Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, kuongezeka kwa operesheni zilizotekelezwa hivi karibuni na kundi la Daesh nchini Syria kunaashiria tahadhari ya kuanza kwa awamu ya kurejea kwa shughuli za kundi hili; hali hii inajiri katika kipindi nyeti na cha mpito baada ya kuanguka kwa serikali ya awali… Je, viongozi wapya watakabiliana vipi na changamoto ya misimamo mikali?
Mwaka mmoja baada ya kuanguka kwa serikali ya awali ya Bashar al-Assad, dalili za kutia wasiwasi za kurejea kwa shughuli za kundi la kigaidi “Daesh” zimejitokeza katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa serikali mpya ya Syria. Kundi hili linatumia vibaya kipindi cha mpito wa kisiasa na kiusalama, pamoja na hitaji la viongozi wapya la kuziba upungufu wa rasilimali watu katika taasisi za usalama na jeshi.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, viashitia vinazohusishwa na kundi hili viliweza kuonekana wakati wa kusambaratika kwa serikali ya awali na kuelekea maeneo ya kaskazini-magharibi mwa nchi, hasa Idlib. Kwa kunufaika na operesheni pana za uajiri zilizotekelezwa kwa ajili ya kuanzisha kwa haraka utawala katika majimbo, waliweza kupenya ndani ya safu za vikosi vya usalama wa umma na jeshi jipya.
Operesheni maalumu za kuleta machafuko katika uwanja wa usalama
Ripoti zinaonesha kuwa watu hawa wameanza kutumia uwepo wao ndani ya taasisi za usalama kutekeleza operesheni zilizopangwa kwa uangalifu, kwa lengo la kuvuruga uthabiti na kuwapa changamoto viongozi wapya mbele ya jumuiya ya kimataifa; jumuiya ambayo imeonesha wazi uungaji mkono wa kuimarisha utawala mpya.
Hivi karibuni, kundi hili lilitekeleza operesheni mbili zilizoelezwa kuwa hatari zaidi tangia kuanguka kwa serikali ya awali. Operesheni ya kwanza ilitokea katika mji wa Tadmur, na kusababisha kuuawa kwa askari wawili wa Marekani na raia mmoja. Operesheni ya pili ilifanyika kwenye barabara kuu ya kimataifa Aleppo–Damascus, karibu na Ma‘arrat al-Nu‘man, ambapo shambulio la kuvizia liliua wanachama wanne wa vikosi vya usalama wa umma.
Vilevile, kusimamishwa kwa vituo vya ukaguzi vinavyohama na watu wa kundi la kigaidi Daesh kumeripotiwa katika maeneo mbalimbali ya viunga vya Damascus na Idlib, vikilenga wanajeshi wa Syria; hatua hizi zimefanywa kwa jaribio la kuleta hali ya kutokuwepo kwa uthabiti wa kiusalama na kuonesha kushindwa kwa viongozi kudhibiti maeneo nyeti.
Sambamba na tishio linalotokana na Daesh waliopenya ndani ya taasisi za usalama, vyanzo vya taarifa na wachambuzi wanaripoti kuwepo kwa “kundi” ndani ya muundo wa kijeshi linalohusishwa na viongozi wa sasa, linalotuhumiwa kwa kuchukua msimamo wa uzembe au kutounga mkono moja kwa moja harakati za kundi hili.
Kwa mujibu wa vyanzo hivi, kundi hilo lina wasiwasi kuhusu kukaribiana kunakozidi kati ya viongozi wapya wa Syria na Marekani, hasa katika uwanja wa uratibu wa kiusalama na vikosi vya muungano wa kimataifa. Wasiwasi huu unatokana na ukweli kwamba muungano huo umejikita katika kuwafuatilia na kuwaangamiza viongozi wa zamani ambao walikuwa wakifanya kazi chini ya mwamvuli wa uhusiano na “Daesh” ndani ya safu za “Jabhat al-Nusra” au “Jund al-Aqsa”.
Kwa mtazamo wa pande hizi, mkabala huu unachukuliwa kama chombo cha kusuluhisha hesabu za zamani na kuchora upya mizani ya nguvu katika uwanja wa kijeshi; wanaamini kuwa viongozi wa sasa, kwa kurahisisha kazi ya vikosi vya muungano, wanakiuka makubaliano ya ndani ambayo yalisaidia kuimarisha udhibiti wao baada ya kuanguka kwa serikali ya awali.
Tafsiri hii inaonyesha kuwa mgawanyiko huu ndani ya mrengo wa kijeshi unaweka changamoto nyingine mbele ya uongozi wa kisiasa, huku viongozi wakijitahidi kuimarisha utawala wa rais wa mpito, Ahmad al-Sharaa (al-Joulani), na kupata uungwaji mkono wa kimataifa wa kudumu ili kuhakikisha uthabiti wa kiusalama na kujenga upya taasisi za dola.
Wachambuzi wanaamini kuwa; kuendelea kwa mipasuko hii, ikiwa hakutashughulikiwa, kunaweza kuunda mazingira mwafaka kwa upenyezaji mpya wa kiusalama, iwe ni wa “Daesh” au wa makundi mengine yenye misimamo mikali. Hali hii inawaweka viongozi mbele ya utata unaohitaji kusawazisha matakwa ya ushirikiano wa kimataifa na ulazima wa kuhifadhi mshikamano wa taasisi zao za usalama na kijeshi.
Malengo ya kundi na changamoto za awamu
Waangalizi wanaamini kuwa “Daesh”, kupitia harakati hizi, inalenga kufikia malengo kadhaa; yaliyo muhimu zaidi ni kudhoofisha hali ya uthabiti wa kiasi fulani, kupiga pigo imani ya kimataifa kwa serikali mpya, na kujifafanua upya kama mdau mwenye uwezo wa kuathiri uwanja wa Syria, kwa kutumia udhaifu na ugumu wa awamu ya mpito.
Kwa upande mwingine, taarifa za “Al-Mayadeen” zinaonesha kuwa viongozi wa Syria kwa sasa wameanza kutekeleza hatua kali za kiusalama. Hatua hizi zinajumuisha kuanzisha operesheni pana za kukagua historia na rekodi za watu ambao wamejiunga nao hivi karibuni, pamoja na kuandaa mifumo mikali zaidi ya ukaguzi wa kiusalama na kijasusi, na kufanya tafiti mpya kuhusu mafaili ya wafanyakazi.
Hatua hizi zinafanyika katika muktadha wa juhudi zilizo wazi za “kusafisha safu” na kuzuia kujirudia kwa upenyezaji, kwani kuna uelewa rasmi kwamba hatari ya kundi hili la kigaidi haitishii tu taasisi za usalama, bali pia amani ya kijamii na uthabiti wa jumla wa nchi.
Wafuatiliaji wa masuala haya wanatabiri kuwa mafanikio ya viongozi katika kutatua changamoto hii yatakuwa jaribio muhimu kwa uwezo wao wa kuvuka kutoka hatua ya kuimarisha udhibiti kuelekea kuunda dola yenye uthabiti; dola itakayoweza kudhibiti vitisho vya ndani na kuzuia taasisi zake kutumiwa vibaya na mashirika yenye misimamo mikali.
Maoni yako