwa, baadhi yake zikiwa ni za kawaida na za kimaumbile, na nyingine zikiwa za kimiujiza.
Miongoni mwa alama hizo, tutataja kwa muhtasari zile ambazo zimeelezwa kwa uwazi zaidi katika vyanzo vya kuaminika, kisha mwishoni tutazitaja kwa kifupi baadhi ya alama nyingine.
Imamu Swadiq (a.s.) anasema katika hadithi:
«خَمْسٌ قَبْلَ قِیَامِ اَلْقَائِمِ عَلَیْهِ السَّلاَمُ: اَلْیَمَانِیُّ، وَ اَلسُّفْیَانِیُّ، وَ اَلْمُنَادِی یُنَادِی مِنَ اَلسَّمَاءِ، وَ خَسْفٌ بِالْبَیْدَاءِ، وَ قَتْلُ اَلنَّفْسِ اَلزَّکِیَّةِ.»
Kabla ya kusimama kwa al-Qaa’im (Imamu Mahdi), kuna alama tano: al-Yamani, as-Sufyani, mwito kutoka mbinguni, kudidimizwa ardhi ya Baydaa, na kuuawa kwa Nafsi isiyo na makosa. (Kamaalud-Din, j. 2, uk. 649)
Kwa mujibu wa hadithi hii, sasa tutaeleza kwa muhtasari alama hizi tano ambazo zimerudiwa katika riwaya mbalimbali, japokuwa maelezo yote ya kina kuhusu matukio haya bado hayako wazi kwetu.
A. Kutokea kwa Sufyani
Kutokea kwa Sufyani ni miongoni mwa alama zilizotajwa mara nyingi katika riwaya. Ameelezwa kuwa ni mtu kutoka katika ukoo wa Abu Sufyan ambaye atainuka kutoka ardhi ya Shaam (Syria) muda mfupi kabla ya kujitokeza kwa Mahdi (a.s.). Yeye ni mhalifu ambaye hana huruma wala aibu katika kuua na kufanya jinai, na hutenda maovu kwa ukatili dhidi ya maadui zake.
Kwa mujibu wa baadhi ya riwaya, muda wa kuanzia kuanza kwa harakati za Sufyani hadi kuuawa kwake ni miezi kumi na mitano.
B. Kudidimizwa kwa ardhi ya Baydaa
"Khusuf" maana yake ni kumezwa na ardhi, na "Baydaa" ni eneo kati ya Makka na Madina.
Maana ya kumezwa kwa ardhi ya Baydaa ni kwamba Sufyani atapeleka jeshi kwenda kukabiliana na Imamu Mahdi (a.s.) huko Makka. Lakini jeshi hilo litakapofika katika eneo la Baydaa, litaangamia kwa njia ya kimiujiza, likididimizwa ardhini.
C. Kutokea kwa Yamani
Kuinuka kwa kiongozi kutoka Yemen ni alama nyingine ambayo itatokea muda mfupi kabla ya kujitokeza kwa Imamu. Mtu huyu ni mwema, mwenye imani, na atainuka dhidi ya uovu na upotovu kwa nguvu zote, akipambana na uharibifu kwa juhudi kubwa. Hata hivyo, maelezo ya kina kuhusu harakati zake hayako wazi kwetu.
D. Sauti ya Mbinguni
Miongoni mwa alama nyingine kabla ya kujitokeza ni sauti ya mbinguni. Kwa mujibu wa baadhi ya riwaya, hii ni sauti ya Jibril (a.s.) ambayo itasikika katika mwezi wa Ramadhani. Kwa kuwa harakati ya Imamu Mahdi (a.s.) ni mapinduzi ya kimataifa na watu wote wanalisubiri, basi mojawapo ya njia ya kuwatangazia watu duniani ni sauti hii ya kimiujiza kutoka mbinguni.
Sauti hii itakuwa ni bishara kwa waumini na onyo kwa waovu, ili waache maovu yao na waingie katika safu ya wasaidizi wa mkombozi ulimwengun
E. kuuawa kwa Nafsi isiyo na makosa
"Nafs Zakiya" maana yake ni mtu aliyekomaa na kutakasika, au mtu asiye na hatia ambaye hajafanya kosa. Kuuawa kwa Nafsi isiyo na makosa kunamaanisha kuwa muda mfupi kabla ya harakati ya Imamu Mahdi (a.s.), mtu mashuhuri au mwenye usafi wa moyo atauawa na mikono ya wapinzani wa Imamu.
Kwa mujibu wa baadhi ya riwaya, tukio hili litafanyika usiku wa kumi na tano kabla ya kuanza kwa harakati za Imamu Mahdi (a.s.).
Alama Nyingine
Riwaya zimeonesha ishara nyingine nyingi pia, baadhi ya hizo ni kama:
Kutokea kwa Dajjaal/ kiumbe mdanganyifu na muovu atakayewapotosha watu wengi.
Kupatwa kwa jua na mwezi katika mwezi wa Ramadhani.
Kuibuka kwa fitina mbalimbali.
Kuingia kwa mtu kutoka Khurasan katika uwanja wa harakati...
Inapaswa kueleweka kuwa maelezo ya kina na uchambuzi wa alama hizi vimeandikwa kwa urefu katika vitabu maalum.
Utafiti huu unaendelea...
Imenukuliwa kutoka katika kitabu kiitwacho “Negin-e Āfarinish” huku ikifanyiwa marekebisho kiasi
Maoni yako