Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Sayyid Ammar al-Hakim, kiongozi wa harakati ya Hikmah al-Wataniyah nchini Iraq, jana alikutana na Mohammad Kazem Al-Sadiq, balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Baghdad, na kufanya mazungumzo muhimu.
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wawili walibadilishana mawazo kuhusu njia za kuendeleza uhusiano wa karibu zaidi kati ya Iraq na Iran katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kitamaduni na Kiislamu, pamoja na kuimarisha ushirikiano ili kufanikisha maslahi ya pamoja ya mataifa haya mawili jirani.
Sayyid al-Hakim, akizungumzia hali ya kisiasa ya Iraq, alitaja uchaguzi ujao kuwa ni hatua nyeti na yenye kuamua mustakabali wa nchi, akisema: “Uchaguzi huu unaweza kuihamisha Iraq kutoka katika hali ya utulivu tete hadi katika utulivu wa kudumu.”
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kutumia vyema fursa zilizopo na kueleza kuwa kipindi cha sasa ni nukta muhimu katika historia ya kisasa ya Iraq, akihimiza umoja na umakini wa kitaifa ili nchi iweze kupita salama katika hatua hii nyeti.
Kiongozi huyo wa harakati ya Hikmah al-Wataniyah pia aligusia mabadiliko ya kisiasa na kiusalama katika eneo, akisema: “Utulivu wa Mashariki ya Kati ni nguzo kuu ya usalama na utulivu wa kimataifa, na mazungumzo pamoja na kuelewana ndizo njia pekee za kutatua migogoro kati ya mataifa ya eneo hili.”
Al-Hakim vilevile alisisitiza haja ya kuzingatia kwa umakini zaidi suala la Palestina, kuwasaidia wakimbizi, na kuharakisha juhudi za kurejesha ujenzi katika maeneo yaliyoharibiwa na vita.
Kwa upande wake, balozi wa Iran mjini Baghdad, Mohammad Kazem Al-Sadiq, alithibitisha uimara wa uhusiano wa kindugu na wa karibu kati ya Tehran na Baghdad, na akasisitiza utayari kamili wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuendeleza ushirikiano katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kitamaduni.
Maoni yako