Shirika la Habari la Hawza, | Katika maneno ya wanao mzungumzia Ma’sumi (as) kuhusu manufaa ya Imamu aliyepo katika ghaiba, kwa tashbihi iliyojaa uzuri, Imam Mahdi (aj) katika kipindi cha ghaiba amefananishwa na jua lililojificha nyuma ya mawingu. Bila shaka tashbihi hii ni ya hekima, na kwa hivyo wanazuoni wa Kishia wametoa nukta zenye thamani kuhusiana na tashbihi hii, ambazo baadhi yake ni hizi zifuatazo:
-
Jua ndilo mhimili na kituo cha mfumo wake. Vivyo hivyo, Imam wa Zama (as) ndiye mhimili na msingi wa mfumo wa maisha ya wanadamu.
-
Jua lina manufaa mengi sana katika mfumo wa uumbaji, ambapo moja tu kati ya hayo ni kutoa mwangaza. Vilevile Imam wa Zama (as) ana manufaa mengi katika mfumo wa uumbaji, ambapo ni sehemu ndogo tu ya hayo ndiyo inayotegemea kudhihiri kwake.
-
Wingu hufunika uso wa jua kwa walioko ardhini, lakini halizuii ardhi kupata mwangaza. Vivyo hivyo, pazia la ghaiba linamnyima mwanadamu tu kuona moja kwa moja, lakini kamwe halizuii nuru yake kuwafikia watu.
-
Kujaa kwa mawingu ni katika athari za dunia na waliomo ardhini, si jua lenyewe. Vivyo hivyo, ghaiba ni matokeo ya mienendo ya watu.
-
Wingu ni kizuizi tu kwa wale walio chini yake. Mtu akivuka mvuto wa ardhi na kupanda juu ya mawingu, tena hayawezi kuwa kizuizi kwake. Hali kadhalika, katika ghaiba, mtu akishinda mvuto wa kidunia na kufikia upeo wa hali ya kiroho anayostahili, anaweza kuvuka pazia la ghaiba na kupata bahati ya kuona jua hilo lililojificha.
-
Katika kunufaika na jua, hakuna tofauti kati ya wale wanaoliamini na wale wanaolikataa. Vilevile, katika kunufaika na manufaa ya kimaumbile ya Imamu, hakuna tofauti kati ya wanaomkubali Imamu na wanaomkataa.
-
Ni watu tu wenye maarifa kamili kuhusu manufaa ya jua ndio wanaoitazamia kwa kweli kuondoka kwa mawingu. Hali kadhalika, katika kipindi cha ghaiba, maarifa ya Imamu humfanya mtu awe na matarajio halisi ya kudhihiri kwake.
na kadhalika...
Kwa hiyo, hakuna shaka kwamba kiwango cha kunufaika kwa viumbe kutokana na jua linalong’aa huongezeka na kuwa kamili zaidi wakati hakuna kizuizi kilicho mbele yake. Lakini hili halimaanishi kwamba kuwepo kwa pazia juu ya jua kunaondoa kabisa au zaidi ya nusu ya manufaa yake; bali pazia hilo linaondoa au kupunguza baadhi ya manufaa tu.
Kuwepo dhahiri Imamu pindi atakapo dhihiri na kuwepo kwao kwa wazi, kunamaanisha kuwa manufaa yote ya Imamu yanaweza kuwafikia watu. Hata hivyo, ikiwa kuna kizuizi kinachozuia neema kamili ya Imamu kuwafikia wengine, hiyo haimaanishi kwamba kuwepo kwake hakufai. Kuwepo kwa Imamu nyuma ya pazia la ghaiba kuna manufaa sawa na kuwepo kwake akiwa ndani ya magereza ya watawala madhalimu. Ingawa kuna tofauti nyingi kati ya gereza la ghaiba na gereza la watawala wa kiimla, lakini kila moja ni aina ya kizuizi kinachozuia neema kamili ya Imamu kuwafikia ulimwengu wa kuwepo na wanadamu.
Kwa kifupi, suala la ghaiba halipingani na falsafa ya ulazima wa kuwepo kwa Imamu Maasumu (as); kwani Imamu Maasumu, hata akiwa ghaibuni, bado yupo, na manufaa yake yanafika kwa wengine. Ni sehemu tu ya manufaa yake ndiyo isiyowafikia watu kutokana na uzembe wao wenyewe wakati wa ghaiba, na ni watu wenyewe wanaopaswa kujiandaa ipasavyo na kuandaa mazingira kwa ajili ya kudhihiri kwa Mtukufu huyo.
Utafiti huu unaendelea...
Imenukuliwa kutoka katika kitabu “Farhang-Name Mahdawiyyat” huku ikifanyiwa marekebisho kiasi
Maoni yako