Alhamisi 8 Mei 2025 - 12:49
Jukumu kuu zaidi la hawza ni "balāgh mubīn" (ufikishaji ulio bayana) na kuandaa mazingira ya ustaarabu mpya wa Kiislamu / Utekelezaji wa hawza yenye kujenga ustaarabu kupitia kulea “mujahid wa kitamaduni aliyejitakashasha kimaadili” na “mbunifu”

Ayatollah Ali Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika ujumbe wake kwa kongamano la “maadhimisho ya miaka mia moja tangu kuasisiwa upya kwa Hawza ya Kielimu ya Qum,” pamoja na kubainisha vipengele na majukumu mbalimbali ya hawza, alielezea mahitaji ya kutekelezwa kwa ajili ya kufanikisha “hawza inayoongoza na iliyo juu ya nyingine,” ambayo inakuwa na ubunifu, yenye ustawi, ya kisasa, inayojibu changamoto mpya, yenye maadili mema, roho ya kimaendeleo na jihadi, utambulisho wa kimapinduzi, na yenye uwezo wa kubuni mifumo ya uendeshaji jamii. Alisisitiza kuwa: jukumu kuu zaidi la hawza ni "ufikishaji ulio bayana", ambao miongoni mwa vielelezo bora vya dhati yake ni kuchora mistari mikuu na midogo ya ustaarabu mpya wa Kiislamu, kuibainisha, kuiendeleza na kujengea utamaduni katika jamii.

Kwa mujibu wa  Shirika la Habari la Hawza, Ayatollah Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika ujumbe wake kwenye kongamano la kimataifa la maadhimisho ya miaka mia moja tangia kuasisiwa upya kwa Hawza ya Kielimu ya Qum, pamoja na kubainisha vipengele na kazi mbalimbali za hawza, alizungumzia masharti ya kufanikisha “hawza inayoongoza na bora zaidi,” ambayo ni mbunifu, yenye ustawi, yenye uelewa wa sasa, inayojibu masuala mapya, yenye maadili, roho ya maendeleo na jihadi, utambulisho wa kimapinduzi, na pia yenye uwezo wa kubuni mifumo ya uendeshaji wa jamii. Alisisitiza kuwa jukumu kuu zaidi la hawza ni "ufikishaji ulio bayana", na moja kati ya vielelezo vyake vikuu ni kuchora mistari mikuu na midogo ya ustaarabu mpya wa Kiislamu, pamoja na kubainisha, kueneza na kuijengea utamaduni ndani ya jamii.

Matini kamili ya ujumbe wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kama ifuatavyo:

بِسْمِ اللهِ الرَّحْمٰنِ الرَّحِيمِ

وَالحَمدُ لِلّهِ رَبِّ العٰالَمِينَ وَ أَفضَلُ الصَّلاةِ وَالسَّلامِ عَلى سَيِّدِنَا مُحَمَّدٍ المُصْطَفَى وَآلِهِ الطَّاهِرِينَ، سِيَّمَا بَقِيَّةِ اللَّهِ فِي الْعَالَمِينَ

Kuchomoza kwa Hawza Tukufu ya Qum mwanzoni mwa karne ya kumi na nne ya Hijria Shamsi), ilikuwa ni tukio lisilo na kifani, lililotokea katikati ya matukio makubwa na yenye uzito mkubwa; matukio ambayo yaliifanya anga ya eneo la Asia ya Magharibi kuwa na giza, na maisha ya mataifa ya eneo hilo yakawa yamevurugika na kuharibika.

Chanzo na sababu ya mashaka haya makubwa na ya muda mrefu ilikuwa ni kuingilia kwa tawala za kibeberu na washindi wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, ambao kwa lengo la kuvamia na kutawala jiografia hii nyeti na yenye rasilimali nyingi ya aridhini, walitumia kila chombo walichokuwa nacho: kwa nguvu za kijeshi, kwa mipango ya kisiasa, kwa rushwa na kuwatumia wasaliti wa ndani, kwa vyombo vya uenezi wa fikra na utamaduni, na kwa kila njia waliyoweza, waliweza kufanikisha malengo yao.

Huko Iraq, waliunda serikali ya Kiingereza na kisha serikali ya kifalme ya vibaraka; katika eneo la Shāmāt, kwa upande mmoja Uingereza na kwa upande mwingine Ufaransa, walitekeleza ukoloni wao kwa kuunda mfumo wa kimadhehebu katika sehemu moja, na kuunda serikali ya kifalme ya ukoo wa kifalme wa Kiingereza katika sehemu nyingine, na kueneza ukandamizaji na mashinikizo dhidi ya watu, hasa Waislamu na wanavyuoni wa dini, kote katika eneo hilo. Huko Iran, walimkuza polepole jangili mwenye ukatili, tamaa, na asiye na utu, na kumfikisha kwenye uwaziri mkuu na hatimaye kwenye ufalme; huko Palestina, walianza mchakato wa kuwahamisha taratibu mawakala wa Kizayuni na kuwaaandalia silaha, na kwa hatua za polepole, wakaandaa mazingira ya kuanzisha donda la saratani katika moyo wa dunia ya Kiislamu.

Kila walipokumbana na upinzani dhidi ya mipango yao ya hatua kwa hatua, iwe ni Iraq, Shamu, Palestina au Iran waliukandamiza. Katika miji kama Najaf, walifikia hatua ya kuwakamata wanavyuoni kwa pamoja na hata kuwapeleka uhamishoni kwa njia ya udhalilishaji maulamaa wakubwa kama Mirzā Nā'inī, Sayyid Abūl-Hasan Isfahānī, na Shaykh Mahdī Khālisī. Pia walifanya msako wa nyumba kwa nyumba kuwasaka wanaume mjahidina. Mataifa yakawa yametishiwa, yamechanganyikiwa, na matumaini yakapotea. Huko Iran, wapiganaji wa jihadi wa Gilan, Tabriz, na Mashhad waliuawa, na wasaidizi wa mikataba ya khiyana wakawekwa madarakani.

Katikati ya matukio kama haya machungu na usiku kama huo usio na mwangaza, ndipo nyota ya Qom ilipochomoza. Mkono wa uwezo wa Mwenyezi Mungu ulimwinua faqihi mkubwa, mcha Mungu na mwenye tajiriba, ili kwa kuhama kwake kuelekea Qom, kuifufua tena hawza iliyokuwa imedorora na kufungwa, na kupanda mche mpya na wenye baraka katika udongo mgumu wa zama hizo zisizo rafiki, karibu na haramu ya binti mtukufu wa Bwana wetu Mūsā bin Jaʿfar (a.s), na kuuweka katika ardhi hiyo yenye mapokezi.

Qom, wakati wa kuwasili kwa Āyatullāh Ḥāʾirī, haikuwa tupu kutokana na uwepo wa maulamaa wakubwa kama vile: Āyatullāh Mīrzā Muḥammad Arbāb na Shaykh Abū al-Qāsim Kabīr pamoja na wengine kadhaa walikuwa wakiishi katika mji huu, lakini ustadi mkubwa wa kuanzisha hawza ya kielimu, yaani kituo cha kukuza elimu, maulamaa, dini na watu wa dini, kwa uzuri wake wote na kwa mipango yake ya kina, iliweza kutoka shakhsiyyah iliyopewa msaada wa mbinguni kama Āyatullāh Ḥājj Shaykh ʿAbd al-Karīm Ḥāʾirī (r.a).

Tajiriba ya miaka minane ya kuanzisha na kuendesha hawza yenye ustawi huko Arāk, pamoja na miaka kadhaa kabla yake ya kuishi kwa ukaribu na kiongozi mkubwa wa Kishia, Mīrzā-ye Shīrāzī huko Sāmarrā, na kushuhudia mipango yake ya kuanzisha na kuendesha hawza ya mji huo, vilikuwa vikimuongoza. Na busara, ujasiri, ari na matumaini vilimpeleka mbele katika njia hii ngumu.

Hawza katika miaka ya mwanzo, kwa ustahamilivu wake wa kiikhlāṣ na kutawakali, iliepuka salama kutoka katika upanga ulioinuliwa wa Reżā Khān aliyekuwa haachii mdogo wala mkubwa kwa lengo la kufuta alama na misingi ya dini; dhalimu huyu muovu aliteketea, na hawza ambayo kwa miaka mingi ilikuwa chini ya mashinikizo ya kiwango cha juu kutoka kwake, ilibakia na ikaendelea kustawi; na kutoka humo, jua kama Bwana wetu Rūḥullāh liliinuka. Hawza ya kielimu ambayo katika kipindi fulani wanafunzi wake kwa ajili ya kuokoa nafsi zao walikuwa wakikimbilia pembezoni mwa mji kabla ya alfajiri ili kujishughulisha na masomo na mijadala, na kurejea usiku katika vyumba vyao vyenye giza ndani ya madrasa, katika kipindi cha miongo minne baada ya hapo, ikawa kituo kilichokuwa kikituma miale ya mapambano dhidi ya ukoo muovu wa Reżā Khān kote Iran, ikiwasisimua wale waliokata tamaa na walioyeyuka mioyo yao, na kuwavuta vijana waliokuwa wameshajitenga ili waingie katika uwanja wa mapambano.

Na hakika ni hawza hii hii ambayo, muda mfupi baada ya kufariki muasisi wake, kwa ujio wa Marja mkubwa wa cheo, Āyatullāh Burūjerdī, ikawa kilele cha elimu, utafiti, na tablighi ya Ushia katika ulimwengu mzima. Na hatimaye ni hawza hii hii ambayo, katika muda wa chini ya miongo sita, ilifikia kiwango cha nguvu ya kiroho na haiba ya kijamii kiasi cha kwamba iliweza, kwa mikono ya watu, kuung’oa kabisa utawala wa kifalme wa khaini, fisadi na fasiki, na baada ya karne nyingi, kuurudisha Uislamu katika nafasi ya utawala wa kisiasa wa nchi kubwa, yenye utamaduni, na iliyojaa vipawa vya kila namna.

Mhitimu wa hawza hii yenye baraka tele ndiye aliyeifanya Iran kuwa mfano wa kupigania Uislamu katika ulimwengu wa Kiislamu, bali kuwa kinara wa dini duniani kote; kwa hotuba zake zenye mvuto wa kinabii, damu ilishinda upanga; kwa busara zake Jamhuri ya Kiislamu ikazaliwa; kwa ujasiri na tawakkul yake, taifa la Iran likasimama kifua mbele mbele ya vitisho na likashinda mengi; na leo, kwa mafunzo na urithi wake, nchi hii inapiga hatua mbele na kuvuka vizingiti katika nyanja nyingi za maisha.

Rehma na radhi za daima za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya mwanzilishi wa hawza hii yenye baraka na adhama, na mti huu mzuri wenye matunda mengi; mtu bora, mjuzi na mwenye baraka, ‘ālim wa dini na aliyejaa utulivu wa yakini Hadhrat Āyatullāh al-‘Uẓmā Hāj Shaykh ‘Abd al-Karīm Hā’irī.

Sasa ni muhimu kusemwa maneno fulani kuhusu masuala kadhaa ambayo yanadhaniwa kuwa na faida kwa kazi ya leo na kesho ya hawza ya kielimu, kwa matumaini kuwa yataisaidia hawza iliyofanikiwa kwa sasa kuifikia hadhi ya kuwa “kinara na bora kabisa”.

Suala la kwanza ni jina la “hawza ya kielimu” na maana yake kwa kina.

Fasihi iliyopo kwa kawaida kuhusu jambo hili ni fupi na haitoshi. Hawza, kinyume na inavyoonyeshwa na fasihi hiyo, si taasisi ya kufundisha na kusomea tu, bali ni mkusanyiko wa elimu, malezi, na kazi za kijamii na kisiasa. Vipengele mbalimbali vya neno hili lenye maana nzito vinaweza kuorodheshwa kwa namna hii:

Kituo cha kielimu chenye taaluma maalum;

Kituo cha kulea nguvu kazi iliyosafishwa kimaadili na yenye uwezo wa kutoa uongozi wa kidini na kimaadili kwenye jamii;

Safu ya mbele ya uwanja wa mapambano dhidi ya vitisho vya maadui katika nyanja mbalimbali;

Kituo cha kuzalisha na kufafanua fikra ya Kiislamu kuhusu mifumo ya kijamii kuanzia mfumo wa kisiasa na muundo wake na maudhui yake, hadi mifumo inayohusu uendeshaji wa nchi, hadi mfumo wa familia na uhusiano wa mtu binafsi kwa mujibu wa fiqhi, falsafa na mfumo wa maadili wa Kiislamu, na huenda pia kilele cha ubunifu wa kimaendeleo na upangaji wa mbele wa mambo ndani ya mfumo wa ujumbe wa Kiislamu wa kimataifa.

Hivi ndivyo vichwa vya mada vinavyotoa maana ya neno “hawza ya kielimu” na kuonesha vipengele vyake vya msingi, au kwa maneno mengine “matarajiwa” kutoka kwayo; na hivi pia ndivyo vipengele ambavyo kuviimarisha na kuviendeleza kunaweza kuifanya hawza kuwa “kinara na bora kabisa” kwa maana halisi, na kutatua changamoto na vitisho vinavyoweza kujitokeza.

Kuhusu kila moja ya vichwa hivi vya mada, kuna hali halisi na pia mitazamo ambayo inaweza kufupishwa kama ifuatavyo:

Kwanza – Kituo cha Kielimu:

Hawza ya Qom ni mrithi wa hazina kubwa ya elimu ya Kishia. Hazina hii, ambayo ni ya kipekee katika aina yake, ni zao la fikra na utafiti wa maelfu ya maulamaa wa dini katika elimu kama vile fiqhi, kalamu, falsafa, tafsiri na hadithi, ndani ya kipindi cha miaka elfu moja.

Kabla ya kugunduliwa kwa elimu za asili katika karne za hivi karibuni, hawza za Kishia zilihesabiwa kuwa ni sehemu ya kushughulikia pia elimu nyinginezo; lakini katika kila zama, mhimili mkuu wa mijadala na utafiti katika hawza umekuwa ni “elimu ya fiqhi”, na baada yake kwa kiwango kidogo, “kalamu, falsafa na hadithi”

Maendeleo ya hatua kwa hatua ya elimu ya fiqhi katika kipindi hiki kirefu, kuanzia zama za Sheikh Tusi hadi enzi ya Muhqiq Hilli, na kutoka hapo hadi kwa Shahid, kisha hadi kwa Muhqiq Ardebili, na kisha hadi kwa Sheikh Ansari na hadi zama za sasa, ni jambo linaloeleweka wazi kwa watu wa fani hii. Kigezo cha maendeleo ya fiqhi ni kuongeza juu ya yaliyopo, yaani uzalishaji wa elimu bora na kuinua kiwango cha elimu pamoja na matokeo mapya ya kielimu. Hata hivyo, leo hii, kwa kuzingatia mageuzi ya haraka na ya kina ya kiakili na kimatendo katika zama za kisasa, hasa katika karne ya hivi karibuni, inafaa kutazama matarajio makubwa zaidi kuhusu maendeleo ya kielimu ya hawza.

Kuhusiana na elimu ya fiqhi, mambo yafuatayo yanastahili kuzingatiwa:

Kwanza, fiqhi ni jibu la dini kwa mahitaji ya kimatendo ya mtu binafsi na jamii. Kwa maendeleo ya kiakili ya vizazi, majibu haya leo yanapaswa kuwa na misingi imara ya fikra na elimu, na wakati huohuo yawe ni yenye kueleweka.

Jambo jingine ni kwamba matukio magumu na mengi katika maisha ya watu leo hii, yanazua maswali ambayo hayajawahi kuwepo, na fiqhi ya kisasa inapaswa kuwa tayari kuyajibu.

Jambo jingine ni kwamba leo hii, kutokana na kuundwa kwa mfumo wa kisiasa wa Kiislamu, swali kuu ni mtazamo wa jumla wa sheria ya Kiislamu kuhusu vipengele vya maisha binafsi na ya kijamii kwa mwanadamu na misingi yake; kutoka katika mtazamo juu ya mwanadamu, nafasi ya mwanadamu, na malengo ya maisha yake, hadi mtazamo kuhusu muundo unaofaa wa jamii ya wanadamu, mtazamo kuhusu siasa na madaraka, mahusiano ya kijamii, familia, jinsia, uadilifu, na vipengele vingine vya maisha. Fatwa ya faqihi katika kila suala inapaswa kuakisi sehemu ya mtazamo huu wa jumla.

Sharti muhimu kwa kufikia sifa hizi ni, kwanza, faqihi awe na maarifa ya kina kuhusu nyanja zote za elimu na maarifa ya Kiislamu katika maeneo yote, na pili, awe na uelewa mzuri wa matokeo ya sasa ya elimu ya kibinadamu na sayansi zinazohusiana na maisha ya mwanadamu.

Inapaswa kufahamika kuwa hazina iliyokusanywa ya elimu katika hawza ina uwezo wa kumfikisha mwanafunzi wa elimu ya dini katika kiwango hiki cha uwezo wa kielimu, kwa masharti kwamba baadhi ya mambo katika mbinu ya sasa ya kazi yataangaliwa kwa jicho la wazi na kushughulikiwa kwa mkono wenye uwezo.

Moja ya mambo haya ni urefu wa kipindi cha masomo. Kipindi cha kusoma kwa mwanafunzi wa hawza kinapitia njia yenye kuibua maswali; mwanafunzi analazimika kujifunza kitabu kikubwa na cha kitaalamu cha ‘ālim mkubwa kama kitabu cha somo. Kitabu hiki kwa hakika kinahusiana na wakati wa kuingia kwake katika hatua ya utafiti wa ijtihadi, na kumkabidhi kitabu hiki kabla ya hatua hiyo, matokeo yake pekee ni kurefusha muda wa kusoma maandiko. Kitabu cha somo kinapaswa kuwa na maudhui na lugha inayofaa kwa mwanafunzi katika kipindi kifupi kabla ya kuingia katika hatua ya utafiti. Jitihada zilizofanikiwa au zisizofanikiwa za watu wakubwa kama Akhund Khurasani, Haj Sheikh Abdulkarim Ha’eri, na Haj Sayyid Sadruddin Sadr za kubadilisha vitabu kama Qawānīn, Rasā’il, na Kifāyah, Durar al-Fawā’id, na Khulāṣat al-Fusūl zilitokana na kuzingatia hitaji hili muhimu, ilhali wao waliishi katika wakati ambapo mwanafunzi hakuwa anakumbwa na mizigo ya kiakili na majukumu ya kimatendo kama ilivyo leo.

Jambo jingine ni suala la vipaumbele vya fiqhi. Leo, kwa kuundwa kwa mfumo wa Kiislamu na kujitokeza kwa suala la utawala kwa mtazamo wa Kiislamu, masuala muhimu yamepewa kipaumbele na hawza ambayo hayakujitokeza huko nyuma; masuala kama vile uhusiano wa serikali na raia wake, na serikali na mataifa mengine, suala la nafy al-sabīl, mfumo wa kiuchumi na misingi yake, misingi maalumu ya mfumo wa Kiislamu, chanzo cha mamlaka kwa mujibu wa Uislamu, nafasi ya wananchi ndani yake, na msimamo wa Kiislamu katika matukio muhimu na dhidi ya mfumo wa kiimla, dhana na maudhui ya uadilifu, na masuala mengine mengi ya msingi, na mengineyo ya kiuhai kwa ajili ya leo na kesho ya nchi, yana kipaumbele na yanasubiri jibu la kifiqihi. (Baadhi ya hayo pia yana sura ya kielimu ya kalām, ambayo inapaswa kujadiliwa katika nafasi yake mahsusi.

Katika mtindo wa sasa wa kazi ya Hawza, katika upande wa fiqhi, hautolewi uangalifu wa kutosha kwa vipaumbele hivi. Wakati mwingine tunaona kuwa baadhi ya ustadi wa kielimu ambao kwa kawaida huwa ni wa kimuundo na wa awali kwa ajili ya kufikia hukumu ya kisheria, au baadhi ya mada za kifiqhi au za kimsingi zisizo katika vipaumbele, humzamisha faqihi na mtafiti katika ladha yake ya kuvutia kiasi kwamba humpeleka kabisa mbali na masuala ya msingi na yenye kipaumbele, na huteketeza fursa zisizoweza kufidiwa na rasilimali za kibinadamu na kifedha, bila ya kutoa msaada wowote katika mazingira magumu ya mashambulizi ya ukafiri kwa ajili ya kubainisha mtindo wa maisha wa Kiislamu na kuuongoza umma.

Ikiwa lengo la kazi ya kielimu ni kujionesha kuwa na fadhila na kutafuta sifa za kielimu na kushindana katika kuonekana kuwa ni mwenye elimu, basi hiyo itakuwa ni mfano wa kitendo cha kidunia na cha kimaada na «اِتَّخَذَ اِلٰهَهُ هَواه» (3).

Pili – Kulea nguvu kazi iliyosafishwa na yenye ufanisi

Hawza ni taasisi ya kuelekea nje. Matokeo ya Hawza katika ngazi zote ni katika huduma ya fikra na utamaduni wa jamii na binadamu. Hawza ina wajibu wa «kufikisha kuliko bayana ». Wigo wa tabligh hii ni mpana mno – kutoka katika maarifa ya juu ya tauhidi hadi majukumu ya mtu binafsi ya kisheria, na kutoka katika kubainisha mfumo wa Kiislamu na muundo wake na majukumu yake hadi mtindo wa maisha, mazingira ya kuishi, ulinzi wa mazingira na wanyama, pamoja na nyanja nyingi na pembe nyingine za maisha ya mwanadamu.

Hawza za kielimu tangu zamani zimejishughulisha na jukumu hili zito, na watu wengi miongoni mwa wahitimu wao katika ngazi mbalimbali za elimu wameelekea katika njia tofauti za tablighi ya dini na wameishi maisha yao katika hilo. Baada ya mapinduzi, taasisi zilianzishwa kwa ajili ya kuleta utaratibu na pengine kuimarisha maudhui ya harakati hizi za tabligh ndani ya Hawza. Huduma zao zenye thamani pamoja na za wahusika wengine wa harakati ya tabligh ya dini hazipaswi kupuuzwa.

Kilicho muhimu ni kufahamu mazingira ya fikra na utamaduni wa jamii, na kuleta uwiano kati ya maudhui ya tabligh na hali halisi ya fikra na utamaduni miongoni mwa watu, hasa vijana. Katika sehemu hii, Hawza ina tatizo. Mamia haya ya makala, majarida, mihadhara ya majlisi na ya televisheni na mfano wake, mbele ya wimbi la upotoshaji wa kimantiki, haviwezi kutekeleza wajibu wa «ufikishaji ulio bayana» kwa namna inavyohitajika na inavyostahili.

Mahali pa vipengele viwili muhimu katika sehemu hii ndani ya Hawza pana upungufu: “elimu” na “utoharifu wa nafsi”.

Kufikisha ujumbe ulio wa kisasa, unaojaza mapengo na unaotimiza malengo ya dini, hakika kunahitaji elimu na mafunzo. Chombo fulani kinapaswa kuwa na jukumu la kazi hii, na kumfundisha mwanafunzi uwezo wa kushawishi, kufahamu mbinu za mazungumzo, uelewa wa namna ya kuwasiliana na fikra za jamii na mazingira ya vyombo vya habari vya kawaida na vya mtandaoni, na nidhamu ya kukabiliana na wapinzani. Kwa mazoezi na mafunzo, katika kipindi kifupi, amwandaye kuingia katika uwanja huu. Kwa upande mmoja, kwa kutumia zana za kisasa, hukusanya upotoshaji wa karibuni zaidi na wa kawaida wa kimantiki na kimaadili na kutoa majibu bora, fasaha na yenye nguvu zaidi kwa kutumia lugha inayoendana na wakati. Kwa upande mwingine, maarifa ya lazima ya dini yanayoendana na hali ya kiutamaduni na kifikra ya sasa yatayarishwe katika sura ya paketi zinazofaa kwa fikra na utamaduni wa kizazi cha vijana, wanafunzi na familia. Muundo huu wa kimaudhui na wa sura, ndio mada muhimu zaidi ya elimu katika sehemu hii.

Katika kazi ya tablighi, kushambulia ni muhimu zaidi kuliko kujitetea. Yale yaliyoelezwa kuhusu kuondoa na kuepusha mashaka na upotoshaji, hayapaswi kuifanya taasisi ya tabligh kusahau jukumu lake la kushambulia imani potofu za utamaduni wa upotofu unaotawala duniani na pengine pia katika nchi yetu. Utamaduni wa Kimagharibi ulio wa kulazimishwa na wa kupandikizwa, kwa kasi inayozidi kuongezeka, unazidi kupotoka na kuharibika. Hawza yenye wanafalsafa na wataalamu wa kalamu haipaswi kujitosheleza kwa kujibu tu maswali bali inapaswa kutoa changamoto za kimawazo dhidi ya upotofu huu na kuwalazimisha wale wanaosababisha upotofu kutoa majibu.

Kuandaa chombo hiki cha kufundisha ni miongoni mwa vipaumbele vya Hawza; huku ni kulea “mujahid wa kiutamaduni”, na kwa kuzingatia harakati za maadui wa dini ambao kwa bidii wapo katika kuandaa nguvu kazi hasa katika baadhi ya nyanja muhimu, jambo hili linapaswa kuchukuliwa kwa umakini mkubwa na kupewa kipaumbele.

Kuitakasha Nafsi: Hitaji Jingine Sambamba na Elimu

Kuitakasha nafsi (تهذیب) ni hitaji jingine muhimu sambamba na elimu. Uadilifu wa nafsi haumaanishi kulea watu waliotengwa au kujitenga na jamii. Sehemu kubwa ya eneo la shughuli za mujahidi wa kiutamaduni ni kuwaalika watu kwenye kujisafisha kimaadili na kufuata maadili ya Kiislamu. Hili haliwezekani ila kwa mwaliko unaotoka kwa mtu anayemiliki hayo anayoyalingania. La sivyo, jitihada hizo zitakuwa hazina athari wala baraka.

Hawza inahitaji kuwa na harakati zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma katika kusisitiza mawaidha ya kimaadili.

Ninyi, wanafunzi na wanavyuoni vijana, bila shaka mnaweza — kwa msaada wa nyoyo safi na ndimi za ukweli — kutekeleza jukumu la kuwaongoza vijana wa kizazi cha leo katika uadilifu wa maadili, mradi tu muanze na nafsi zenu. Ikhlasi katika matendo, pamoja na kuziba milango ya vishawishi vya mali, sifa na madaraka, ndicho kitufe cha kuingia katika upeo wenye harufu nzuri wa kiroho na haki. Na kwa njia hiyo, kazi ngumu ya jihadi ya kiutamaduni huwa jukumu muhimu na harakati yenye athari, katika hali kama hii badala ya kuwa kizuizi cha tabia ya jihadi ya tablighi, hugeuka kuwa chombo cha kuimarisha nia na azma thabiti.

Nasisisitiza kwamba, kamwe ulingo wa tablighi ya dini usitazamwe kama uwanja usio na mpinzani. Na kamwe mtu asipuuze hata sekunde moja tu mapambano dhidi ya maswali na ujanja wa hoja potofu ambazo huwasilishwa mfululizo katika uwanja huo.

Katika sehemu hii, sambamba na kulea watu kwa ajili ya "بلاغ مبین" (ufikishaji wazi wa risala ya dini), ni lazima pia kuzingatia kulea watu kwa ajili ya majukumu maalumu ndani ya mfumo na uongozi wa nchi, pamoja na kulea watu kwa ajili ya kuendesha mambo ya ndani ya Hawza na kutekeleza majukumu yake, jambo ambalo linahitaji mjadala tofauti.

Sehemu ya Tatu – Mstari wa Mbele wa Uwanja wa Mapambano Dhidi ya Vitisho vya Adui katika Nyanja Mbalimbali.

Hili ni mojawapo ya vipengele visivyojulikana sana kuhusu Hawza na kazi za jumuiya ya maulamaa wa dini. Bila shaka, hakuna harakati yoyote ya mageuzi au mapinduzi katika miaka 150 iliyopita Iran na Iraq ambayo haikuongozwa na maulamaa wa dini au ambayo hawakuwapo katika mstari wa mbele wake. Hili ni ishara muhimu sana ya asili ya Hawza.

Katika kipindi chote hiki, kila mara katika kipindi cha ukoloni na dhulma za kiistibdadi, maulamaa wa dini pekee ndio waliotangulia uwanjani na kwa baraka ya msaada wa watu waliweza mara nyingi kumshinda adui. Hakuna mwingine aliyethubutu hata kusema neno, wala kuelewa vyema suala hilo; na ni baada ya kelele za maulamaa ndipo baadhi ya wengine waliweza kuamka na kupaza sauti.

Kasravi, ambaye anahesabika kuwa miongoni mwa mahasimu wakubwa wa maulamaa wa dini, anakiri kuwa mwanzo wa harakati ya mashruta ilitokana na ushirikiano wa busara wa masayyid wawili: Sayyid Bahbahani na Sayyid Tabataba’i. Naam, katika siku hizo ambapo jitu la dhulma lilikuwa limeinua bendera yake nchini Iran, hakuna yeyote ila marjaa na maulamaa aliyethubutu kusema neno.

Mikataba ya aibu katika kipindi hiki yote ilibatilishwa kwa kupinga na kuzuiwa na maulamaa:

Mkataba wa Reuter ulizuiliwa na Haji Mulla Ali Kani, mwanazuoni mkuu wa Tehran;

Mkataba wa Tumbaku ulifutwa kwa fatwa ya Mirzā Shirāzi, marjaa mkuu, kwa msaada wa maulamaa wakubwa wa Iran;

Mkataba wa Vosough-od-Dowleh ulivurugwa kwa kufichuliwa na Mudarris;

Mapambano dhidi ya bidhaa za nguo za kigeni yaliendeshwa kwa ubunifu wa Āghā Najafi Isfahāni, kwa kushirikiana na maulamaa wa Isfahan na kwa msaada wa maulamaa wa Najaf; na mengineyo pia.

Katika miaka hiyo hiyo ambayo Hawza ya Qom ilikuwa inajengwa, baadhi ya maeneo ya Iraq na mipaka ya Iran yalikuwa uwanja wa mapambano ya kivita ya maulamaa dhidi ya vikosi vya uvamizi vya Waingereza. Si wanafunzi na walimu tu, bali baadhi ya maulamaa mashuhuri kama Sayyid Mustafa Kashani na baadhi ya watoto wa marjaa walishiriki katika mapambano hayo; baadhi yao walikuwa mashahidi, na wengi wao walifukuzwa hadi maeneo ya mbali ya makoloni ya Waingereza.

Shughuli za maulamaa wakuu katika suala la Palestina pia — iwe mwanzoni mwa karne wakati sera ya kuwahamisha na kuwapa silaha Wazayuni ilikuwa ikiendeshwa nchini Palestina, au katika miongo ya tatu wakati sehemu kubwa ya Palestina ilikabidhiwa rasmi kwa Wazayuni na serikali bandia ya Kizayuni ikatangazwa — ni sehemu ya mambo ya kujivunia kwa Hawza. Barua na matamko yao kuhusu jambo hili ni miongoni mwa nyaraka za kihistoria zenye thamani kubwa mno.

Nafasi isiyoweza kuchukuliwa na mwingine ya Hawza ya Qom — na baadaye Hawza nyingine za kielimu nchini Iran — katika kuanzisha harakati ya Kiislamu, kuleta mapinduzi, kuelekeza fikra za jamii, na kuwaingiza watu wengi katika uwanja wa harakati, ni miongoni mwa alama mashuhuri za utambulisho wa jihadi wa Hawza. Wanafunzi wa Hawza, wakiwa na akili zenye utendaji na ndimi zenye uwezo wa kueleza, walikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo walioitikia mwito wa Imam mujahidi uliokuwa unavunja nguvu za maadui, na kwa haraka, kwa umakini na kwa kustahimili madhila, waliingia uwanjani na wakaeneza mafundisho ya mapinduzi na kuelekeza fikra za jamii.

Kwa kuwa na ufahamu wa ukweli huu, ndiyo maana Imam wa Marehemu (r.a) katika ujumbe wake wenye maudhui nzito na wa kusisimua aliouelekezaHawza, alimtambua uongozi wa kidini kuwa ndio wa mwanzo katika kujitolea muhanga katika mapinduzi yote ya wananchi na Kiislamu. Na kinyume chake, aliutambua njia ya mashahidi na kazi yao kuwa ni kufikia hakika ya kufaqihi. Katika kauli nyingine, amewasilisha maulamaa kuwa ni wa mwanzo katika uwanja wa jihadi na ulinzi wa taifa na utetezi kwa wanyonge. Kuhusiana na mustakabali wa chuo, ameiweka tumaini lake kubwa kwa wanafunzi wa kidini, waliovutwa na harakati ya mapinduzi na kuamka kwao kulikosababishwa na hamasa hiyo, na ameeleza masikitiko yake juu ya wale ambao, mbali na masuala haya muhimu ya uhai, waliridhika tu na vitabu na masomo yao.

Katika ujumbe huu, mara kadhaa ameashiria juu ya watu wenye mwelekeo wa uzandiki na kupinga maendeleo, na akatoa onyo kuhusu uingiliaji wa adui kupitia uzembe wa watu hao, na kutangaza hatari kuhusu mbinu mpya za kuuza dini. Kwa mtazamo sahihi wa Imam mkubwa, uwindaji wa mkoloni duniani kote wamekaa mkao wa kuwavizia mashujaa wa kidini wenye maarifa ya kisiasa, na wanapanga mikakati ya kupambana na heshima, adhama na ushawishi wa umma wa uongozi wa kidini.

Katika maandiko hayo yenye busara, yaliyoandikwa kwa hisia za maarifa na mapenzi, wasiwasi wa Imam mkubwa unaonekana wazi – kuwa harakati ya uzandiki na uonyeshaji wa ucha-Mungu wa kinafiki huenda ikaitia hawza katika vishawishi vya kutenganisha dini na siasa na shughuli za kijamii, na kuzuia njia sahihi ya maendeleo. Wasiwasi huu unatokana na kuenea kwa mtazamo hatari unaodai kuwa kuingilia kwa hawza katika masuala ya msingi ya watu na kushiriki katika shughuli za kijamii na kisiasa, pamoja na mapambano dhidi ya dhulma na ufisadi, ni kinyume na utakatifu wa dini na heshima ya kiroho yake, na huwashauri viongozi wa kidini kuwa watu wa amani ya jumla na kuepuka hatari za siasa.

Kueneza dhana hii potofu ni zawadi kubwa kwa mawakala wa ukoloni na uistikbari, ambao kila wakati wamepata hasara kutokana na uwepo na ushiriki wa maulamaa wa dini katika medani ya mapambano dhidi yao, na mara kadhaa wameshindwa. Pia ni zawadi kubwa kwa mawakala wa mfumo fisadi, waovu na vibaraka, waliong’olewa kwa harakati ya taifa la Iran chini ya uongozi wa marjaa wa taqlid.

Utakatifu wa dini hujidhihirisha zaidi kuliko mahali popote katika medani za jihadi ya fikra, siasa na kijeshi, na huimarishwa kwa kujitolea na jihadi ya wabebaji wa maarifa ya dini pamoja na kumwaga damu yao safi. Utakatifu wa dini unapaswa kuonekana katika mwenendo wa Mtume Mtukufu (saw), ambaye alipoingia Yathrib, hatua yake ya kwanza ilikuwa kuunda serikali, kupanga jeshi, na kuunganisha uwanja wa siasa na ibada ndani ya msikiti.

Hawza kwa ajili ya kulinda heshima yake ya kiroho na uaminifu kwa falsafa ya kuwepo kwake, kinapaswa kamwe kisitenganishwe na watu, jamii na masuala yao ya msingi, na kiutambue jihadi katika aina zake zote kama jukumu lisiloepukika wakati wa haja.

Hili ndilo neno muhimu ambalo Imam mkubwa amekuwa akilishirikisha mara nyingi na chuo pamoja na wazee wake na wakubwa, na kwa namna maalumu na wanafunzi wa kidini na mafadhili vijana, na kulisisitiza.

Nne – Kituo cha Ushiriki katika Uzalishaji na Ufafanuzi wa Mifumo ya Kijamii

Nchi na jamii za kibinadamu katika nyanja zao zote za kijamii huendeshwa kwa mfumo maalum; aina ya serikali, mbinu ya uongozi (kama ni ya kidikteta au ya mashauriano, n.k.), mfumo wa mahakama na uamuzi wa migogoro, makosa, masuala ya haki au jinai, mfumo wa kiuchumi na kifedha, suala la fedha na mengineyo, mfumo wa kiutawala, mfumo wa biashara, mfumo wa familia, na mengine mengi, yote ni miongoni mwa nyanja za kijamii za nchi ambazo katika jamii mbalimbali duniani huendeshwa kwa njia mbalimbali na kwa mifumo tofauti.

Bila shaka kila mojawapo ya mifumo hii hutegemea msingi wa kifikra – iwe umetokana na fikra za wanafikra na wataalamu, au umetokana na mila na mazoea ya kienyeji na ya kurithi – na imechipuka kutoka humo.

Katika serikali ya Kiislamu, msingi huu na kanuni zake kwa hakika vinapaswa kuchukuliwa kutoka Uislamu na maandiko yake sahihi, na mifumo ya kuendesha jamii itolewe kutoka humo.

Ingawa fiqhi ya Kishia, isipokuwa katika baadhi ya maeneo – kama mlango wa hukumu (باب قضا) – haijajihusisha vya kutosha na kazi hii, lakini kwa baraka ya kaida pana za kifiqhi zilizopatikana kutoka Kitabu na Sunna, na pia kwa msaada wa anuanu za pili (عناوین ثانویه), ina uwezo wa kutosha wa kubuni mifumo mbalimbali ya uendeshaji wa jamii.

Kuhusu asili na chanzo cha serikali, kazi mashuhuri ya Imam Marehemu katika maudhui ya Wilāyat al-Faqīh alipokuwa uhamishoni Najaf, ilikuwa ni mwanzo wa heri na ilifungua mlango wa utafiti kwa mafadhili wa chuo, na baada ya kuundwa kwa Jamhuri ya Kiislamu, vipengele vyake mbalimbali vilikamilishwa kwa nadharia na kwa vitendo. Lakini kazi hii katika mifumo mingi ya kijamii ya nchi bado haijakamilika wala haijapangwa ipasavyo. Pengo hili ni wajibu wa chuo wa kulijaza; hii ni miongoni mwa majukumu ya lazima ya chuo cha kidini. Leo hii, pamoja na kuwepo na uthabiti wa mfumo wa Kiislamu, jukumu la faqihi na fiqhi ni zito. Leo haiwezekani tena, kwa mujibu wa kauli ya Imam Marehemu, kuiangalia fiqhi – kama wafanyavyo wasio na maarifa – kuwa ni kuzama tu katika hukumu za mtu binafsi na ibada. Fiqhi ya kujenga umma haijifungi kwa mipaka ya hukumu za ibada na wajibu wa mtu binafsi.

Bila shaka hawza, kwa ajili ya kubuni na kupanga mifumo ya kijamii, inahitaji kuwa na maarifa ya kutosha kuhusu yale yaliyogunduliwa leo kuhusu mifumo hiyo duniani. Maarifa haya yatamwezesha faqihi kuweza kuchambua yaliyosahihi na yasiyosahihi, na kupata umakinifu wa kiakili wa kutumia matamko ya wazi na ishara zilizomo katika Kitabu na Sunna, ili abuni muundo wa mifumo ya kijamii kwa ajili ya kuendesha jamii kikamilifu kwa msingi wa fikra ya Kiislamu.

Kando ya hawza, pia chuo kikuu cha nchi kina uwezo na wajibu katika hili; hili linaweza kuwa mojawapo ya maeneo ya ushirikiano kati ya hawza na chuo kikuu. Kazi kubwa ya chuo kikuu ni kwamba katika elimu za kijamii zinazohusiana na mifumo ya uongozi na ya wananchi, kupitia mtazamo wa utafiti na uchambuzi, kibaini yaliyo sahihi na yasiyo sahihi miongoni mwa mitazamo iliyopo duniani, na kwa kushirikiana na chuo cha kidini, watoe maudhui ya fikra ya kidini kwa muundo unaofaa.

5. Ubunifu wa Kimaendeleo katika Mfumo wa Ujumbe wa Ulimwengu wa Uislamu

Hili ndilo tumaini lililo kuu zaidi kwa taasisi ya hawza ya kielimu. Huenda likaonekana kuwa ni la kupenda makuu au la kutamani yasiyowezekana. Katika usiku ule wa kihistoria baada ya shambulio la mwaka 1342 Hijria Shamsia dhidi ya Feyziyyeh, ambapo Imam Muasisi (quddisa sirruh) alizungumza katika nyumba yake baada ya swala ya ‘Isha akiwa na kundi dogo la wanafunzi waliokuwa wameshikwa na hofu, kauli yake hiyo ya juu kuwa: “Hawa wataondoka na ninyi mtasalia”, huenda ilionekana kwa baadhi yetu kuwa ni kauli ya kupenda makuu na ya matumaini yasiyo na msingi. Lakini muda ulithibitisha kuwa imani, subira, na tawakkul humng’oa mlima wa vizingiti kutoka mahala pake, na hila za maadui haziwezi kufua dafu mbele ya sunna ya Mwenyezi Mungu.

“Uanzishwaji wa ustaarabu wa Kiislamu” ndilo lengo la juu kabisa la kidunia la Mapinduzi ya Kiislamu; yaani ustaarabu ambao ndani yake, elimu, teknolojia, rasilimali watu, rasilimali asilia, uwezo wote wa binadamu na maendeleo yote ya kibinadamu, pamoja na utawala, siasa, nguvu za kijeshi, na kila kilicho mikononi mwa mwanadamu, vinawekwa katika huduma ya uadilifu wa kijamii, ustawi wa umma, kupunguza tofauti za kitabaka, kukuza malezi ya kiroho, kuinua elimu, kuongeza maarifa ya kimaumbile, na kuimarisha imani.

Ustaarabu wa Kiislamu umejengwa juu ya msingi wa tawhidi na vipengele vyake vya kijamii, kibinafsi na vya kiroho; umejengwa juu ya kuheshimu mwanadamu kwa misingi ya ubinadamu wake – na siyo kwa jinsia, rangi, lugha, kabila wala jiografia – umeegemezwa juu ya uadilifu na vipengele vyake vyote; umeegemezwa juu ya uhuru wa mwanadamu katika nyanja mbalimbali; umeegemezwa juu ya jihadi ya umma katika nyuga zote ambazo zinahitaji kuwepo kwa harakati za jihadi.

Ustaarabu wa Kiislamu uko katika kinyume kabisa na ustaarabu wa kimaada wa sasa. Ustaarabu wa kimaada ulianza kwa ukoloni, kwa kuvamia ardhi za watu na kudharau mataifa dhaifu, kwa mauaji ya halaiki dhidi ya wenyeji wa maeneo mbalimbali, kwa kutumia elimu kama chombo cha kuwakandamiza wengine, kwa dhulma, kwa uongo, kwa kuzalisha tofauti kubwa za kitabaka, na kwa mabavu. Na hatua kwa hatua, ufisadi na kupotoka kwa maadili na kuondoka kwa heshima ya kingono vimepenya ndani yake na kustawi.

Leo hii, mifano ya wazi na iliyokamilika ya ujenzi huu uliojengwa kwa msingi mbovu tunaiona katika nchi za Magharibi na wafuasi wao: vilele vya utajiri sambamba na mabonde ya umasikini na njaa; wanyanyasaji wenye tamaa ya madaraka wakiwadhulumu kila ambaye wanaweza kumdhulumu; matumizi ya elimu kwa ajili ya mauaji ya halaiki; kusambaza ufisadi wa kingono hadi ndani ya familia, hata kwa watoto wadogo; dhulma na ukatili wa hali ya juu kama ilivyoonekana Ghaza na Palestina; na vitisho vya vita kwa sababu ya kuingilia masuala ya wengine, mfano wa mwenendo wa watawala wa Marekani katika nyakati za hivi karibuni.

Ni wazi kabisa kuwa ustaarabu huu wa batili unaelekea kutoweka na utaondolewa; hii ni sunna isiyobadilika ya uumbaji:

 "اِنَّ الباطِلَ كانَ زَهوقاً"; "فَأَمَّا الزَّبَدُ فَيَذهَبُ جُفاءً".

Jukumu letu leo ni, kwanza, kusaidia katika kuubatilisha hii batili, na pili, kuandaa ustaarabu mbadala kwa kiwango cha uwezo wetu, kimtazamo na kivitendo. Kauli ya kwamba "Wengine walishindwa, basi nasi hatuwezi", ni hoja ya kupotosha. Wengine popote waliposonga mbele kwa imani, kwa hesabu makini na kwa uhimili, waliweza na walishinda. Mfano ulio wazi na mbele ya macho yetu ni: Mapinduzi ya Kiislamu na Jamhuri ya Kiislamu.

Katika mapambano haya, kuna majeraha, vipigo, maumivu, na upotevu wa watu na vitu ambavyo lazima vyavumiliwe. Katika hali hiyo, ushindi ni wa hakika. Mtume Mtukufu (saw) aliondoka usiku kwa siri kutoka Makka, huku akiwa amezingirwa na waabudu masanamu, na akajificha pangoni. Lakini baada ya miaka minane alirejea Makka kwa utukufu na mamlaka, na akaitakasa Kaaba dhidi ya masanamu na Makka dhidi ya waabudu masanamu. Katika miaka hii minane, alipitia mateso yasiyo na hesabu, na alipoteza wafuasi kama Hamza, lakini alishinda.

Vita vitakatifu vya miaka minane vya ulinzi wa nchi yetu dhidi ya muungano wa madhalimu na waongo wa kimataifa ni mfano mwingine wa wazi. Hawza kubwa na yenye ufanisi ya leo ya Qom, ambayo mwanzoni ilikumbwa na mitihani mikubwa, ni mfano mwingine unao mbele ya macho yetu; na mifano kama hii inaweza kupatikana kwa wingi.

Hawza ya kielimu katika kipengele hiki inabeba jukumu lenye thamani kubwa, nalo, kwa daraja ya kwanza, ni kuchora mistari mikuu na midogo ya ustaarabu mpya wa Kiislamu, kisha kuufafanua, kuueneza, na kuujengea utamaduni katika jamii. Hili ni miongoni mwa vielelezo bora kabisa vya ufikishaji ulio bayana.

Katika kuchora muundo wa ustaarabu wa Kiislamu, fiqhi kwa namna moja na elimu za kiakili kwa namna nyingine, vina nafasi. Falsafa ya Kiislamu yetu inapaswa kuchora uendelezo wa kijamii kwa masuala yake makuu. Fiqhi yetu nayo, kwa kupanua upeo wake wa kuona na kwa ubunifu katika istinbat, inapaswa kuainisha masuala mapya ya ustaarabu huu na kuweka hukumu zake.

Maelezo ya wazi ya Imam mkubwa (quddisa sirruh) kuhusu fiqhi na mbinu yake katika hawza ya kielimu ni yenye kufungua njia. Katika maelezo haya, mbinu ya istinbat ni ile ile ya fiqhi ya kitamaduni, na kwa tafsiri yake, ni ijtihadi ya Jowahiri; pamoja na hayo, “wakati” na “mahali” ni vipengele viwili vinavyotawala katika ijtihadi. Inawezekana jambo fulani lilikuwa na hukumu katika zama zilizopita, lakini kwa sababu ya mabadiliko ya mahusiano ya kisiasa, kijamii au kiuchumi, sasa likapata hukumu mpya. Mabadiliko haya ya hukumu yanatokana na ukweli kwamba ingawa jambo hilo linaonekana kuwa ni lile lile kama zamani, lakini kwa kuzingatia mabadiliko ya mahusiano ya kisiasa, kijamii na mengineyo, kivitendo limekuwa ni jambo jipya, hivyo linahitaji hukumu mpya.

Zaidi ya hayo, matukio ya mfululizo duniani na maendeleo ya kielimu na kadhalika yanaweza kumfikisha faqihi mwenye ujuzi kwenye uelewa mpya wa dalili ya Qur'ani au Sunna, na kuwa hoja ya kisheria ya kubadilisha hukumu; kama inavyotokea mara nyingi katika kubadilika kwa rai ya mujtahid. Hata hivyo, fiqhi inapaswa kubaki kuwa fiqhi, na uelewa mpya usigeuke kuwa njia ya kupotosha usafi wa sharia.

Kuhusu maana na tafsiri ya dhana ya hawza ya kielimu na maudhui yake ya kina, ninatosheka na haya yaliyosemwa. Na sasa ninasema kwa muhtasari kuhusu hawza ya Qom ambayo sasa imefikia mwaka wake wa mia moja

Hawza ya Qom leo ni hawza hai na yenye kustawi. Kuwapo kwa maelfu ya walimu, waandishi, watafiti, wachapishaji na wanafikra katika elimu za Kiislamu, kuchapishwa kwa majarida ya kielimu na kiutafiti, na uandishi wa makala za kitaalamu na za kijumla, kwa ujumla wake ni hazina kubwa kwa jamii ya leo na ni uwezo mkubwa kwa ajili ya kesho ya nchi na umma. Kuenea kwa masomo ya tafsiri na maadili, na kuongezeka kwa vituo na masomo ya elimu za kiakili, ni nukta ya nguvu ya kipekee ambayo hawza kabla ya Mapinduzi haikuweza kuifikia. Hawza ya Qom haijawahi kuona idadi hii ya wanafunzi na mafasaha wenye fikra.

Ushiriki wa kikamilifu katika nyanja zote za Mapinduzi na hata katika uwanja wa kijeshi, na kutoa mashahidi wa thamani katika kipindi cha utetezi mtakatifu na kabla na baada yake, ni miongoni mwa fahari kubwa za hawza na ni miongoni mwa mema yasiyo na idadi ya Imamu Muasisi. Kufungua njia kuelekea uwanja wa tablighi ya kimataifa na kulea maelfu ya wanaotafuta elimu kutoka mataifa mbalimbali, na kuwapo kwa wahitimu wake katika nchi nyingi ni kazi kubwa na isiyo na mfano ambayo ni lazima kushukuriwa. Kuzingatia kwa mafuqaha wapya masuala ya kisasa yanayohusiana na maisha ya sasa, pamoja na masomo ya fiqhi yanayohusiana nayo, nako kunatoa bishara ya siku za usoni zenye mafanikio na mabadiliko ya kielimu. Mwelekeo wa mafasaha vijana katika kuchunguza kwa kina mambo ya kiutambuzi yaliyomo katika maandiko sahihi ya Kiislamu, hasa Kalamullah al-Majid, ni bishara nyingine ya kushughulikiwa zaidi kwa Qur’ani ndani ya hawza. Kuundwa kwa hawza za kielimu kwa wanawake ni ubunifu muhimu na wenye athari, ambao thawabu yake ya milele hufikia kwa roho takatifu ya Imamu Muasisi. Kwa mtazamo huu, Hawza ya Qom ni mkusanyiko hai na unaoendelea, na huamsha matumaini.

Hata hivyo, matarajio ya kimantiki kwamba Hawza ya Qom iwe hawza inayoongoza na iliyo juu ya zote, yapo mbali kwa kiasi kikubwa na hali ya sasa. Kuzingatia mambo yafuatayo kunaweza kupunguza umbali huo:

ــ Hawza inapaswa kuwa ya kisasa; iendelee kusonga mbele na wakati, bali hata iwe mbele ya wakati.

ــ Kipaumbele kitolewe katika kulea nguvu kazi katika nyanja zote. Njia ya harakati ya taifa hili na siku za usoni za Mapinduzi zitaainishwa na wale ambao leo wanalelewa hawza.

ــ Wanaohusiana na hawza waongeze uhusiano wao na wananchi. Mpango wa kuwepo kwa mafasaha wa hawza miongoni mwa watu na uhusiano wa karibu baina yao uandaliwe.

ــ Wasimamizi wa hawza kwa busara zao wazuie ushawishi mbaya unaowafanya wanazuoni vijana kukata tamaa kuhusu siku za usoni. Leo hii Uislamu, Iran na Ushia vina heshima na hadhi duniani ambayo havijawahi kuwa navyo katika historia. Mwanazuoni kijana asome kwa hisia hii na akue katika mazingira hayo.

ــ Vijana wa jamii wazingatiwe kwa mtazamo wa matumaini na mawasiliano yao yawe kwa mtazamo huu. Sehemu muhimu ya vijana wa leo wana kiwango cha juu cha akili, na licha ya ushawishi wote wa kubomoa fikra na hisia za kidini, bado ni waaminifu kwa dini na ni watetezi wake. Wengi wao pia hawana uhasama wowote dhidi ya dini na Mapinduzi. Wachache mno waliopuuza maonyesho ya kidini, hawapaswi kuifanya hawza itoe tathmini isiyo halisia.

ــ Mitaala ya masomo ya hawza iandikwe kwa namna ambayo fiqhi iwe yenye nuru, inayojibu maswali na ya kisasa, bila shaka ikiwa ya kitaalamu na inayotegemea njia ya ijtihadi; pamoja na falsafa iliyo wazi, yenye mwelekeo wa kijamii, na yenye mtazamo kuhusu muundo wa maisha ya kijamii; sambamba na elimu ya kalamu iliyo thabiti, yenye uwezo wa kushawishi. Haya yote yafundishwe na walimu mahiri, na yaangaziwe na kufanikishwa kwa kuelewa Qur’ani na masomo ya tafsiri.

ــ Zuhudi, taqwa, kujitosheleza, kutokuwa na tamaa kwa kiumbe yeyote asiye Mungu, kutawakali, roho ya maendeleo, na utayari wa kufanya jihadi, ni nasaha za daima za Imamu mkubwa na wakuu wa maadili na maarifa kwa wanafunzi wa hawza, na leo hii pia ninyi vijana wapenzi wa hawza ni walengwa wa nasaha hizo hizo.

ــ Kuhusiana na vyeti vya elimu ya hawza, wosia wangu wa daima ni kwamba cheti kinapaswa kutolewa na hawza yenyewe, na si kituo chochote cha nje ya hawza kwa wahitimu wake. Bila shaka, nafasi za kielimu za hawza zinaweza kubadilishwa majina na kuitwa kwa majina yanayotambulika katika vituo vya elimu vya kitaifa na kimataifa, mfano: shahada ya kwanza, shahada ya uzamili, shahada ya uzamivu ya utafiti (PhD), na mfano wake.

Namalizia hapa maneno yangu, na namuomba Mwenyezi Mungu Aliyetukuka aendeleze izza na adhama ya Uislamu, uimara na uthabiti wa Umma wa Kiislamu, maendeleo na ufanisi wa taifa la Iran, na ufanisi na tija ya hawza za kielimu, na ushindi dhidi ya maadui na wenye chuki na wanaopinga.

Salaamu za Mwenyezi Mungu zimshukie Bwana wetu Baqiyyatullah (a.j.f), na salamu zetu za dhati ziwe juu ya roho za mashahidi na roho takatifu ya Imamu wa Umma.

والسّلام علیکم و رحمة‌الله و برکاته

Sayyid Ali Khamenei

1404/2/8

 (1) Suratul-Furqān, sehemu ya aya ya 43

 (2) Ṣaḥīfah Imām, juzuu ya 21, uk. 273; Ujumbe kwa maulamaa, wanavyuoni wa kidini, walimu, wanafunzi wa elimu ya dini, na maimamu wa Ijumaa na wa jamaa (1367/12/3)

(7) Sūratul-Isrā’, sehemu ya aya ya 81;

(8) Sūratur-Raʿd, sehemu ya aya ya 17;

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha