Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Akizungumza katika kikao cha pamoja cha wasimamizi wa idara za tabligh (uenezi wa elimu ya dini) kutoka mikoa mbalimbali ya Iran, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Yaavaran Mahdi (aj) huko Jamkaran Qum Iran, Ayatullah Araki alisema:
“Mkutano wa Sharm al-Sheikh ulikuwa uwanja wa wazi wa fedheha kwa viongozi wa baadhi ya nchi. Trump aliwadhalilisha waziwazi viongozi wa mataifa ya Kiislamu ambao kwa miaka mingi wamekuwa watumishi wa Marekani na utawala wa Kizayuni. Rais wa Misri ambaye kwa muda mrefu amekuwa akijitahidi kuidhoofisha harakati ya muqawama, hakuwa na hadhi yoyote mbele ya Trump; alidhalilishwa.”
Ameongeza kuwa ulimwengu mzima uliisifu Iran kwa kukataa kushiriki katika mkutano huo, jambo ambalo linaonesha hadhi na uhuru wa taifa la Kiislamu la Iran.
Silaha ya Adui: Vita vya Kisaikolojia
Ayatullah Araki alisema kuwa silaha kali zaidi ya maadui leo si ya jeshi, bali ni vita vya kisaikolojia.
“Katika uwanja wa kivita wa kijeshi, adui hana nafasi ya kushinda. Lakini kabla ya vita, kupitia propaganda na mashambulizi ya kiakili, husababisha hofu na kukata tamaa. Kazi yetu kama wanatabligh ni kupambana na vita hivi vya kisaikolojia na kuwaonesha maadui kwamba sisi ni taifa lenye nguvu ya kweli.”
Kuwaelimisha Vijana Kuhusiana na Mafanikio ya Mapinduzi
Kiongozi huyo wa kidini alisisitiza umuhimu wa kuwaeleza vijana mafanikio ya Mapinduzi ya Kiislamu na sababu za uadui wa maadui wake.
“Vijana wanapaswa kuelewa kwa nini maadui wanachukia mapinduzi haya, ili imani na ufahamu wao wa kisiasa uwe imara.”
Imani ndio Chanzo cha Nguvu na Kujitegemea
Ayatullah Araki alifafanua kuwa imani ndiyo msingi wa nguvu na ushindi wa jamii:
“Qur’ani inasema: ‘Wala msikate tamaa wala msihuzunike, nanyi mtakuwa juu ikiwa mna imani.’ Imani humfanya mwanadamu awe jasiri na jamii iwe imara.”
Vita vya Kwanza vya Kiislamu ni Shule ya Imani na Ujasiri
Akizungumzia historia ya Uislamu, alisema:
“Vita vya Khaybar na Ahzab havikuwa tu mapambano ya kijeshi, bali ilikuwa shule ya imani, subira, na hekima. Tunapaswa kuifundisha historia hii kwa vijana ili waone jinsi waumini wa mwanzo walivyoshinda kupitia tawakkul (kutegemea Mungu).”
Kufanya Kazi kwa Nia Safi ni Siri ya Mafanikio
Ayatullah Araki alisema kuwa; kazi ya kidini na kijamii lazima ifanywe kwa ajili ya Mola pekee:
“Iwapo kazi zetu za tabligh zitakuwa kwa ajili ya Mungu, basi Yeye atatupa nguvu na taufiki. Nia safi ndiyo siri ya mafanikio.”
Yakin (Uhakika) na kumtii Imam ndio Msingi wa Harakati
Amesema msingi wa mfumo wa kielimu na kiitikadi wa Kiislamu ni yakin (uhakika) na utii kwa Imam na uongozi wa Kiislamu.
“Ikiwa tutasimama juu ya uhakika, adui hawezi kutushinda hata katika vita vya kisaikolojia. Ni wajibu wetu kuendeleza mapambano ya kiakili na kitamaduni kwa kujiegemeza kwenye imani na misingi ya mafundo ya Kiislamu.”
Mwito kwa Mubalighi na Walezi wa Kiislamu
Mwisho, Ayatullah Araki aliwataka mubalighina na viongozi wa sekta za kidini kupanga mikakati madhubuti ya kuwaelimisha vijana juu ya thamani za Mapinduzi ya Kiislamu, historia ya Uislamu na uwezo wa taifa la Iran:
“Jengeni ngome thabiti ya kitamaduni na kiroho ili kukabiliana na vita vya kisaikolojia vya maadui.”
Mwisho wa taarifa.
Maoni yako