Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, siku ya Jumatano tarehe 1 Oktoba, Rais wa Colombia alitangaza kwamba mabalozi wote wa Israel lazima waondoke nchini. Uamuzi huu umetolewa katika mazingira ambayo uhusiano wa kidiplomasia kati ya Bogotá na Tel Aviv ulikuwa tayari umekatwa tangu Mei 2024 kwa amri ya Petro. Aidha, alisisitiza kuwa: “Mkataba wa Biashara Huria na Israel unafutwa mara moja.”
Msimamo huu mkali umechukuliwa kufuatia hatua iliyofanywa na utawala wa Kizayuni ya kuizuia meli ya “Flotilla ya Kimataifa – Sumud”, ambayo ilikuwa imebeba msaada wa chakula na dawa kwa ajili ya wakazi walioko chini ya mzingiro huko Ghaza. Katika tukio hilo, wanaharakati kadhaa wa kimataifa walikamatwa, wakiwemo raia wawili wa Colombia: Manuela Bedoya na Luna Barreto.
Katika ujumbe wake, Petro alimshutumu vikali Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, akisema: “Kama habari hii ni sahihi, basi tunashuhudia uhalifu mpya wa kimataifa unaofanywa na Waziri Mkuu wa Israel, ambaye mara kadhaa nimemuita mhalifu na mfanyaji wa mauaji ya kimbari.”
Pia aliwahitajia wanasheria wa kimataifa kushirikiana na mawakili wa Colombia kufuatilia kisheria kesi hii.
Siku hiyohiyo, kundi dogo la wanaharakati wanaoiunga mkono Palestina lilifanya maandamano katika eneo la kifedha la Bogotá, huku likipaza sauti dhidi ya kukamatwa kwa wanaharakati wa meli ya – Sumud.
Kuhusu kufutwa kwa Mkataba wa Biashara Huria, wataalamu walikumbusha kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 15.4 cha mkataba huo, kila upande una haki ya kuuvunja kwa kuwasilisha noti ya kidiplomasia, na kuvunjwa huko hutekelezwa miezi sita baada ya kupokelewa kwa taarifa rasmi. Mkataba huo ulisainiwa mwaka 2013 na kuanza kutekelezwa rasmi mwezi Agosti 2020.
Petro hapo awali alikuwa tayari amepiga marufuku mauzo ya makaa ya mawe kwenda Israel, ingawa hivi karibuni alikiri kwamba bado kuna meli zinazobeba makaa ya mawe kutoka Colombia kuelekea Israel — jambo ambalo alilitaja kama changamoto kwa serikali yake.
Maoni yako