Alhamisi 16 Oktoba 2025 - 00:03
“Uzayuni wa kisiasa unatumia fikra ya ‘taifa teule’ kwa ajili ya maslahi yake binafsi”

Hawza/ Rais wa zamani wa Kitivo cha Sheriah na Masomo ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Qatar, akizungumza katika kikao cha kielimu kilichobeba anuani isemayo “Maisha ya Kiakhlaqi katika Uislamu na Ukristo”, ameelezea masikitiko yake juu ya mauaji yanayoendelea huko Ghaza na kusisitiza juu ya mambo ya pamoja baina ya dini za Kiibrahimu. Amesema kuwa harakati ya Uzayuni ni mrengo wa kisiasa unaotumia vibaya mambo matakatifu ya kidini kwa manufaa yake binafsi.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Yusuf Mahmoud Al-Siddiqi, rais wa zamani wa Kitivo cha Sheriah na Masomo ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Qatar, siku ya Jumanne tarehe 22 Mehr (sawa na Oktoba 14), katika kikao hicho cha Elimu kilichoandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Falsafa na Itikadi za Kiislamu chini ya Taasisi ya Sayansi na Utamaduni wa Kiislamu katika Kituo cha Mikutano cha Ghadir, Ofisi ya Tabligh ya Hawza ya Qom, alitoa salamu za rambirambi kwa jinai za Ghaza na kusisitiza umuhimu wa mshikamano wa kidini.

Amesema: “Thamani za Kikristo, kinyume na zile za Uyahudi ambazo zimejengwa juu ya kujiona bora na ubaguzi wa kikabila, zinajikita katika udugu wa kimataifa.”

Mwalimu huyo wa Chuo Kikuu cha Qatar aliongeza: “Tabia tunayoishuhudia leo kutoka kwa Wazayuni nchini Israel imetokana na fikra ya ‘Taifa teule’, ingawa inapaswa kutofautisha baina ya Uyahudi na Uzayuni, kwa kuwa baadhi ya Wayahudi wenyewe wanapinga Uzayuni.”

Ubinadamu uliozama katika ujahili licha ya maendeleo ya kimaada

Rais huyo wa zamani wa Kitivo cha Sheriah cha Chuo Kikuu cha Qatar, akigusia maendeleo ya viwanda na mambo ya kimaada, alisema hali ya sasa ya mwanadamu imezama katika ujahili. Akaongeza: “Wote tunapaswa kufikia hitimisho moja kwamba licha ya utofauti wa mitazamo na dini – iwe ya mbinguni au isiyo ya mbinguni – tunapaswa kufikia amani na kuachana na tofauti kwa kushikamana na akili na utashi.”

Tawhidi na maadili ndio nguzo kuu za dini za mbinguni

Al-Siddiqi akifafanua kuhusiana na mambo ya pamoja baina ya dini tatu za mbinguni – Uislamu, Ukristo na Uyahudi – alisema kuwa; jambo kuu linalowaunganisha ni wito wa kumpwekesha Mwenyezi Mungu.

Akaeleza: “Makudiwa ya Qur’ani katika kauli yake kwamba ‘Dini sahihi mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu’, ni kujisalimisha mbele ya Mola, si tu dini ya Uislamu kama mfumo maalum. Hivyo basi, kuna uwezekano wa kuwa na maelewano na dini zisizo za Kiibrahimu katika masuala ya pamoja.”

Akaendelea kusema: “Kuna mambo ya kimaadili na kisheria ya pamoja baina ya dini hizo, kama vile katazo la uzinzi, wizi, kuumiza wengine, pamoja na wito wa maadili, uadilifu na huruma.”

Aidha, alitaja kuachana na mafundisho ya dini kuwa ndio chanzo kikuu cha matukio mabaya duniani.

Umuhimu wa kujenga taaluma ya maadili kwa ajili ya kutatua matatizo ya kibinadamu

Al-Siddiqi alisisitiza umuhimu wa kufahamu mitazamo ya wengine katika enzi hii ya mitandao ya kijamii, akisema: “Dini zote zina orodha ndefu ya maadili na kiroho; tunapaswa kupitia mazungumzo kuielekeza jamii katika ukamilifu wa kibinadamu na kielimu, na kuleta ukaribu baina ya mataifa.”

Akitaja vitendo vya ukosefu wa maadili vinavyoonekana wazi Ghaza na maandamano ya raia wa Marekani na Ulaya dhidi ya utawala wa Kizayuni, alisema maandamano hayo yametokana na thamani za kimaadili zilizopandikizwa ndani ya nafsi za wanadamu.

Akasema: “Lengo kuu la maadili ni kupunguza makosa ya kibinadamu na kuinua mwenendo wa kibinadamu na ustaarabu wa ulimwengu. Wanafikra na viongozi wa kidini wanapaswa kutumia kanuni zinazokubalika za dini katika kushughulikia masuala ya kimataifa, kama vile mashinikizo makubwa dhidi ya Iran.”

Asili ya kisiasa ya Uzayuni na tofauti yake na Uyahudi

Mwalimu huyo wa Chuo Kikuu cha Qatar alibainisha kwamba dini ya Kikristo, tofauti na Uyahudi uliojengwa juu ya kujiona bora, imejikita katika udugu wa kimataifa.

Akasema: “Kinachoonekana leo kutoka kwa Wazayuni ni matumizi mabaya ya dini na harakati ya kisiasa kwa ajili ya manufaa binafsi.” Alisisitiza tena juu ya ulazima wa kutofautisha kati ya Uyahudi na Uzayuni wa kisiasa.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha