Ijumaa 19 Desemba 2025 - 06:00
Kauli za Chuki Dhidi ya Uislamu Zalaaniwa Vikali Nchini Marekani

Hawza/ Kauli za chuki dhidi ya Waislamu zilizotolewa na maafisa wawili wa chama cha Republican cha Marekani, ikiwemo wito wa kupiga marufuku kuingia kwa Waislamu na hata kuwafukuza Waislamu, zimelaaniwa vikali na taasisi za Kiislamu. Wakosoaji wamezitaja kauli hizi kuwa ni hatari, za kibaguzi na zinazokinzana na maadili ya Marekani.

Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, kufuatia kauli kali za maafisa wawili wa chama cha Republican cha Marekani kuhusu Waislamu, jumuiya za Kiislamu nchini humo zimetoa taarifa za kulaani vikali kauli hizo.

Randy Fine, mwakilishi wa jimbo la Florida, na Tommy Tuberville, seneta wa jimbo la Alabama, wametoa wito wa kupiga marufuku kuingia Waislamu nchini Marekani na hata kuwafukuza Waislamu wanaoishi ndani ya ardhi ya Marekani; kauli ambazo zinawasilisha Uislamu kama tishio kwa usalama na umoja wa kitaifa wa Marekani.

Misimamo hii imeibua mitazamo tofauti miongoni mwa wanasiasa. Alexandria Ocasio-Cortez amezitaja kauli za Randy Fine kuwa “zinachukiza”, na Chuck Schumer, Chris Murphy na Patty Murray pia wamezielezea kauli hizo kuwa “hatari”, “duni” na zinazopingana na maadili ya Kimarekani. Wamesisitiza kwamba; kauli hizi haziwezi kuhalalishwa kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza, bali ni sehemu ya mkakati wa kisiasa unaojengwa juu ya hofu na unyanyapaa.

Baraza la Mahusiano ya Kiislamu na Marekani (CAIR) pia limekosoa kauli hizo, likimtaja Tommy Tuberville kuwa mwenye misimamo ya chuki dhidi ya Waislamu, na kusisitiza kwamba; aina hii ya kauli huongeza ubaguzi na hatari dhidi ya jamii ya Waislamu wa Marekani.

Tukio hili limetokea katika mwendelezo wa hali ya mvutano wa kisiasa unaowahusu Waislamu nchini Marekani, hali inayokumbusha sera ya “marufuku ya safari kwa Waislamu” wakati wa urais wa Donald Trump pamoja na kauli zake za hivi karibuni.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha